Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gwajima aponda wasiotambua mafanikio ya JPM

85655b8afef6387bbf84b3273f404724 Gwajima aponda wasiotambua mafanikio ya JPM

Thu, 11 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima (CCM) ameliamsha bungeni baada ya kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli na kuwashangaa wanaoyapinga kuwa wana ugonjwa maalumu unaohitaji tiba maalumu.

Pia, wabunge wengine wamewahamasisha watendaji wa serikali, kuhakikisha wanaitekeleza vyema mipango ya kimkakati iliyowasilishwa na serikali ili iweze kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Wabunge hao waliyasema hayo bungeni jana wakati wakichangia hoja kuhusu mipango miwili ya maendeleo, iliyowasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Mipango hiyo ni Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo wa mwaka mmoja 2021/22 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/2022 hadi 2025/26. Akichangia hoja hiyo, Askofu Gwajima alisema katika mjadala huo kumekuwa na hoja zinazozungumzwa bungeni hapo, kuonesha kwamba awamu ya Rais Magufuli haijafanya jambo lolote.

“Mheshimiwa Spika mimi nasema mtu ambaye halioni hilo ana ugonjwa hatari usiotibika nchini,” alisema.

Alisema kuanzia mwaka 1976 hadi 1981 kulikuwa na ndege 11, na hadi nchi inaingia kwenye hatua ya ubinafishaji kulikuwa na ndege tisa. Alisema Rais Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015 kulikuwa hakuna ndege, lakini ndani ya kipindi cha miaka mitano Tanzania ina jumla ya 12.

“Lakini mheshimiwa Naibu Spika unakumbuka vizuri Tanesco kabla ya Rais Magufuli hajaingia madarakani ilikuwa inaendeshwa kwa kupewa ruzuku ya shilingi bilioni 438 kila mwaka, lakini tangu mwaka 2015 inajiendesha kwa fedha yake yenyewe na inafanya vizuri, asiyeona ana ugonjwa maalum unaohitaji daktari maalumu,” alisema.

Alisema pia mwaka 2015, Tanzania ilikuwa na vijiji 2,018 vilivyokuwa na umeme lakini ndani ya miaka mitano vijiji 10,263 vimepata umeme. “Na kwa taarifa ya asiyeona ni kwamba vimebaki vijiji 2,005 tu kwa Tanzania yote iwe na umeme.

Mwenye macho ni muhimu atazame wapi tunatoka na wapi tunapoelekea kwa sasa,” alisema. Alisema anajua vizuri kuwa kuna watu wanasema Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, usiongelewe sana.

“Sikiliza niwaambie tangu Tanzania ianze enzi za marais waliopita ilikuwa na megawati za umeme 1,602 lakini sasa mradi huu wa Mwalimu Nyerere pekee yake utazalisha umeme wa megawati 2,115, sasa utaachaje kuongea kuhusu huu mradi? alihoji.

Alisema akiwa nchini Japan alishuhudia nchi hiyo ikiwa na reli ya umeme yenye kasi ya 250 kwa saa pamoja na treni nyingine itakayozinduliwa hivi karibuni inayopita ardhini, itakayokuwa na kasi ya kilometa 500 kwa saa.

“Sisi hapa Tanzania kwa upande wa Afrika Mashariki tumekuwa nchi ya kwanza kutekeleza mradi wa treni yenye uwezo wa kwenda kilometa 160 kwa saa.

Utasemaje Rais Magufuli hajafanya vitu? Anayesema hivyo anahitaji dawa maalumu na daktari maalumu,” alisisitiza Gwajima.

Alisema wakati Rais Magufuli anaingia madarakani, tembo nchini walikuwa wamebaki 15,000 lakini ndani ya uongozi wake wa miaka mitano leo kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Maliasili na Utalii wapo tembo 60,000.

Kwa upande wa afya, mbunge huyo alisema wakati wa Uhuru nchi ilikuwa na hospitali za wilaya 77 lakini ndani ya miaka mitano ya Dk Magufuli, sasa zimejengwa hospitali 102 na kushangaa wanaobeza hatua hiyo.

“Tulikuwa na hospitali za rufaa za mikoa 18 tangu Uhuru, lakini ndani ya miaka mitano zimejengwa 10,” alisema.

