Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Tulia awataka wabunge kuvishtaki vyombo vya habari mahakamani

64044 Pic+tulia

Mon, 24 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Naibu Spika wa  Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amewataka wabunge wanaotajwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuhusika na mambo ambayo hawajayafanya kufungua kesi mahakamani, si kutaka Bunge kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 24, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu mwongozo wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe aliyedai baadhi ya vyombo hivyo vinaandika habari za kuwachafua wabunge, baadhi wakitajwa kuhusika katika vitendo vya rushwa.

“Siku za hivi karibuni kuna magazeti (anayataja) yanaandika habari za kuwachafua wabunge hasa linapotokea jambo zito la kitaifa. Lipo moja limewataja wabunge kuwa  wamepokea rushwa. Kwanini Bunge lisione ulazima kwa wahariri wa magazeti hayo kuitwa mbele ya kamati ya maadili  maana wanachafua mhimili wa Bunge,” amesema Mwambe.

Akijibu mwongozo huo, Dk Tulia amesema licha ya jambo hilo kutotokea bungeni leo kwa mujibu wa kanuni za chombo hicho cha kutunga sheria ili liweze kupatiwa majibu stahiki, lakini habari kuhusu mbunge kuandikwa gazetini haiwezi kujadiliwa bungeni.

“Ninawashauri tu kama mbunge umeandikwa vibaya kwenye gazeti au chombo chochote cha habari unapaswa kwenda mahakamani,” amesema Dk Tulia.

Chanzo: mwananchi.co.tz