Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatma ya Balozi Karume kufukuzwa CCM ipo mikononi mwa Rais Samia

Karume 4372595 Balozi Karume

Sun, 9 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kusini Unguja kwa kauli moja imependekeza kumfukuza uanachama kada na mwanachama mkongwe wa Chama hicho, Balozi Ali Abeid Karume kutokana na mwenendo wake wa kukiuka maelekezo ya maadili, miongozo na nidhamu iliyoainishwa katika Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022.

Akizungumza mara baada ya kutolewa maazimio ya kikao hicho Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa huo, Ali Timamu Haji, alisema maamuzi hayo yamefikiwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 ibara ya 89 inayoeleza kazi za Halmashauri Kuu ya Mkoa inayoelekeza kuangalia mienendo ya wanachama na viongozi wa CCM wa ngazi ya Mkoa kichama na kulazimika kutoa taarifa kwa vikao vinavyohusika ngazi za juu.

Pia Ibara ndogo ya 14 kifungu kidogo cha 14 kinaelekeza kumuachisha au kumfukuza uanachama mwanachama yeyote endapo itaridhika kwamba tabia na mwenendo wake vinamuondolea sifa za uanachama wake na mwanachama anayeachishwa au kufukuzwa uanachama anaweza kukata rufaa kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Katika maelezo yake Katibu wa Siasa na Uenezi, Ali Timamu, alifafanua kuwa Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa huo imeridhia na kuridhika kwamba kutokana na kauli na vitendo vya mwanachama huyo, Ali Abeid Amani Karume imekubali kumuachisha uanachama wa CCM na kumtaka arudishe kadi ya uanachama wa CCM ya kielektroniki namba C000/2809/993/1 ya tarehe 17/03/2022.

Hata hivyo, hatima ya uanachama kwa kubariki kufukuzwa ama kusalia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kada huyo imebaki mikononi mwa Mwenyekiti wa chama hicho Rais Samia Suluhu Hassan.

Hatua hiyo ni baada ya Halmashauri Kuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kusini Unguja kutangaza kutoa mapendekezo ya kumfuta uanachama kada wake, Balozi Karume.

Vikao vya ngazi ya juu ya CCM vimeanza jana jijini Dodoma na kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar, kilichokaa juzi chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live