Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hamahama ya vyama yampa ukakasi Nape

Sat, 18 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati joto la wapinzani kuhamia CCM likiendelea kuwa juu, Mbunge wa Mtama kupitia chama hicho, Nape Nnauye amesema suala hilo lina ukakasi akitaka itungwe sheria itakayosimamia mchakato huo.

Nape aliyasema hayo juzi wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge.

“Ifikie mahali turuhusu mtu akihama chama, ahame na ubunge wake au na cheo chake alichonacho,” alisema.

“Hii kitu ina ukakasi, ingawa haivunji sheria, lakini ina ukakasi na kama ina ukakasi ni vizuri tukatengeneza forum (jukwaa) kwa ajili ya kusimamia sheria za mchezo huo katika mfumo wa vyama vingi.”

Alisema suala hilo ni msimamo wake wa siku nyingi na ni vyema likaangaliwa kwa kiasi gani linaimarisha demokrasia nchini.

Nape alisema ni vizuri kuangalia ni kwa kiasi gani ‘hamahama’ hiyo italinda kura zilizopigwa na wananchi walipomchagua mwakilishi wao.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, kumekuwapo na wimbi la madiwani na wabunge wa upinzani kuhamia CCM, jambo lililosababisha kufanyika uchaguzi mdogo mara nne, wa hivi karibuni ukiwa ni ule wa Agosti 12.

Wabunge waliohamia CCM na vyama walivyotoka ni Mwita Waitara aliyekuwa mbunge wa Ukonga (Chadema); Julius Kalanga (Monduli-Chadema); Dk Godwin Mollel (Chadema-Siha) na Zuberi Kuchauka (CUF-Liwale) na Maulid Mtulia (CUF- Kinondoni).

Pia yumo Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini) aliyetoka CCM kwenda Chadema.

Hata hivyo, Mollel na Mtulia walipitishwa na CCM kugombea tena katika majimbo hayo na kushinda, huku Kalanga na Waitara wakiwa tayari wamepitishwa na chama hicho katika majimbo hayo.

Pia aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro naye amehamia CCM hivi karibuni.

Kadhalika ‘hamahama’ hiyo imesababisha uchaguzi mwingine wa Septemba 16 utakaohusisha majimbo matatu na kata 21.

Mbali na Ukonga na Monduli, uchaguzi huo utahusisha Jimbo la Korogwe Vijijini ambalo liko wazi baada ya mbunge Stephen Ngonyani kufariki dunia Juni 2.

“Kuna wajibu wa chama na wa wapiga kura, hatuwezi kupuuza wajibu wa wapiga kura, sio tu kwa sababu ni vyama vya siasa, lakini nchi yetu haina utaratibu wa mgombea binafsi, basi hatuwezi kupuuza wajibu wa wapiga kura,” alisisitiza Nape.

“Yaani wakishapiga kura haturudi kuwauliza chochote, halafu tunaondoka, halafu tunarudi kwao tena baadaye.”

Nape ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema hilo ni suala la mjadala mpana kwa sababu chama ni sehemu ndogo ya jamii iliyopiga kura.

“Suala hili lina ukakasi na ukakasi wake ni sehemu ndogo, ipo wapi nafasi ya wapiga kura ambao hawana vyama, wapiga kura ambao walimpigia mtu bila kujali vyama vyao, nafasi yao ipo wapi. Hii ndiyo hoja.”

Pia, alizungumzia kwa uchache kuhusu sababu za wapinzani kuhama vyama akisema ni vigumu kujadili sababu za wanaohama, lakini ni kwa kuwa sababu ni zilezile.

“Umefika wakati wa kujadili nafasi ya wapiga kura ambao waliamua kutoka asubuhi na mapema kwenda kupiga kura bila kujadili vyama vyao, nafasi yake imeheshimiwa kwa kiasi gani, ipo wapi na inalindwaje,” alisema Nape.

Aibua mjadala

Akizungumzia kauli ya Nape, Katibu wa Wabunge wa CCM, Jason Rweikiza alisema ndani ya chama chao kuna changamoto na vilevile mambo mazuri.

Alisema kuwa wapinzani wanaoona huko walipo mambo hayaendi wanaweza kwenda popote wanapotaka.

