Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Duni awatwisha jukumu ACT-Wazalendo

Piic Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Juma Duni Haji

Sat, 7 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho mkoani Mwanza kuweka mikakati ya ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Akisalimiana na wana ACT-Wazalendo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa ofisi za chama hicho mkoa wa Mwanza leo Mei 6, Duni ambaye ni maarufu kwa jina la "Babu Duni" amewataka viongozi na wanachama hao kuweka msingi wa ushindi wa nafasi za udiwani, ubunge na urais katika uchaguzi mkuu ujao kwa kushinda kwanza nafasi za wenyeviti na wajumbe wa Serikali za Mitaa.

"Njia ya kufikia malengo hayo ni kunadi sera za chama kupitia siasa safi na za kistaarabu za kujenga hoja kujadiliana; siyo siasa za kibabe na kuhasimiana. Kule Zanzibar tulijaribu siasa za kibabe tukagundua haziwezi kutufikisha kwenye lengo la kujenga Taifa na mimi ni miongoni mwa waathirika," amesema Duni

Mbele ya Kiongozi wa chama, Zitto Kabwe, Makamu Mwenyekiti, Dorothy Seni na Katibu Mkuu, Addo Shaibu ambao pia wamehudhuria hafla hiyo, "Babu" Duni amewataka wana ACT-Wazalendo kuteka mioyo ya Watanzania kupitia siasa zinazopigania na kupata haki, usawa na ushindi katika ulingo wa siasa bila kufarakana wala kuhasimiana miongo.

"Harakati za kisiasa zinalenga mabadiliko, ustawi na maendeleo ya wananchi; hakuna maendeleo yanayopatikana penye vurugu. Sisi ACT-Wazalendo tuonyeshe tofauti kati yetu na wengine kwa kufanya siasa safi za kujenga hoja na majadiliano," amesisitiza

Viongozi wa ACT-Wazalendo wakiongozwa na Zitto wako mkoani Mwanza katika wiki ya miaka minane ya kuanzishwa kwa chama hicho kwa kushiriki shughuli kadhaa ikiwemo uzinduzi na ufunguzi wa matawi, utoaji wa misaada ya kijamii na kuchangia damu.

Chama hicho leo kitafanya kongamano la Kitaifa la kudai mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa kuweka mazingira bora ya kisiasa ikiwemo kuundwa kwa Tume huru ya uchaguzi na hatimaye Katiba Mpya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live