Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hamahama ya Wanasiasa inavyoyumbisha wananchi

95476 Pic+hamahama Hamahama ya Wanasiasa inavyoyumbisha wananchi

Fri, 14 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kauli za kubadilikabalika za baadhi ya wanasiasa wakati wanapohama kutoka chama hicho cha siasa kwenda kingine imewaweka lawamani na kuonekana ama vigeugeu au watu wenye kusukumwa na maslahi binafsi.

Kutokana na kauli hizo, wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema wanasiasa hao wamekuwa wanatenda kinyume na matamshi au ahadi zao.

Tabia hiyo imeongeza uzito katikamsemo kuwa “mwanasiasa akikwambia saa hizi ni usiku, lazima utoke nje ujiridhishe kwa kuangalia kama ni kweli.”

Hali hiyo imetokana na kuwa na kauli zinazobadilika au zisizo na msimamo thabiti, ambazo Dk Muhidini Shangwe anasema wanasiasa wa aina hiyo wanakuwa “wamejenga usugu wa kukosa soni (aibu) katika kauli wanazotoa bila kujali athari zake katika siasa na jamii.”

Mhadhiri huyo wa siasa nma utawala bora katika ikuu cha Dar es Salaam, anasema hoja anazotoa mwanasiasa wakati wa kuhama chama ndiyo zinaweza kuchafua au kukomaza siasa nchini.

“(Tabia hii) Inashusha hadhi ya mwanasiasa. Inapunguza heshima na taswira ya siasa za nchi, wananchi wanaanza kuona siasa ni eneo la mzaha,” anasema na kuongeza;

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Athari zake ni pamoja na dhana iliyosambaa kwa sasa, yaani mtu ukiongea sana au kusema uongo, mtu atakwambia ‘usiniletee siasa’, ” anasema Dk Shangwe.

Mhadhiri huyo anasema mtu anaweza kuhama chama bila kutukana na akalinda heshima yake.

“Sasa wewe unaondoka halafu unarudi hukohuko wakati ulishatukana na ukawaambia chama hicho ni wezi wa kura? Sasa mbona unarudi kwa wezi wa kura?” alihoji Dk Shangwe.

Dk Shangwe anasema kwa bahati mbaya asilimia kubwa ya Watanzania wamejenga imani kwa mwanasiasa mmoja mmoja badala ya kujali masuala. “Namna ya kuepuka athari kwa jamii ni pamoja na kujikita kwenye mijadala ya masuala, tusiamini sana mwanasiasa ila tuangalie anasema nini.

Kauli za wanasiasa

Kauli ya karibuni kabisa iliibua mjadala huo ni ya Waziri mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye aliyetangaza kujitoa Chadema Desemba mwaka jana akisema hatajiunga na chama chochote cha siasa, lakini juzi ikiwa imepita tu miezi miwili akatangaza kujerea CCM.

Sumaye alisema amechukua uamuzi huo ili apate sehemu ya kutoa mawazo na ushauri wake.

“Nimekuwa waziri mkuu kwa miaka 10 na kiongozi kwa miaka kadhaa nitakuwa sitendi haki endapo nitakaa mahali bila kutoa ushauri au mchango wangu kwenye Taifa,” alisema na kuongeza:

“Huwezi kutoa mchango kama hauna mahali na ukiutoa barabarani watu watakushambulia, nikaona mimi si wa hadhi ya kufika kudharauliwa. Nikasema ngoja nirudi kwenye chama changu kilichonilea, kunikuza hadi nilipofika na kujivunia kuwa nina mchango katika Taifa hili.”

Sumaye alitangaza kujiunga na Chadema Agosti 2015 akisema ilikuwa ni kazi kubwa kuzuia wimbi la mabadiliko, hivyo aliamini muungano wa Ukawa ungeshinda katika uchaguzi huo ambao mgombea urais wa upinzani alikuwa Edward Lowassa.

Alisema hakujiunga Ukawa kwa kuwa mgombea urais alikuwa akitoka Kanda ya Kaskazini, wala kuwa kuwa viongozi wengi waandamizi wanatoka huko, bali ni kutaka kutoa uzoefu wake kushirikiana na Lowassa katika uongozi wa nchi.