Alisema kwenye vituo vya afya, tangu Uhuru vilikuwepo 535 lakini ndani ya miaka mitano vimejengwa vituo 487, zahanati zilikuwepo 4,554 tangu Uhuru lakini 1,998 zimejengwa ndani ya miaka mitano.

Mbunge wa Kuteuliwa, Humphrey Polepole (CCM), alisema kazi kubwa imefanyika katika mpango wa pili katika kuimarisha uchumi mkubwa. Alieleza kuwa eneo hilo likifanyiwa kazi vizuri, litakwenda kwenye uchumi mdogo unaohusisha watu.

Alielezea viashiria vichache, kuonyesha kwamba kazi imefanyika kwenye uchumi mkubwa katika mpango wa pili ; na kuna kila sababu ya kuendeleza mafanikio hayo katika Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano 2021/22 hadi 2025/26.

Alisema kiashirikia cha kwanza ni ukuaji wa uchumi kupitia ujenzi, ambapo Serikali ya Awamu ya Tano imejenga bandari kubwa na ndogo, imejenga viwanja vya ndege na barabara. Pia inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Kiashiria kingine ni mfumuko wa bei kutoka asilimia tano hadi tatu ; na nafuu ya kodi kwa watumishi kwenye kodi katika mishahara (PAYE) kutoka 12 hadi asilimia tisa.

Polepole alisema katika eneo la umeme, kazi kubwa imefanyika kufikia vijiji vingi na vimebakia vijiji 2,000.

“Umeme ambao tumezalisha mpaka sasa tuna ziada, tulianza na megawati 1,300 na sasa tuna 1,600 na hiyo ni ziada ya matumizi ambayo tunayo,” alisema.

Alisema pia uchumi huo mkubwa, unakwenda sambamba na uwekezaji katika sekta binafsi, ambapo serikali katika eneo hilo imeweka mazingira wezeshi kwenye kodi ya kampuni iliyopunguzwa kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa viwanda vinavyohusika katika kutengeneza dawa.

Hatua hiyo inawezesha viwanda nchini kutengeneza dawa na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa. Alisema lazima viwanda vya ndani, vilindwe na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ndani, haziagizwi kutoka nje.

Aliipongeza serikali kwa uamuzi wa kuongeza kodi katika uingizaji wa sukari kutoka asilimia 25 mpaka 35 ili viwanda vya ndani vizalishe na kuuza sukari nchini.

Aliwashauri watendaji wa serikali, kufanya kila linalowezekana, kuhakikisha miradi ya uzalishaji wa nishati, inakamilika kabla Rais John Magufuli hajaondoka madarakani.

“Upo mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere megawati 2,115 unaendelea, lakini kwenye hotuba yake Rais ameeleza kuwa kuna miradi mingine karibu 10 ambayo itazalisha umeme na kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.

Watendaji wahakikishe miradi yote hiyo inakamilika” alisema.

Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota aliishauri serikali katika eneo la uzalishaji wa korosho, iwekeze zaidi kwenye ubanguaji; na kuondoa kodi katika mashine za ubanguaji, jambo litakalowezesha wakulima kuacha kuuza korosho ikiwa ghafi.

Alishauri vivutio maalumu viwekwe kwa wawekezaji wapya, ikiwemo kuondoa kodi na tozo katika vifungashio .

Alisema hatua hiyo itapunguza gharama, hivyo watapatikana wawekezaji wengi na wawekezaji wa ndani.

Kuhusu mradi wa Mchuchuma na Liganga, alisema umefika wakati wa fedha ziwekwe za kutosha katika miradi hiyo na kujenga reli kutoka Mtwara hadi Mbababay.

Mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini alisema katika utekelezaji wa mipango hiyo ya maendeleo, ufanyike uchambuzi wa watekelezaji ili ifahamike nani anafanya nini, rasilimali gani zitatumika na mipango ya wizara, taasisi na halmashauri ianishwe.

Mbunge wa Mpendae, Taufiq Turky alishauri uchumi wa Zanzibar ili uwe mkubwa, uanzishwe mpango wa upakiaji na upakuaji wa mizigo, jambo ambalo linafanyika katika takribani visiwa vyote duniani vilivyoendelea.

Chanzo: habarileo.co.tz