Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Duni na mzigo wa viatu vya Maalim Seif

Dunipic Juma Haji Duni, Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo

Thu, 3 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wiki iliyopita, chama cha ACT Wazalendo kilihitimisha safari ya miezi 11 bila kuwa na mwenyekiti wake baada ya Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa kwenye nafasi hiyo kufariki Februari 17, mwaka jana.

Kufariki kwa mwanasiasa huyo mkongwe lilikuwa pigo kubwa kwa Taifa, chama hicho hasa kwa upande wa Zanzibar kutokana na nguvu ya ushawishi wake katika visiwa hivyo na katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Ili kujaza nafasi hiyo, ilibidi chama kiitishe mkutano mkuu ambao unahusisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini ili wafanye uchaguzi wa mwenyekiti na nafasi nyingine zilizokuwa wazi katika kipindi hicho.

Kiongozi wa chama, Zitto Kabwe anasema baada ya kufariki kwa Maalim Seif, chama kilipitia changamoto kubwa mbili, ambazo ni kujaza nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa chama.

“Kuna watu walianza kuandika tanzia kwamba sasa chama ndiyo kinakufa, lakini tukavuka salama,” alisema Zitto na kuwataka wajumbe wasimwangushe, bali wapite vizuri katika hatua hiyo ya uchaguzi.

Mkutano mkuu huo ulihudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wa dini; Askofu Emmaus Mwamakula, Sheikh Issa Ponda, Padri Godfrey Nestory na viongozi wa vyama vingine vya siasa.

Pia, walikuwepo wanasiasa kutoka nchi marafiki wa chama hicho ambao ni kiongozi wa muungano wa CCC huko Zimbabwe, Nelson Chamisa na Cindy Kauka ambaye amemwakilisha Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema kutoka chama tawala cha UPND.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ambaye aliwapongeza ACT Wazalendo kwa kufanikisha mkutano huo kwa kuzingatia matakwa ya sheria katika kujaza nafasi ya mwenyekiti iliyokuwa wazi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Nyahoza alivitaka vyama vya siasa nchini viendelee kuboresha demokrasia ya ndani kwa sababu ndiyo msingi wa kuimarisha demokrasia ya nchi.

“Vyama vya siasa muanze na demokrasia ndani ya vyama vyenu, mkishakuwa na demokrasia ndani ya chama, hata nje itakuwa rahisi,” alisema Nyahoza.

Alikipongeza chama hicho kwa kufanya siasa za kistaarabu na kushiriki katika mkutano wa wadau uliofanyika Dodoma na kuwataka waendelee hivyo na kunapokuwa na changamoto Basi njia bora ni mazungumzo kama alivyokuwa akifanya Hayati Maalim Seif.

Duni achaguliwa

Wajumbe wa mkutano mkuu wa ACT Wazalendo walimchagua Juma Duni Haji kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho, akijaza nafasi ya Maalim Seif ambaye walifanya kazi pamoja tangu walipokuwa CUF.

Duni, ambaye alikuwa akishindana na Hamad Masoud Hamad, alipata kura 339 sawa na asilimia 73.06 ya kura 464 zilizopigwa, wakati mpinzani wake huyo naye akipata kura 125, sawa na asilimia 26.94.

“Kwa matokeo haya, ninamtangaza Juma Duni Haji kuwa mwenyekiti wa chama,” alisema mwenyekiti wa uchaguzi, Joram Bashange wakati akitangaza matokeo hayo, huku wajumbe wa mkutano huo wakishangilia.

Kwa upande wa nafasi ya makamu mwenyekiti, wajumbe walimchagua Othman Masoud Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa kura za “ndiyo” 443, sawa na asilimia 98.83 ya kura zilizopigwa.

Othman alikuwa akishindana na Juma Said Saanane katika nafasi hiyo, hata hivyo, Saanane alijitoa kwenye kinyang’anyiro hicho siku moja kabla ya uchaguzi.

Akitoa shukrani baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Duni aliwashukuru wanachama kwa kufanikisha uchaguzi huo salama na kwa kumwamini kuongoza chama hicho.

“Nawashukuru sana kwa dhamana hii, tumeweza kuvuka salama hata katika hili, nawashukuruni sana wajumbe,” alisema Duni, huku hotuba yake ikikatishwa na shangwe za wanachama.

Duni ni nani?

Duni alizaliwa mwaka 1950 huko Zanzibar, alisoma shule ya msingi Mkwajuni kati ya 1959 - 1965, baadaye akajiunga na sekondari ya juu ya Lumumba kati ya mwaka 1966 - 1969.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) kwa masomo ya shahada ya kwanza ya elimu ya Sayansi kuanzia mwaka 1972 - 1975. Baadaye mwaka 1994 - 1995 alisoma shahada ya uzamili ya rasilimali watu katika Chuo Kikuu cha Manchester huko Uingereza.

Mwanasiasa huyo amefanya kazi Serikali ya Zanzibar katika nafasi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango (1981 -1982), Katibu Mkuu - viwanda (1980 -1981), ofisa mipango - elimu (1976 -1979) na mwalimu wa sekondari (1975 - 1979).

Katika medani za siasa, Duni pia ameshika nafasi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na makamu mwenyekiti wa ACT Wazalendo, naibu kiongozi wa chama, Waziri wa Afya katika serikali ya Umoja wa Kitaifa, naibu katibu mkuu wa CUF, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF.

Wadau walonga

Wakizungumzia kuchaguliwa kwa Duni katika nafasi hiyo, wachambuzi wa siasa na wanazuoni wamesema mwanasiasa huyo ni chaguo sahihi katika nafasi hiyo, kwa sababu ana uzoefu na alikuwa mstari wa mbele kwenye mapambano sambamba na Maalim Seif.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema Duni anakabiliwa na changamoto ya kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar, kwa sababu siasa katika visiwa hivyo ni ngumu kiasi cha kutishia SUK.

Anasema kiongozi huyo atakuwa na wajibu pia wa kuimarisha demokrasia kwa kufanya mazungumzo na kuwashawishi upande wa pili ili demokrasia ichukue nafasi yake, hasa huko Zanzibar ambako ana ushawishi mkubwa.

“Kwa uzoefu alionao katika siasa, ni mtu ambaye anaweza kusukuma ajenda za Maalim Seif. Hawezi kuwa kama yeye lakini ana uwezo wa kuzibeba ajenda zake. Nina uhakika Duni ni chaguo sahihi hasa kwa siasa za Zanzibar,” anasema.

Dk Loisulie anaongeza kuwa Duni atakuwa na jukumu la kusukuma ajenda ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na kuchangamana na vyama vingine. vya siasa hasa vya upinzani ili wafanye kazi pamoja.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Francis Malila anasema Duni ni kiungo muhimu upande wa Zanzibar, atakisaidia chama hicho kuimarika zaidi hasa wakati huu baada ya Maalim Seif kufariki.

Anasisitiza kwamba kiongozi huyo anakabiliwa na changamoto ya kulinda ushindi ushindi wa chama chake wakati wa uchaguzi huko Zanzibar na kukifanya kiendelee kuwemo kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Sina mashaka na Duni, ni mpambanaji aina ya Maalim Seif, ana misimamo yake. Nadhani atafanikiwa kuwaunganisha Wazanzibar kupitia chama hicho kilichokuwa kikiongozwa na Maalim Seif,” anasema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live