Wakati huo Sumaye alisema dhana kwamba hakuna maisha ya kisiasa nje ya CCM imepitwa na wakati.

Baada ya kukaa Chadema kwa miaka minne, Desemba mwaka jana Sumaye alitangaza kujiondoa akidai chama hicho hakina demokrasia.

Sumaye alifikia uamuzi huo siku chache baada ya kushindwa kutetea kiti chake cha uenyekiti wa Kanda ya Pwani ambako hakuwa na mpinzani, kwa kupata kura nyingi za hapana.

Pia alidai kufedheheshwa na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho baada ya kuchukua fomu kuwania uenyekiti wa chama hicho Taifa.

“Najua katika kujikosha watasema nimepewa pesa, lakini kama nilijiunga Chadema kwa pesa, basi na kuondoka pia nimepewa pesa. Lakini kama nilijiunga kwa utashi wangu basi najiondoa kwa utashi wangu,” alisema.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Sumaye kufanya hivyo, baada ya kustaafu uwaziri mkuu (1995-2005) alitangaza kuachana na siasa na miaka michache baadaye alikwenda Marekani kusoma.

Aliporudi, baadaye mwaka 2015 alikuwa ni miongoni mwa wana CCM 42 waliojitokeza kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kuwa mgombea urais, na alipoenguliwa alikimbilia upinzani akidai kwenda kumuunga mkono Lowassa.

Hata hivyo, si Sumaye pekee aliyetangaza kurejea CCM au kuwahi kutoa kauli za kubadilika. Baadhi yao ni waliojiunga upinzani mwaka 2015 akiwamo Lowassa na sasa wamerudi CCM.

Lowassa ambaye aliweka upinzani mkali katika uchaguzi mkuu 2015 akichuana kwa karibu na Rais John Magufuli, alishindwa katika uchaguzi huo ambao vyama vya upinzani vilivuna wabunge na madiwani wengi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Lowassa alipata kura zaidi ya milioni sita, huku Rais Magufuli akishinda kwa kura zaidi ya milioni nane.

Kama ilivyokuwa kwa Sumaye, Lowassa wakati akirejea CCM alisema amerudi nyumbani na kutaka watu wasimuulize amekwenda kufanya nini, huku akiwaomba Watanzania milioni sita waliompigia kura kuzielekeza kwa Rais Magufuli.

Wakati akijiondoa CCM, Lowassa alisema hakutendewa haki katika kupitisha majina ya wagombea urais, hiyo hawezi kuendelea kubaki kwenye chama hicho.

“CCM si baba yangu wala Mama yangu, Watanzania kama wameyakosa mabadiliko ndani ya CCM, basi watayapata nje ya CCM,” alikaririwa Lowassa.

Katika kusisitiza kauli yake hiyo Desemba 2018 alipohojiwa na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Lowassa alisema hana mpango, hajafikiria wala kupanga kuondoka Chadema.

Lowassa alitoa kauli hiyo baada ya naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu kumtaka ajitokeze kuweka msimamo wake hadharani baada ya kusifiwa mara kwa mara na viongozi wa juu wa CCM na Serikali.

Wabunge waliohama

Ukiacha mawaziri hao wakuu wastaafu, viongozi wengine waliorudi CCM ni Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), Chacha Marwa Ryoba (Serengeti), Godwin Mollel (Siha), James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati) na Joseph Mkundi (Ukerewe) waliokuwa wabunge wa Chadema na kwa upande wa CUF ni Maulid Mtulia (Kinondoni) na Zuberi Kachauka (Liwale).

Aliyekuwa mbunge wa Babati mjini kwa tiketi ya Chadema, Pauline Gekul alisema amejiondoa katika chama hicho kwa madai ya kuchoshwa kunyanyaswa, kutengwa na kuachiwa mzigo wa kusimamia majukumu ya jimbo bila msaada kutoka makao makuu.

Ingawa alikiri kutoifahamu vizuri CCM licha ya kuhamia, alisema amefanya hivyo, ili kutimiza wajibu wa wananchi wake kwani anashindwa kuzitimiza akiwa upande wa upinzani.

