Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Filamu ya Balozi Kagasheki, Dk Amani kurudi kivingine

18083 Pic+balozi TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mvutano wa kisiasa kati ya wanasiasa wawili, Mbunge wa zamani wa Bukoba, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa zamani wa Manispaa ya Bukoba Dk Anatory Amani unafanana na filamu iliyowachosha watazamaji baada ya kuendelea kwa muda mrefu bila mshindi kupatikana.

Viongozi hao walitofautiana kwa hoja na hivyo kuwagawa watazamaji ambao waliunda vikundi vya upambe na kuanzisha mashambulizi ya maneno kwenye vijiwe vya kahawa kwa kudandia hoja za wanasiasa hao.

Hatimaye Dk Amani alihama CCM na kujiunga na NCCR-Mageuzi mwaka 2015 na kutetea nafasi yake ya udiwani katika Kata ya Kagondo lakini akashindwa kurejea katika umeya; Kwa upande wa pili, Balozi Kagasheki akapoteza jimbo la Bukoba Mjini dhidi ya mgombe wa Chadema, Wilfred Lwakatare.

Baada ya kutangaza kurejea CCM hivi karibuni, Dk Amani ametangaza kuwasamehe maadui wake wote, miongoni mwao wakiwamo saba ambao alikuwa tayari amewasajili katika kundi la ‘adui namba moja’.

Katika mkutano wa ‘ndani’ uliofurika mamia ya wanachama wa Kata ya Hamugembe, hivi karibuni, Katibu wa CCM katika Manispaa ya Bukoba, amefanya upatanisho usio rasmi akimtaka Kagasheki kurejea ulingoni kuwanadi wagombea wa CCM pindi kampeni za uchaguzi mdogo zitakapoanza.

Wakati mkutano ukiendelea katibu huyo anatoa taarifa ya kupokea ujumbe aliotumiwa na Kagasheki kwa njia ya simu, akikubali kushiriki hatua zote za kampeni za wagombea wa CCM katika kata za Hamugembe na Kagondo ambako madiwani wamejiuzulu.

Kama ilivyofanyika katika kata zote ambazo madiwani wa upinzani wamerejea CCM, hata jina la Dk Amani linatarajiwa litapita bila kupingwa kuwania tena udiwani katika Kata ya Kagondo na pengine Balozi Kagasheki ataongoza timu ya ushindi.

Kosa la kwanza

Pamoja na kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatangaza kuanza kwa kampeni katika kata za Hamugembe na Kagondo, wagombea wa CCM tayari wanajulikana na viongozi wamekwishawaombea kura katika mkutano huo wa kuwakaribisha.

Katibu wa CCM Manispaa ya Bukoba, Mohamed Ali anatoa onyo kwa mwanachama atakayeonyesha nia ya kugombea katika kata hizo kuwa atachukuliwa hatua za kinidhamu na uchunguzi utafanyika dhidi yake.

Anaomba wanachama ambao tayari wameunda mitandao kwa maandalizi ya kugombea nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 waunganishe nguvu kukomboa kata hizo kwanza ambazo zilikuwa zinaongozwa na upinzani.

Hata hivyo, lawama na karipio dhidi ya baadhi ya viongozi wa ngazi ya wilaya ambao waling’oka au kung’olewa, kwa tuhuma kuwa walishiriki kukiangusha chama na kukifikisha hapo kilipo, ni shambulizi ambalo halikutakiwa kufanyika hadharani.

Baadhi yao bado wana nguvu ya ushawishi kwenye siasa ndani na nje ya chama. Hata kama hawahitajiki katika uchaguzi mdogo wa madiwani, nguvu yao inaweza kujitafsiri kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na nyingine zijazo.

Katika kusanyiko hilo kilichosahaulika ni kuwa kilichowafikisha hapo walipo ni viongozi kukosoana hadharani, jambo ambalo huchochea mgawanyiko zaidi na kuwa na chanzo cha kuibuka kwa makundi yanayoanzisha hoja za utetezi dhidi ya mashambulizi yanayofanyika hadharani.

Ugumu wa Hamugembe

Kata ya Hamugembe ni miongoni mwa kata 14 za Manispaa ya Bukoba ambayo matukio ya kihistoria kwenye majukwaa ya kisiasa yanaifanya itofautiane na kata nyingine. Imewahi kuongozwa na madiwani wa vyama vya CCM, CUF na Chadema kwa vipindi tofauti.

Wapiga kura wa kata hiyo kilio chao hakijawahi kubadilika kwenye suala la ubovu wa miundombinu ya barabara na maji, ambapo hata madiwani wa vyama tofauti waliotangulia walitoa ahadi ambazo hazikutekelezeka.

