Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Figisufigisu zamuibua Lipumba

Video Archive
Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwenyekiti wa Cuf anayetambuliwa na Msajili ya Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba ameungana na wapinzani wengine kudai kuwa chaguzi ndogo zinazoendelea nchini hazizingatii demokrasia na zimekuwa zikigubikwa na ukandamizaji.

Profesa Lipumba alikwenda mbele na kuitaka Serikali kutamka wazi kama Tanzania ni nchi ya chama kimoja, ili kuwaondolea wapinzani usumbufu wa kushiriki uchaguzi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema hakuna maana kujiita nchi ya kidemokrasia wakati nguvu zinatumika kuifanya CCM kuendelea kuongoza.

“Kama vipi bora turejee mfumo wa chama kimoja kama ilivyo China lijulikane moja, nchi ya chama kimoja na tujifunze kutoka kwao wanaendeshaje nchi kuliko hii tunasema tufanye uchaguzi halafu watu wanakwenda kuchukua fomu wanatekwa, wanazuiliwa au kunyang’anywa,” alilalamika.

Alisema itafika wakati watu watachoka kuonewa na kujikuta wanaamua kuliingiza Taifa kwenye machafuko.

Alitoa kauli hiyo kwa kile alichodai kuwapo kwa wanachama wa Cuf ambao walitaka kugombea udiwani, lakini wamekutana na vitendo vya hujuma ili wasishiriki.

Profesa Lipumba alisema wagombea hao kutoka Kibiti na Mkuranga walifanyiwa hujuma ikiwamo kuporwa fomu, kutekwa na wengine kunyimwa fomu.

“Nataka niwapeleke wagombea hawa (anawaonyesha) kule tume wakaelezee majanga yaliyowakuta, isiwe watu wanajigamba wamepita bila kupingwa kumbe kuna michezo yao wameifanya.

“Kama tumeamua kuwa nchi ya demokrasia basi tuzingatie misingi ya demokrasia siyo kutumia nguvu na kuzuia wengine wasishiriki,” alisema.

Lipumba aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mkutano wa baraza kuu la chama hicho unaolenga kujadili mambo kadhaa, huku ajenda kuu ikiwa ni matatizo yaliyopo na kutoka na majibu nini kifanyike ili wananchi wapate haki na furaha.

“Hali siyo nzuri tusijidanganye, hii ni nchi yetu sote hakuna mtu mwenye haki miliki lazima tujenge misingi ya demokrasia,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Chama chetu kinaamini kwenye demokrasia kila mtu awe huru ili mradi havunji sheria.”

Chanzo: mwananchi.co.tz