Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo kupitisha sera usawa wa jinsia

ACT.jpeg Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo kupitisha sera usawa wa jinsia

Mon, 12 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha ACT Wazalendo kesho kitafanya mkutano wa halmashauri kuu ambapo pamoja na mambo mengine itapokea na kupitia mapendekezo ya sera ya chama ya jinsia inayolenga kuweka misingi ya usawa wa kijinsia katika nafasi na ngazi zote za uongozi ndani ya ACT Wazalendo.

Agosti 2023, chama hicho kilifanya mabadiliko ya kamati ya wasemaji wa kisekta (mawaziri kivuli) ambapo katika mabadiliko hayo uwiano wa kijinsia uliiimarika.

Waliteuliwa jumla ya wasemaji wanawake (mawaziri kivuli) 14 kati ya wasemaji wote 25, sawa asilimia 54 ya wasemaji wote.

Akifafanua kuhusu kupitishwa kwa sera hiyo kesho Februari 12, 2024, Waziri Mkuu Kivuli wa chama hicho, Dorothy Semu amesema kinachokwenda kufanyika ni kuweka misingi ya kisera ndani ya chama hicho.

“Ni kweli chama chetu kina maono chanya ya usawa wa kijinsia, lakini hakikuwa na miongozo na misimamo ya kichama ambayo inatuongoza, hivyo inaweza kuwa tofauti endapo akitokea kiongozi mwingine asiye na maono ya kijinsia,” amefafanua alipotafutwa na Mwananchi Digital.

Amesema walikuwa wanafanya kwa utashi kwa kuwa haikuwa imeandikwa sehemu yeyote, hivyo wanaweka mikakati ya kisera ndani ya chama ili wafikie usawa huo kwa kuwa kuna kitu kinachowaongoza.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Februari 11, 2024 na Naibu Katibu wa Habari Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Janeth Rithe, miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa na kutolewa uamuzi katika kikao hicho ni pamoja na maandalizi ya mkutano mkuu wa chama taifa uliopangwa kufanyika Machi 5 na 6, 2024.

“Ajenda nyingine ni kupokea taarifa ya ujenzi wa chama. Halmashauri kuu pia itapitia na kutoka na mapendekezo ya maboresho ya katiba ya chama kwa kuzingatia maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wanachama na wadau mbalimbali wa demokrasia,” imesema.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa halmashauri kuu inafanyika kwa mujibu wa ibara ya 74(1) ya katiba ya ACT Wazalendo ya mwaka 2015 toleo la mwaka 2020 ambapo kikao kitafanyika katika ukumbi wa halmashauri kuu uliopo katika ofisi za makao makuu Magomeni.

“Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo ni kikao cha pili cha uamuzi kwa ukubwa baada ya mkutano mkuu wa chama. Wajumbe wanaounda kikao hiki ni wenyeviti na makatibu wa mikoa yote 39 ya kichama kutoka bara na Zanzibar pamoja na wajumbe wa kamati kuu ya chama,” inaeleza taarifa hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live