Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Duni, Masoud mmoja kumrithi Maalim Seif

0804ac3f5d8591d71ed6a71a63662392.png Duni, Masoud mmoja kumrithi Maalim Seif

Wed, 19 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji pamoja na waziri wa zamani, Masoud Hamad Masoud ndio wagombea pekee waliojitokeza kutaka kurithi kiti cha Uenyekiti kilichoachwa na Mwenyekiti Maalim Seif Sharif Hamad.

ACT-Wazalendo kinatarajia kupata Mwenyekiti wa Taifa Januari 29, mwaka huu mkoani Dar es Salaam katika Mkutano Mkuu utakaofanyika Ukumbi wa Mlimani City, Mwenge na kufanya uchaguzi kwa wagombea waliojitokeza kuwania nafasi tatu zilizoachwa wazi.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Joram Bashange alitoa taarifa hiyo jana mkoani Dar es Salaam wakati alipozungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya Mkutano Mkuu huo.

Bashange alisema mpaka kazi ya uchukuaji na urudishaji fomu inafungwa juzi, wanachama 11 walijitokeza kutaka kujaza nafasi zilizoachwa wazi ikiwemo ya Mwenyekiti kutokana na kifo cha Maalim Seif aliyefariki dunia Februari 17, mwaka jana.

Alisema mchakato wa kujaza nafasi hizo ulianza Januari 4 ikiwa ni uchukuaji wa fomu na urejeshaji wa fomu hizo na kuhitimishwa juzi Januari 17, mwaka huu ambapo jumla ya wagombea waliojitokeza kutaka kujaza nafasi tatu ni 11.

Alisema nafasi zinazotakiwa kujazwa ni ya Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti wa Taifa kutoka upande wa Zanzibar na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nafasi moja. Aliongeza kuwa kwa nafasi ya Mwenyekiti Taifa, waliojitokeza ni wawili ambao ni Juma Duni Haji kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja na Masoud Hamad Masoud kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba.

“Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Taifa ambayo ni nafasi inayotakiwa kujazwa na mtu kutoka Zanzibar, ina wagombea wawili ambao ni Othman Masoud Othman kutoka Kaskazini Pemba na Juma Saidi Saanani kutoka Mjini Magharibi Unguja,” alisema Bashange.

Kwa upande wa nafasi moja ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu inagombewa na wajumbe kutoka Tanzania Bara kwa kuwa mwanachama aliyefariki anatoka Bara, ina wagombea saba ambao ni Chrisant Joseph Msipi kutoka Shinyanga, Esther Thomas na Fungo Godlove wote kutoka Dar es Salaam, Johnson Mauma kutoka Arusha, Msafiri Mtemelwa na Fidewil Christopher wote kutoka Tabora na Japhet Masawe kutoka Kilimanjaro.

Bashange alisema baada ya kazi ya kurudisha fomu kufungwa, Kamati ya Uchaguzi itakaa leo kuandaa taarifa ya wagombea wote na kuiwasilisha kwa Sekretarieti ambayo nayo itakaa Januari 22 kuandaa kikao cha Kamati Kuu.

Alisema Kamati Kuu itakaa kikao Januari 27, mwaka huu na kuandaa taarifa na taratibu za kikao cha Halmashauri Kuu itakayokaa Januari 28 na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea na kampeni zitafanyika siku hiyo hiyo kupitia mdahalo wa wazi kisha kuitisha Mkutano Mkuu Januari 29 ili wajumbe wafanye uchaguzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live