Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fukuto Chadema lazua maswali mapya

7bec9ea116f3c504d76ffc141d86bfd3 Fukuto Chadema lazua maswali mapya

Sun, 29 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOGORO uliobuka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo kuhusu sakata la viti maalumu 19 bungeni, umezua hisia tofauti miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya siasa na wanazuoni huku wengi wao wakihoji kama ni maigizo au la.

Wachambuzi na wanazuoni hao waliozungumza na HabariLEO wameeleza kuwa mgogoro huo ungeweza kuepukika na kuondokana na hatua ya kuwafukuza wanachama hao, endapo ungeshughulikiwa ndani ya vikao na watuhumiwa kupewa nafasi ya kujieleza kabla ya hukumu.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sayansi, Siasa na Utawala wa Umma Dk Richard Mbunda alisema chama hicho kingeweza kuepuka mgogoro wa kuwafukuza wanachama wake 19 endapo kingekuwa makini tangu mwanzo minong'ono ilipoanza mitandaoni kuhusu wabunge hao.

Alisema kwa mtazamo wake jambo hilo analiona kama igizo kwa kuwa chama hicho kililiacha likafika mbali hadi mitandaoni.

"Chadema ilikosea katika kusimamia jambo hilo kwani wameacha taarifa nyingi zimesambaa mitandaoni, wakashindwa kudhibiti mpaka wabunge hao 19 wakaapishwa. Matokeo yake ni kwamba wamelazimika kuwafukuza wanachama wao mahiri 19 waliobeba chama kwa muda mrefu akiwemo Halima Mdee," alisema.

Aliongeza kuwa wanachama hao 19 wamefukuzwa bila kuwepo na kusikilizwa na chama hicho hali hiyo inatoa maswali mengi kwani endapo wataamua kupambana kubomoa chama madhara yake yatakuwa makubwa zaidi.

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Maggid Mjengwa kwa upande wake, alisema kinachotokea ndani ya chama hicho sasa hivi ni mbegu inayoota iliyopandwa tangu mwaka 2019 waliposusa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Alisema kutokana na kususia uchaguzi huo chama kilikosa wabunge na madiwani hali inayowaweka waliokuwa wabunge wa chama hicho katika hali ngumu ya kiuchumi.

Kutokana na ukweli huo wabunge wa viti maalumu ambao wengi wao walikuwa wabunge hawatakubali kuachia nafasi hiyo kwa kuwa ndio njia pekee iliyobaki ya kuwaingizia kipato.

“Vyama vya upinzani vinatakiwa vijaribu kuiga mbinu za Chama Cha Mapinduzi za kuimarisha chama kuanzia ngazi za chini ili viweze kuaminika kama ambavyo CCM inaaminika kutokana na kujiimarisha katika ngazi ya chini kila baada ya uchaguzi,” alisema Mjengwa.

Alisema kitendo cha kususia uchaguzi wa serikali za mtaa kulisababisha chama kukosa uwakilishi katika ngaza za mashina. Alisema hali hiyo inasababisha chama kishindwe kujikimu katika uendeshwaji wake kwa kuwa hakina rasilimali watu wa kukiwezesha kupata fedha.

“Hivyo mgogoro huu una sababishwa na ukosefu wa fedha kutoka kupata zaidi ya milioni 300 na mtaji wa wabunge karibu 100 mpaka kufikia kukosa wabunge na kupata mmoja na fedha za ruzuku kupungua kwa kiwango kikubwa,” aliongeza.

Alisema kutokana na hali hiyo chama hicho kitarajie mgogoro zaidi wa kimaslahi kuanzia viongozi wa juu na wabunge na waliokuwa wabunge kutokana na suala zima la kimaslahi. “Walioamua kwenda kuapishwa na kukiuka msimamo wa chama wameamua mustakabali wa maisha yao,” alisema.

