MGOMBEA ubunge jimbo la Arusha mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM), Mrisho Gambo anatarajia kuanza kampeni za mlango kwa mlango hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni za kata ya Sekei, mgombea huyo alisema amebakiza kata tatu amalize kata zote za jimbo hilo kufanya mikutano ya hadhara na atabadili namna ya ufanyaji wa kampeni.
"Tumefanya mikutano zaidi ya kata 20 na hizi tatu zilizobaki tukimaliza tunaanza kampeni za nyumba kwa nyumba, mlango kwa mlango na ikibidi kitanda kwa kitanda,"alisema Gambo.
Awali aliwaomba wakazi wa kata hiyo kukipigia kura CCM kwa mtindo wa mafiga matatu yaani diwani, mbunge na rais ili iwe rahisi kupenyeza hoja za vipaumbele vya jimbo lake.
Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Sekei, Gerald Sebastian ambaye alishaanza kampeni za nyumba kwa nyumba alisema alianza kuwatumikia wananchi wake kabla hata hajapitishwa na chama chake, hivyo ni mtu sahihi kwao.
"Inashangaza kata ambayo ina karibu taasisi zote za serikali kukosa shule ya kata, jambo ambalo naahidi kulisimamia ili watoto wetu wasiende kusoma kata za jirani,"alieleza.
Wagombea hao walivishwa mashuka ya kimasai lakini pia walipewa fimbo kama ishara ya usimamizi na uongozi kwa kabila hilo ambalo ndio wenyeji wa mkoa wa Arusha.