“Lakini sheria yetu inasema ukihama chama chochote unapoteza cheo chako, tungekuwa na mgombea binafsi mambo yangekuwa tofauti,” alisema Rweikiza

Rweikiza ambaye pia ni mbunge wa Bukoba Vijijini, alisema mtu aliyehama chama kwenda kingine anapoteuliwa kugombea tena uongozi kwenye chama alichohamia huo unakuwa siyo uamuzi wa mtu mmoja, bali ni ya chama.

“Ninatofautiana na Nape kwamba mtu anapohama anakuwa amewasaliti wapiga kura, kwani chama kinapoamua kumrejesha agombee nafasi ileile ni kuheshimu wananchi na kutumia haki yao kumchagua tena kama kweli wanampenda.”

Alisema changamoto anayoiona katika hamahama hiyo ni gharama za uchaguzi ambazo hata hivyo alidai kuwa ni sehemu ya maisha kwa kuwa gharama katika maisha haziepukiki.

Alitoa mfano kuwa mtu akijenga nyumba nzuri kuna siku anaweza kukuta rangi imetoka au ina nyufa, lakini hawezi kuacha kuikarabati.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema maoni ya Nape ni sahihi.

“Lazima tuangalie tulipotoka, awali waliohama vyama walihama kutokana na sababu za msingi, lakini sasa ni kama mchezo wa kuigiza. Tukiacha haya yaendelee hatutaipeleka nchi pazuri,” alisema Mwalimu.

Alisema ni lazima kuwe na utaratibu wa kuwa na chombo cha kudhibiti hilo na wale wanaotoa sababu za kuunga mkono juhudi wasiruhusiwe kugombea tena.

“Hao wanatuingiza kwenye hasara na hatari kubwa. Labda kama tutaamua kwamba atakayejitoa, anapewa miaka mitano ndipo anagombea tena pengine wataheshimu utu na gharama zinazoteketea.”

Mwalimu ambaye aligombea ubunge Jimbo la Kinnondoni mwaka huu, alisema wapo wanasiasa wenye sababu za msingi za kutoka na hawawezi kuzuilika.

“Lakini wapo ambao wanafanya siasa na kudai kuwa wanaunga mkono juhudi za mtu mmoja pekee,” alisema.

Akizungumzia kauli ya Nape, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema ndiyo maana siku zote Katiba mpya inadaiwa na wananchi kwa kuwa kila kitu kitapata majibu kupitia Katiba hiyo.

Hata hivyo, Profesa Mpangala alisema kama kuna wanaoona Katiba si kipaumbele chao, hawana budi kuirekebisha sheria ya vyama vingi. “Lazima tuheshimu uamuzi wa wananchi ambao ndiyo wapiga kura, hatuwezi kuingia gharama kila kukicha kwa kisingizio cha kwamba mtu anafuata demokrasia,” alisema.

Alisema hali hiyo inaleta vurugu kisiasa na kusababisha nchi kutoheshimika.

“Lazima tuweke utaratibu kuwa mtu akichaguliwa kuwa mbunge ni lazima akimalize kipindi chake cha miaka mitano. Wabunge, madiwani wasiruhusiwe kuhama vyama mpaka uchaguzi mwingine. Lakini pia matakwa ya wapiga kura yaheshimike.”

Kuchauka amjibu Nape

Aliyekuwa Mbunge wa Liwale (CUF), Kuchauka aliyehamia CCM hivi karibuni alisema Nape ni mbunge na ana haki ya kupeleka hoja binafsi bungeni kuhusu suala hilo. “Kingine ni kwamba, Nape ana uwezo wa kupeleka maoni yake CCM ili yafanyiwe kazi, mimi sijaona shida ipo wapi,” alisema.

Alisema jambo la msingi ambalo mbunge huyo alitakiwa kueleza ni kuwa CCM inafanya kazi nzuri.

“Yale yaliyokuwa yanalalamikiwa na wapinzani, sasa yanafanyiwa kazi ukilalamika unasikilizwa,”alisema.

Kadhalika alizungumzia suala la gharama za uchaguzi na kusema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ina bajeti iliyotengwa kwa ajili ya chaguzi.

“Labda Tume ilalamike kuwa wapo nje ya bajeti, lakini ninajua wana fungu lao, siwezi kulalamika katika hilo.

Chanzo: mwananchi.co.tz