Vilevile Mjengwa alisema kwa sasa matamko yanayotolewa na viongozi wa juu wa Chadema ni matamko ya kisiasa zaidi ya uhalisia kutokana na ukweli kuwekwa hadharani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alishauri uongozi wa Chadema kuja na hoja kama kweli hawajawahi kutoa majina kama ambayo Tume imeleta hoja namna majina yalivyowasilishwa kwao. Vilevile wabunge 19 wanaolalamikiwa wametakiwa kupeleka hoja mahakamani ikiwa watapinga hoja zitakazotolewa na Chadema.

“Chadema wameshikilia ufunguo wa ama kusambaratika kabisa au kuzaliwa upya. Hii itategemea kwa namna gani watavyoushughulikia mgogoro huu, wakiendelea hivi hawatachukua muda watasambaratika vibaya mno,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mchambuzi wa Masuala ya Kiuchumi na Siasa nchini Gabriel Mwang’onda aliliambia HabariLEO kinachoendelea ndani ya Chadema ni kukabiliana na athari za nguvu za Baraza la Wanawake ndani ya chama baada ya viongozi wa juu kutaka kupoka madaraka yao.

Alisema kimsingi nguvu ya Chadema inastawishwa na hazina kubwa ya wabunge wake wa kike waliojengwa kwa misingi ya chama kama vile Halima Mdee na Esther Matiko wakiungana na wabunge kama Esther Bulaya, Naghenjwa Kaboyoka na wengine.

“Chadema ndio watakaoshindwa katika mgogoro huu kwa sababu waliosababisha Chadema isimame na kujinasibu walikuwa wabunge hao ambao ndio kioo cha chama kwa sasa,” alisema Mwang’onda.

Alisema Chadema kimeshashindwa katika hatua za awali kutokana na kutoa adhabu ya kuwavua nyadhifa wabunge hao pamoja na kuwafukuza uanachama kitu ambacho kinaeleweka kwa kuwa walishafanya makosa kwa mujibu wa msimamo wa chama.

“Kinachoshangaza hapa ni swali alilotakiwa aulizwe Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema) ni kuwa iweje watu mliowapa adhabu ya kuwapokonya nyadhifa zao na kuwafukuza uanachama muwape nafasi ya kukata rufaa? Ikiwa wataomba msamaha mtawakubalia,” alisema Mwang’onda.

Juzi saa tano usiku, Mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe, alitangaza uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu wabunge hao 19 wa viti maalumu walioapiswa kuwa wabunge, ambao ni kuwafukuzwa uanachama wanachama Halima Mdee na wenzake 18 kwa tuhuma za usaliti.

Kikao cha kamati kuu kilifanyika juzi jijini Dar es Salaam huku wajumbe wawili wa kikao hicho, Tundu Lissu, makamu mwenyekiti wa Chadema-bara na Ezekiel Wenje wakishiriki kwa njia ya mtandao.

“Wabunge wetu hawa 19, mama zangu na dada zangu wameapishwa kiapo batili kwani Katiba inasema waapishwe mbele ya Bunge. Sasa kanuni zimebadilishwa ili kumruhusu Spika kumwapisha popote hata eneo la gereji.”

Hata hivyo, Spika wa Bunge Job Ndugai hivi karibuni alieleza kuwa uapisho wa wabunge hao nje ya Bunge ni moja ya mabadiliko ya kanuni yaliyopitishwa katika Bunge la 11 ambapo sasa mbunge anaweza kuapishwa mbele ya Spika nje ya Bunge, na wakati wa vikao vya Bunge, Spika atatakiwa kumtangaza mbunge huyo mpya.

“Kamati kuu imewavua nyadhifa zao zote ndani ya chama na kuanzia sasa wasijihusishe kwa namna yoyote na masuala ya chama. Wako waliokuwa viongozi Bawacha na wengine Bavicha. Kamati tendaji za mabaraza hayo zikutane kujaza nafasi hizo.” Alisisitiza Mbowe.

Wabunge wengine pamoja na Mdee walifukuzwa uanachama ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ni Ester Bulaya na Esther Matiko. Katibu Mkuu wa Bavicha, Nusrat Hanje. Katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), na Grace Tendega.

Chanzo: habarileo.co.tz