“Natangaza kuomba kujiunga CCM, chama ambacho licha ya kuwakosoa sana, nimeona wana dhamira njema ya kujifanyia mageuzi makubwa ya chama kitaasisi,” ilieleza sehemu ya barua yake kwenda kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Aliyekuwa mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chadema, Mwita Waitara ambaye sasa ni mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, alisema amehama Chadema kwa sababu ya kutofautiana na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe baada ya kumhoji kwa nini chama hicho hakifanyi uchaguzi wa mwenyekiti.

Hata hivyo, Chadema klisema kuwa Waitara alikuwa mzigo kwa chama hicho na kwamba sababu alizotoa ni za uongo na kwamba chama kilikuwa katika mkakati wa kumfukuza.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa kichama Ilala, Makongoro Mahanga alisema Waitara alishapewa barua za kufukuzwa na alikuwa ameshanyang’anywa nafasi zote za kichama.

Julai mwaka 2018, aliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga alisema amejitoa Chadema kwa sababu ya kwenda kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Alisema siasa za uhasama, malumbano na chuki zimemuondoa Chadema na kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano kwa maslahi ya taifa kwa sababu huwezi kufanya hivyo ukiwa upande wa pili bila kuonekana msaliti. Kalanga aliwahi kuwa diwani kupitia CCM, kabla ya kuhamia Chadema mwaka 2015.

Naye aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja aliyehamia Chadema 2015, Machi mwaka jana alitangaza kurudi.

Mgeja alirudi CCM siku chache baada ya Lowassa kujiondoa katika chama hicho na kueleza kuona sababu zilizomfanya ahamie Chadema wakati wa uchaguzi mwaka 2015 hazipo.

“Nimeamua kurudi nyumbani, sijafuata mkumbo wala kushawishiwa na mtu bali, utendaji kazi wa Serikali yangu ya awamu ya tano umenifanya nirudi,” alisema Mgeja ambaye anatajwa kuwa rafiki wa karibu wa Lowassa.

Kwa upande wake, aliyekuwa mbunge wa Siha kwa tiketi ya Chadema, Dk Godwin Mollel alisema hakuwa amewaza kurudi CCM, lakini uamuzi huo aliufanya baada ya kutafakari kwa saa tatu na kilichomsukuma zaidi ni kutokana na kuchoshwa na namna Chadema inavyoendesha shughuli zake.

“Niliamini Chadema ni watetezi wa wananchi, lakini bahati mbaya nikagundua ni kundi tu la watu ambalo nalo linatafuta mbinu ya kwenda Ikulu na suala muhimu kwao si wananchi,” alisema Mollel.

Naye aliyekuwa mgombea ubunge Kahama mjini kwa tiketi ya Chadema, James Lembeli alitangaza kurudi CCM akisema kwa Tanzania anayoijua hakuwa amepoteza mkia, kwani huko aliko ndiko mafisadi wamekimbilia.

Hata hivyo, Julai mwaka 2016 Lembeli aliwahi kukaririwa na gazeti hili akisema hana mpango wa kurudi CCM.

Alisema licha ya chama hicho kupata mwenyekiti mpya kimejaa wanafiki, hivyo si kazi rahisi kurejea, jambo ambalo alishalikiuka na kurejea ndani ya chama hicho

Maoni ya wachambuzi

Suala la kuhama chama linatazamwa na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohamed Bakari kuwa linatokana na wengi hupigania kulinda maslahi yao binafsi ya kisiasa.

Anasema kila mwanasiasa ana maslahi yake, hivyo huangalia ni wapi na kwa wakati gani maslahi yake yatatimia.

Sababu ya pili ni upepo wa kisiasa unaochagizwa na hesabu za kubahatisha kwa wakati husika, akisema wanasiasa wengi hufanya hesabu hizo, akitolea mfano wa wimbi la wanasiasa waliohama vyama 2015.

“Mwanasiasa aliyehama mwaka 2015 hakushawishika na itikadi za vyama, huyo hakuwa na msingi wa itikadi. Kwa mfano wanaCCM wengi walihamia upinzani wakiamini upinzani utachukua nchi kurejea CCM, baada ya kushindwa.”

Chanzo: mwananchi.co.tz