Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii ndiyo barua ya kung’atuka Mangula kwa Mwenyekiti wa CCM

Baruaapic Mangula Rais Samia akiwa na Makamu mstaafu wa CCM, Philip Mangula

Fri, 1 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amesoma barua ya kumg’atuka kwa makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula leo Ijumaa Aprili 1, 2022 mbele ya Mkutano Mkuu unaoendelea mjini Dodoma. Akisoma barua hiyo Mzee Mangula anaadika……

BARUA YA KUNG’ATUKA NAFASI YA MAKAMU MWENYEKITI WA CHAMA –TANZANIA BARA

Tafadhari rejea kichwa cha habari hapo juu,

Kwa heshima na taadhima naomba kukujulisha kuwa, nimeamua kung’atuka nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara. Uamuzi huu umetokana na sababu zangu binafsi zikiwamo za umri na utumishi wa muda mrefu, zimesababisha kutotimiza majukumu yangu kikamilifu.

Umri wangu ifikapo Machi 31, 2022 (jana) nitatimiza miaka 81. Nimeanza utumishi tangu Januari Mosi 1962. Nilianza kazi ya ualimu katika chama.

Niliteuliwa kuwa mwalimu wa siasa mwaka 1968 baada ya kamati kuu ya chama kuteua makada 75 walioandaliwa kwa kazi ya kutoa mafunzo kuhusu siasa ya chama na pia kuhusu ujenzi wa chama. Mwaka 1969 niliteuliwa na chama kuwa miongoni mwa walimu katika chuo cha Tanu Kivukoni.

Advertisement Nilikuwa mhariri wa majarida mawili yaliyokuwa yakitolewa na chuo hicho kila baada ya miezi mitatu. Majalida hayo ni Ujamaa na Mbioni. Niliendesha mafunzo ya masafa katika Radio Tanzania kupitia vipindi vya Fimbo ya Mnyonge kilichohusu ujenzi wa ujamaa vijijini na kingine kuhusu ukombozi kusini mwa Afrika kilichoitwa ‘THE RATIONAL CHOICE’.

Nilikuwa mwalimu mshauri wa wanachuo katika chuo hicho na baadaye Kamati Kuu ya Tanu iliteua kuwa makamu mkuu wa chuo kwa miaka sita. Niliteuliwa kuwa katibu wa chama wa wilaya na mkuu wa wilaya. Baadaye niliteuliwa kuwa katibu wa chama wa mkoa na kisha mkuu wa mkoa kwa miaka 11 kabla sijachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM kwa miaka 10.

Nimekuwa makamu mwenyekiti wa chama kwa miaka kumi sasa. Huu ni wakati muafaka wa kupanga na kusuka timu ya kukiimarisha chama kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya 2020-2025.

Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mwenyekiti wa CCM Taifa, mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Sekretarieti ya Taifa ya CCM, Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya CCM pamoja na wanachama wote wa CCM.

Ushirikiano mlionipatia katika kipindi changu cha kushika nafasi hii kuliniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi na amani. Naomba kuwahakikishia kwamba nitaendelea kuwa mwanachama mtiifu na mwadilifu kwa chama chetu cha mapinduzi na raia mwema wa Tanzania.

Aidha, kufuatia uamuzi wangu huo wa kung’atuka katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, nafasi hiyo itakuwa wazi hivyo nashauri achaguliwe mwanachama mwingine wa CCM wa kujaza nafasi tajwa kwa mujibu wa katiba ya chama chetu.

Kidumu Chama cha Mapinduzi

Philip Japhet Mangula

Chanzo: www.tanzaniaweb.live