Dodoma. Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema) John Heche ametaka Waziri wa Fedha na Mpango Dk Philip Mpango kueleza ni vipi wametekeleza ahadi sita walizozitoa katika uchaguzi mkuu 2015 ikiwemo kutoa Sh50 milioni kwa kila kijiji.
Akichangia mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni, leo Jumatano Juni 19, 2019, Heche amesema hii ni bajeti ya nne ya awamu ya tano.
Amesema bajeti ya mwakani itakuwa sio ya kwao kwa sababu Serikali itakayokuja kutekeleza ni ya awamu ya sita ambayo CCM kwa imani yake watakuwa wametoka madarakani.
“Tuko hapa kwa ajili ya kuwakumbushia ahadi mlizoahidi wakati wa uchaguzi, mojawapo ya ahadi ni kuwa mtapeleka milioni 50 iko wapi hiyo Sh50?”amehoji.
Ahadi nyingine aliyoizungumzia ni pesheni kwa wazee ambayo bado haijatekelezwa na kutaka waizungumzie maana waliitaja katika ilani ya uchaguzi.
“Hampaswi kuchaguliwa hata kijiji kimoja kwasababu hamstahili. Mliahidi pia kuongeza ajira,”amesema.
Pia Soma
- Rais Magufuli kuongoza kongamano la korosho Mtwara
- Watoto 15 wenye vichwa vikubwa kuwafanyia upasuaji MOI
- Mzumbe kuadhimisha wiki ya utumishi kwa kutatua changamoto mbalimbali
“Tunaenda mbele nyuma mnapaswa kuchaguliwa ama la. Mmepunguza ajira ya zaidi ya 30,000,”amesema.
Amesema wazazi wamejikamua na kuwasomesha watoto wao katika vyuo mbalimbali vya ualimu nchini.
Heche amesema tangu mwaka 2015 wanafunzi waliomaliza katika vyuo mbalimbali vya ualimu walikuwa ni 75,000 na kuhoji ni wangapi walioajiriwa.
“Unatembelea VX na sisi tunalipwa fedha. Tueleze mnapaswa kuchaguliwa. Mnawaacha mtaani mnawaambia waendelee kula mtori nyama ziko chini. Tunataka majibu ni fedha za walipa kodi utuambie unatoa lini ajira,”amesema.
Heche amesema pia wameahidi kuwa wataongeza mishahara na kupunguza kodi katika mishahara (PAYE) lakini hawajatekeleza ahadi hiyo.
Pia Heche amemtaka Dk Mpango amjibu kuwa mradi wa kufua umeme wa maji wa Stiglers Gorge ambao amesema utatumia Sh7 trilioni hadi kukamilika utatumia miaka mingapi kuzalisha megawati 2100.