Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fukuto jipya TLP

Tlp Pic Fukuto jipya TLP

Thu, 4 May 2023 Chanzo: mwanachidigital

Harufu ya mgogoro mpya inanukia katika chama cha TLP baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Wanawake wa chama hicho taifa, Mwaka Mgimwa kuondolewa kwenye wadhifa huo na nafasi yake kurithiwa na Rukia Kimwaga.

Kwa mujibu wa Mwaka, uamuzi wa kuondolewa kwake umefanyika kinyume na kanuni ya jumuiya hiyo inayoupa mkutano mkuu mamlaka ya kufanya uchaguzi wa kiongozi wa nafasi hiyo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Richard Lyimo amesema uamuzi huo ni matokeo ya kikao cha sekretarieti ya TLP iliyoketi wiki iliyopita.

Akizungumza kuhusu kuondolewa kwake, Mwaka amesema hakupokea taarifa yoyote kuhusu mabadiliko ya nafasi yake.

“Nimesikia tu kwamba ameteuliwa mwenyekiti mpya wa wanawake taifa, uamuzi huu umefanyika kinyume na kanuni ya jumuiya yetu, kwa sababu nafasi hiyo si ya kuteuliwa,” amesema.

Kulingana na Mwaka, ili kujaza nafasi hiyo ulipaswa uitishwe uchaguzi na wajumbe wa mkutano mkuu wa wanawake ndiyo wenye mamlaka ya kumchagua mwenyekiti.

“Mimi nimechaguliwa mwaka 2020 na kanuni inataka mwenyekiti kuwa madarakani kwa miaka mitano, nashangaa wamemteuwa mwingine tena bila taarifa kwangu,” ameeleza.

Kinachomshangaza ni kile alichokifafanua kuwa, hakuwahi kupewa taarifa kuhusu ama kutenda makossa au kukiuka taratibu za uongozi wa nafasi hiyo, iweje aondolewe.

Amesisitiza nafasi yake ilipaswa kukoma iwapo angefariki na kuumwa hasa ugonjwa utakaokwaza utendaji wake, lakini yeye ameondolewa ilhali hana kati ya matatizo hayo.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Katibu Mkuu wa TLP, Lyimo amesema si uamuzi wake ni sekretarieti ya chama hicho ndiyo iliyoamua.

Sekretarieti hiyo iliyoketi wiki iliyopita, amesema iliazimia kupunguza madaraka kwa viongozi wote wa TLP wenye cheo zaidi ya kimoja.

“Kwa mfano huyu Mwaka alikuwa mwenyekiti wa wanawake taifa, pia ni mwenyekiti wa chama Mkoa wa Iringa, ndiyo tumempunguzia nafasi moja ili abaki na moja,” amesema.

Amesema kwa kuwa uamuzi ulikuwa na sekretarieti jukumu lake ni kutekelea na si vinginevyo.

Si Mwaka pekee, amesema viongozi wengine wengi watapoteza moja kati ya nafasi zao kuendana na mapendekezo hayo ya sekretarieti.

“Kuna nafasi ya Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa TLP Dar es Salaam tunatafuta mtu wa kujaza nafasi moja ili tumpunguzie madaraka, hayo tutaendelea kufanya kwa kadri watakapopatikana viongozi wa kuziba nafasi hizo,” amefafanua.

Hata hivyo, uamuzi huo wa sekretarieti umetokana na kile alichokieleza kuwa, kuna wanachama wanaoongezeka hivyo si vema mtu mmoja abaki na nafasi mbili.

Chanzo: mwanachidigital