Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hesabu za CCM kurejesha vigogo kundini zimelenga mwaka 2020

33945 Pic+ccm Tanzania Web Photo

Sat, 29 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Machi mwaka jana makada 12 wa CCM walivuliwa uanachama jijini Dodoma kupitia Mkutano Mkuu wa chama hicho huku wengine wakipewa onyo kali kwa sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni usaliti katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Kwa mujibu wa chama hicho, makada hao walikutwa na makosa ya maadili kinyume na katiba na kanuni za uongozi na maadili za chama hicho.

Vigogo kati ya hao waliotimuliwa walikuwa ni wenyekiti wa zamani wa CCM, Ramadhani Madabida (Dar es Salaam), Erasto Kwirasa (Shinyanga), Christopher Sanya(Mara) na Jesca Msambatavangu(Iringa) na Salum Madenge(Kinondoni).

Katika sakata hilo, kada mkongwe Sophia Simba alipoteza nafasi ya Uenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na ubunge wa viti maalumu kabla ya kurejeshwa Novemba mwaka jana huku Adam Kimbisa akisamehewa na Emmanuel Nchimbi akipewa onyo kali.

Hata hivyo, mwaka mmoja baada ya kumrejesha Sophia Simba, Halmashauri Kuu ya chama hicho Desemba 18, mwaka huu, imetangaza kuwasamehe na kuwarejeshea uanachama Ramadhani Madabida, Erasto Kwirasa, Christopher Sanya, na Salum Madenge huku Jesca Msambatavangu(Iringa) akiwekwa chini ya uangalizi usiokuwa na ukomo.

Nec chini ya mwenyekiti ambaye ni Rais John Magufuli, ilifikia uamuzi huo baada ya kupokea barua za wanachama hao wakiomba msamaha kwa makosa ya kimaadili waliyoyafanya 2015 wakiwa madarakani.

Uamuzi huo ni hesabu sahihi na unatafsiri nini kwa chama hicho tawala wakati wa Taifa likielekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020?

Wakili na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Dk Onesmo Kyauke anasema uamuzi huo ni hesabu sahihi kwa chama hicho kutokana na ushawishi wa kila mmoja ndani ya mkoa anaotoka.

Dk Kyauke anasema kabla ya kurejesha kwa wanachama hao, yako maeneo ya kiutafiti yaliyofanywa na chama hicho ili kuwa na matokeo chanya yanayoongeza mtaji wa kisiasa ndani ya chama hicho.

“Siyo kila anayeomba msamaha anaweza kuruhusiwa, ila wanaangalia nani anayeomba na atakuwa na mchango gani ndani ya chama, au wanaweza kukuweka chini ya uangalizi hadi watakapojiridhisha umuhimu na mchango wako kama hautakuwa na madhara ya mpasuko,” anasema Dk Kyauke.

Mkuu wa Kitivo cha sayansi ya Sanaa kutoka Chuo Kikuu cha Tumain Tawi la Dar es Salaam, Dk James Kazoka anasema uamuzi huo unaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa vyama vingine vya siasa pale inapotokea mwanachama kajirekebisha anastahili kurejeshwa kundini.

“Ni jambo jema kwa sababu kama mwana mpotevu (mwanachama) alipotea, lakini akaamua kurejea na kutubu basi hilo ni jambo jema. Na kama mzazi (Chama) ameona wale wamejirekebisha ni kumpokea, kwa hiyo CCM kimetafakari na kimeona kiwarejeshe na ukiangalia CCM ni chama tawala inatakiwa kuonyesha mfano mzuri,” anasema Dk Kazoka.

Mitandao, udhaifu

Pamoja na hesabu hizo, wachambuzi wanasema mtandao wa kuimarisha CCM ndani na nje ni changamoto.

Licha ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally kutoweka wazi sababu za kimkakati za kuwarejesha vigogo hao, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino(Sauti), Profesa Mwesiga Baregu, anasema uamuzi huo ni mkakati wa kupunguza nyufa ndani ya CCM.

“Mfano ni suala la Membe (Bernard Membe), lakini hayuko peke yake , kuna washindani wengine wa Magufuli (Rais John Magufuli), wanaotaka kuwania kuteuliwa, kwa hiyo inaonekana kwamba, adui ni bora uwe naye karibu kuliko akiwa mbali.” anasema Profesa Baregu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema.

“Crisis nyingine inatokana na kundi la wanachama ambao hawaridhishwi na uamuzi wa uongozi kuwapitisha bila kupingwa wale wanaojiunga CCM wakitokea upinzani, kwa hiyo wanajaribu kupunguza makali ili kurejesha utulivu, jambo ambalo sidhani kama itawezekana.”

Tafsiri nyingine ya kurejeshwa kwa wanachama hao ni pamoja na kubaini maamuzi ya kuwafukuza wanachama hao mwaka jana hayakuwa makini. “Lakini tafsiri ya nne ni kuhofia viongozi wa vyama vya upinzani wanavyounganisha nguvu ya pamoja kwa sasa, vikao hivyo ni tishio kwa CCM.”

Profesa Baregu anasema CCM inasumbuliwa na udhaifu katika utayari wa kuendesha mikutano ya kutafuta maridhiano ya kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu ujao chini ya Taasisi ya The Mwalimu Nyerere Foundation.

“Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, taasisi hiyo iliona uchaguzi mkuu ujao unaweza kuchafuka endapo tukienda bila marekebisho katika sheria kadhaa, waliendesha vikao na vyama vyote lakini baadaye wakasitisha kwa kuonekana siyo mkakati wa CCM, kwa hiyo inaongeza nyufa kwani wapo waliokuwa wanaunga mkono,” anasema Profesa Baregu.

Uzani kwa waliobakia

Hii ina maana ya kwamba, sita kati ya 12 ambao hawakuwasilisha barua ya kuomba msamaha, wanatoka ngazi ya wilaya. Watano kati ya hao sita ambao hawajarejeshwa kundini wanatoka ukanda wa Kaskazini.

Wanasiasa hao ni wenyeviti wa zamani wa wilaya; Makolo Leizer(Longido), Wilfred Molel(Arusha Mjini) Omary Awadhi(Gairo), Ally Msuya(Babati mjini) na wajumbe wawili wa NEC, Mathias Manga(Arumeru) Ally Sumaye(Babati mjini).

Katibu wa NEC ya CCM, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Mstaafu, Ngemela Lubinga anasema wanachama sita ambao hawajarejesehwa uanachama, hawatakuwa na athari kwenye chama.

“Kila mtu anajipima, kuomba msamaha ni matakwa ya mtu binafsi, na walioomba walisamehewa lakini siyo wote, kwa mfano Jesca hakukubarika, akapewa muda achunguzwe zaidi kwa hiyo suala la athari lipo lakini ni very miner…maana hata ukiwa unakula chakula ukijing’ata ni athari, ni very miner(athari ndogo sana) kwenye chakula,” anasema Kanali Lubinga.



Chanzo: mwananchi.co.tz