Dar es Salaam. Viongozi wanne wa Chadema wamekamatwa wakati wakifuatilia utaratibu wa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutoka katika gereza la Segerea baada ya kulipa faini ya Sh70 milioni.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Machi 13, 2020 mkuu wa kitengo cha mawasiliano Chadema, Tumaini Makene amewataja waliokamatwa kuwa ni mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Bunda. Ester Bulaya; Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na katibu wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo.
Mwingine aliyekamatwa ni mjumbe wa baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Hadija Mwago.
Mdee na Bulaya walitoka jela jana baada ya kulipa faini, leo walikwenda kumpokea Mbowe ambaye amekamilisha taratibu za kutoka jela.
Viongozi hao wamekamatwa saa 7:30 mchana baada ya kufika katika gereza hilo na kuanza kuzuiwa na askari wa Jeshi la Magereza waliotumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.
Wakati mabomu hayo yakipigwa, viongozi hao wa Chadema waliwekwa chini ya ulinzi kwa madai ya kukiuka amri halali ya kuwataka kuondoka katika eneo hilo.
Habari zinazohusiana na hii
- Wanachama wa Chadema watawanywa kwa mabomu ya machozi gereza la Segerea
- VIDEO: Mnyika, Heche na Mwalimu watoka jela
- VIDEO: Mchungaji Msigwa azungumzia uhusiano wake na Rais Magufuli
- VIDEO: Msigwa afunguka kuhusu kilichotokea gerezani, asema aliwaachia vumbi
Hali ya ulinzi bado imeimarisha katika gereza la Segerea ambapo askari wenye silaha wamejipanga kuanzia kwenye lango la gereza mpaka barabarani na kutoruhusu mtu yoyote kupita katika eneo hilo.