Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fursa za wanawake katika siasa bado kiduchu nchini

46977 Pic+wanawake

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni mwaka mmoja tu umesalia kufika 2020 ambapo kipenga cha kampeni kitapulizwa tena kugombania uongozi nchini kupitia vyama vya siasa.

Unapozungumza siasa, na hasa wakati wa uchaguzi nchini hutaacha kuizungumzia upande wa Zanzibar ambako huwa na mvuto na msisimko wa aina yake kulinganisha na maeneo mengine.

Na kwa Zanzibar, pamoja na msisimko huo, siasa zimebebwa na upande mmoja wa jinsia. Huwaoni wanawake wengi wakishiriki kama ilivyo kwa wanaume.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Zanzibar ina wakazi wasiopungua 1,300,000. Kati ya hao wanawake wana akisi asilimia 51 ya watu wote.

Lakini, umewahi kujiuliza ni kwa nini wanawake hawa ambao ni wengi kuliko wanaume hushindwa kupata nafasi za uongozi katika vyama vyao na majimboni?

Kwa suala hili wapo wanaoamini kwamba ni kutokana na mfumo dume unaoendelea kutawala kwenye vichwa vya wengi na wengine wakidhani ni wanawake wenye kukosa ujasiri wa kuwania nafasi hizo.

Kwa kuona matatizo hayo, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa-Zanzibar) kwa kushirikiana na Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoratibu shughuli za wanawake (UN-Women), wamezindua kitabu cha mwongozi wa kuwapa fursa wanawake katika uongozi kupitia uchaguzi wa mwaka 2020.

Mkurugenzi wa Tamwa-Zanzibar, Dk Mzuri Issa anasema bado kuna changamoto kubwa ya uongozi kwa wanawake visiwani, kwa kuwa kinachohubiriwa ni tofauti na kinachotendeka.

Alisema jamii inaendelea kuhubiri usawa katika demokrasia lakini wanawake wanaendelea kunyimwa fursa za uongozi kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema hali hiyo inatokana mfumo mbovu na imani waliyonayo baadhi ya watu kwenye jamii kwamba mwanamke hawezi kuwa mwenye nafasi kubwa zaidi katika jamii.

“Kwa mfano katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa mwaka 2015, baadhi ya wanawake waliachika kwenye ndoa zao kwa sababu ya kuweka dhamira ya kutaka kugombea nafasi fulani,” aliongeza.

Alisema mazingira ya aina hiyo kwenye ndoa ni kuwanyima fursa wanawake na kuwafanya waendelee kuishi kwenye mfumo dume ambao ni kandamizi kwao.

Kutokana na hali hiyo, nafasi ya wanawake katika uongozi bado ni finyu licha ya kuwapo dhamira ya kufikia asilimia 50 kwa 50.

Mathalan, mwaka 2015 wanawake waliopata nafasi za uongozi hasa ubunge kupitia mifumo mbalimbali (jimboni, viti maalumu na uteuzi wa rais) ilikuwa ni asilimia 32.

Kwa Zanzibar wanawake walioingia katika Baraza la Wawakilishi ni asilimia 36 ambao ni jumla ya wawakilishi 28 kati ya 84.

Kwa upande wa udiwanini, wanawake waliopenya ni 85 kati ya 173, ikiwa ni sawa na asilimia 49.

Takwimu hizo zinabainisha wazi kuwa wanawake hawajapata fursa sawa ya uongozi na uwakilishi katika vyombo vya utoaji maamuzi vya Bunge, Baraza la Wawakilishi na halmashauri.

Lililo wazi ni kuwa idadi ya wanawake inazidi kuongezeka, lakini imeongezwa na uwepo wa viti maalumu ambao ni mkakati wa dharura tu, lengo ifikie wakati wengi waingie katika ngazi za maamuzi kupitia sanduku la kura majimboni au kwenye kata.

Mathalan, tumeona ni wanawake sita tu walioshinda viti vya uwakilishi kupitia majimbo kati ya 54, sawa na asilimia 11.

Hata kwa ubunge, wanawake walioshinda viti majimboni kutoka Zanzibar ni watatu tu katika majimbo 50 yaliyopo, hiyo ni sawa na asilimia 6 tu.

Ni kutokana na takwimu hizo, wanaharakati wanaikumbatia hoja ya 50/50 ili kuongeza na uwiano kati ya wanawake na wanaume katika nyanja zote za uongozi kwa mujibu wa Katiba.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 21 kila raia wa Jamhuri ya Muungano ana haki sawa za kushiriki katika uongozi wa nchi aidha moja kwa moja au kwa njia ya uwakilishi.

Pia, sehemu ya 21 ya Katiba ya Zanzibar inasema kila mtu apewe nafasi sawa katika kupata nafasi za uongozi kwenye serikali, aidha kwa njia ya moja kwa moja ama kupitia wawakilishi wao waliochaguliwa kwa njia huru na haki.

Hivyo, wanawake ni kiungo muhimu katika maendeleo ya Taifa na Tanzania haiwezi kupigana na umaskini, wala kuimarisha demokrasia bila ushiriki wa wanawake katika nyanja zote za maamuzi.

Hoja hizo zinamgusa Fatma Omar, mwanamke aliyewania ubunge (CUF) katika jimbo la Chakechake Kusini Pemba ambaye anadai alikutwa na kadhia ambayo hataisahau.

Fatma anasema katika uchaguzi huo matokeo ya awali yalionyesha amepata kura 84, sawa na mpinzani wake na hakukua na kura iliyoharibika na mchakato uliporudiwa ilionekana kura moja imeharibika na hivyo akaambulia 83 dhidi ya 84 za mwenzake.

Alisema alishangazwa na matokeo hayo, lakini aliamua kukubaliana nayo kwa vile ni maamuzi ya chama.

Hata hivyo, Fatma hakukata tamaa aliendelea kuamini angeweza kupitishwa na Baraza Kuu la CUF ambalo ndilo lenye mamlaka ya mwisho ya uteuzi na yeye alikuwa mwanamke pekee aliyejitokeza kwenye kinyang’anyiro hicho kwa majimbo yote 18 ya Pemba, lakini hakupenya.

Fatma anasema bado hajakata tamaa na ataendelea kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020 akiwa na matumaini makubwa na kwamba huenda walio wengi sasa wamejifunza na kutambua nafasi ya mwanamke.

Licha ya changamoto hiyo, baadhi ya wanawake wanaamini mwanamke anaweza na hatimaye kuwa mfano kwa wengine.

Miongoni mwao ni Amina Salum Ali, Waziri wa Bishara, Viwanda wa Zanzibar ambaye mwaka 2015 aliingia katika kinyang’anyiro cha urais hadi kufika kwenye nafasi ya tatu kupitia CCM.

Amina anasema ujasiri na maamuzi ndiyo yaliyomsukuma kuamua kugombea nafasi hiyo na hatimaye kuingia katika tatu bora, jambo ambalo anasema hata kwake halikuwa rahisi lakini aliweza kwa sababu ya uthubutu.

Hata hivyo, Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Nao anasema chama hicho kinawapa wanawake wengi fursa za uongozi na ndio maana hata yeye ameweza kushika nafasi ya juu.

Hata Mkurugenzi wa habari uenezi wa CUF, Salim Abdalla Bimani anasema kila mmoja anafahamu na kujua nafasi ya mwanamke na hata chama chake kinatekeleza hilo na kina mpango madhubuti wa kuwapa wanawake nafasi zaidi ikiwemo za majimbo katika uchaguzi mkuu wa 2020.



Chanzo: mwananchi.co.tz