Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gambo ataja turufu za Rais Samia uchaguzi wa 2025

Mrisho Gambooooooo Gambo ataja turufu za Rais Samia uchaguzi wa 2025

Fri, 5 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo amesema kurejea kwa shughuli za kisiasa, kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji na utekelezaji bora wa miradi ya maendeleo ni turufu za Rais Samia Suluhu Hassan kuelekea uchaguzi ujao.

Turufu nyingine ni uboreshaji wa huduma za kijamii kama miundombinu, huduma za afya na elimu; kukuza kilimo pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma.

Gambo amebainisha hayo jana Alhamisi Januari 4, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano maalumu alipotembelea makao makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini ambayo inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, MwanaSpoti na mitandao ya kijamii.

Amesema utawala wa Rais Samia uliondoa marufuku ya shughuli za kisiasa Januari 3, 2023, akisema uamuzi huo ulijibu kilio cha muda mrefu cha vyama vya siasa vya upinzani.

"Lakini sioni wanasiasa wa upinzani wakitumia fursa hiyo. Katika Jimbo la Arusha kwa mfano, mimi pekee ndiye ninafanya mikutano ya kisiasa, jambo ambalo limepunguza ladha ya kufanya mikutano,” amesema na kuwakumbusha wapinzani wajibu wao mkuu wa kuikosoa Serikali.

Amesema Serikali ya awamu ya sita imetatua changamoto zilizoathiri uwekezaji kwa kuchelewa kutoa vibali vya kazi.

“Wawekezaji wanaoleta mitaji yao wamekuwa wakileta baadhi ya wataalamu ambao watalinda uwekezaji wao, lakini utoaji wa vibali vya kazi bado ni changamoto,” amesema.

“Hata hivyo, Serikali imefanyia kazi changamoto hiyo. Fursa za uwekezaji na miradi imeongezeka kwa kiasi kikubwa, hivyo kutengeneza ajira na ulipaji wa kodi ili kukuza maendeleo ya nchi,” amesema.

Amesema akiwa amewahi kuwa Makamu wa Rais wa nchi katika utawala wa awamu ya tano, Rais Samia alisimamia ipasavyo ukamilishaji wa miradi ya maendeleo iliyoanzishwa.

Miradi hii ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).

Mkuu wa mkoa huyo wa zamani wa Arusha amesema mengi yamefanywa na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya miundombinu, utoaji wa huduma za afya, huduma za maji na kuleta mageuzi katika sekta ya elimu.

Amesema Serikali imeongeza posho ya chakula kwa wanafunzi wa vyuo vikuu hadi Sh10,000 kwa siku kutoka Sh8,000 ya awali, imepandisha mgawo wa bajeti kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na kufuta riba zinazotozwa kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

“Serikali imeongeza bajeti ya kilimo na kuwapa wakulima pembejeo za ruzuku,” amesema, akiongeza kuwa hatua za Serikali zimegusa sekta tofauti.

"Watumishi wa umma walikuwa wakihangaika na malimbikizo yasiyolipwa na walifanya kazi kwa miaka mingi bila mishahara yao kuongezwa, lakini Rais Samia amefanyia kazi changamoto hizi zote,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live