BAADA ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumaliza mchakato wa kutoa na kurejesha fomu kwa wagombea ubunge, udiwani na uwakilishi, sasa kinaingia kwenye mchakato wa kura za maoni, kikisisitiza kwamba kitazingatia haki na nidhamu kupata wagombea wake.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Humphrey Polepole alisema jana kwamba bila kujali wingi wa waliojitokeza kuwania nafasi hizo, kitatoa nafasi kwa kila mtu kujieleza, kujadiliwa na kupigiwa kura kwa haki.
Aidha, makatibu wa CCM wa wilaya na mikoa waliozungumza na Habari- Leo, wamesisitiza kuwa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha mchakato huo wa kura, unafanyika kwa haki hatimaye wanapatikana watu sahihi wa kupeperusha bendera ya chama kwenye ubunge, uwakilishi na udiwani.
“Sasa tunaingia kwenye kura za maoni, haijalishi wagombea ni wengi kiasi gani, tumejipanga. Kila mtu atajieleza, kujadiliwa na kupigiwa kura kwa haki. Tunataka utaratibu huu kuwa ni mfano Afrika,” alisema Polepole jana kwenye mkutano wa utekelezaji wa Ilani ya chama mkoani Ruvuma.
Polepole ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, aliwataka wagombea wote waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali, kuwakilisha chama kwenye uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, kuendeleza nidhamu hata baada ya uteuzi wao kwa kuwa umoja ni ushindi.
Alisema chama kimebadili mfumo wa kuteua wagombea wake wa nafasi hizo za udiwani, ubunge na uwakilishi, kwa lengo la kuweka nidhamu, uwazi na haki, jambo ambalo kimejipanga kulitekeleza.
“Ndiyo maana tulisema watia nia lazima wawe wanyenyekevu na watulivu. Naomba hata baada ya mchakato huu kukamilika na Kamati Kuu kuteua jina moja la mgombea, nidhamu ya watia nia iendelee kuwepo kwa sababu umoja ndio ushindi,” alisisitiza.
Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga aliliambia gazeti hili kwamba wamejipanga kufanya uchaguzi kesho . “Leo (jana) tupo kwenye maandalizi ya uchaguzi huo, tupo kwenye mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi,” alieleza.
Alisema CCM mkoa huo wa Dodoma, itaanza vikao vyake mapema kutokana na wingi wa wagombea waliochukua fomu. Pia alisema watatoa muda kwa kila mgombea kujieleza, kupigiwa kura na matokeo ya kura zake.
Katibu wa CCM Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Andrea Gwaje alisema pia watapiga kura kesho kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa za mfumo mpya. Alisema kwa jimbo la Mbagala, uchaguzi ni keshokutwa.
“Kuhusu wingi wa wagombea maana wilaya yetu kwa ubunge pekee tuna wagombea 177, haina ugumu wowote tumejipanga kila mmoja atafikiwa kwa kuzingatia haki,” alisema.