Kero hizi na nyinginezo ndizo zimechangia wananchi kujikuta wanabadili madiwani kwa vipindi tofauti na vyama vyao kama njia ya kutafuta majibu ya changamoto zao, hivyo wana uzoefu wa kutosha na lugha tamu za madiwani.

Uchaguzi wa kata ya Hamugembe pia utabeba mvuto wa kijimbo, ikitegemewa wapambe wa wagombea wa vyama watakaopitishwa watasafiri kutoka katika kata zao na kwenda kuongeza idadi kwenye mikutano ya kampeni.

Pamoja na kuwa Dk Amani anategemewa kuwa katika kibarua cha kurudisha udiwani wake katika kata ya Kagondo, pia inatarajiwa ataonekana mara nyingi kwenye jukwaa moja na Balozi Kagasheki wakimnadi Muhaji Kachwamba aliyerejea CCM akitokea Chadema.

Wanasiasa hao wanatarajiwa kutangaza mbele ya umma wakati wa kampeni hizo kuwa wamezika tofauti zao, huku kila mmoja akionyesha umahiri wake wa kuumba maneno wakati akijitetea kwa mambo yaliyopita.

Ajenda ya tetemeko

Kwa vyovyote vile ajenda ya tetemeko la ardhi inatarajiwa kukoleza uzito wa kampeni za udiwani katika Kata ya Hamugembe. Kwa kuwa bado kuna makovu ya tukio hilo wagombea wanatakiwa kuchagua maneno ya kuongea hasa wakati wa kutafuta kura nyumba kwa nyumba.

Hii ndiyo kata ambayo katika tukio hilo la Septemba 10, 2016 watu wanane katika mtaa wa Omukishenye walipoteza maisha. Hivyo suala la msiba ulioikumba kata hiyo halikwepeki wakati wanasiasa na wapambe wao watakapokuwa majukwaani wakiomba kura.

Mtaa wa Omukishenye ulitembelewa zaidi na viongozi tofauti kujionea maafa ya tetemeko na baadhi yao wanatarajiwa kuonekana tena wakati wa kampeni wakiomba kura na kuwaeleza waathirika jinsi walivyoshughulikia janga lililowapata.

Kampeni za nyumba kwa nyumba zinaweza kuwa ngumu zaidi katika mtaa huu kwa kuwa baadhi ya familia ziko kwenye mahema baada ya kushindwa kujimudu tena. Katika kuomba kura katika familia hizi mgombea anahitaji ujasiri wa ziada.

Kwa wanasiasa ambao hawakufika kutoa pole wakati wa janga hilo ujio wao wakati wa kampeni unaweza kukoleza mijadala ya wapambe kwenye vijiwe vya kahawa kuhusu thamani ya mpiga kura wakati wa shida na umuhimu wake wakati wa uchaguzi.

Upinzani washtuka

Kuondoka kwa madiwani wa Hamugembe na Kagondo na kurejea CCM, ulikuwa mwanzo wa kutimua vumbi kwenye kambi ya upinzani na kusababisha baadhi ya madiwani kutiliwa shaka kuwa nao wako njiani kuondoka.

Uvumi huo ulizimwa na diwani wa Kashai, Nuruhuda Kabaju aliyejitokeza hadharani na kukanusha madai ya kupokea gharama za uhamisho, huku akikubali kuwa miongoni mwa wanasiasa waliokuwa wanawindwa.

Katika mkutano na waandishi wa habari, diwani huyo alishauri kama kuna fungu limeandaliwa kwa ajili ya kufanikisha mipango ya kumhamisha ni bora likaelekezwa kwenye huduma nyingine za kijamii kama barabara, maji na umeme.

Hata hivyo, shutuma za madiwani kurubuniwa kwa fedha na ahadi nyingine zinakanushwa mara zote na viongozi wa CCM wanaodai wimbi la madiwani na wabunge kuukimbia upinzani ni baada ya chama hicho kupata mvuto mpya unaotokana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.

Utekelezaji wa ilani ya chama hicho pia umesisitizwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo ambaye hivi karibuni amewataka wananchi kujitenga na uvumi kuwa miradi yao inakwamishwa na Serikali makusudi.

Anasema kuwa kituo cha Afya cha Zamzam kimeboreshwa kwa gharama kubwa kama sehemu ya miradi iliyotekelezwa na Serikali kwa ajili ya wananchi na kuwa kama ingekuwa ni kukwamisha miradi kituo hicho kisingeboreshwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz