Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Tulia akabidhi mil 61/- kusaidia kujenga madarasa

52f421dc2a06cab969569914e0fd28c0 Dk Tulia akabidhi mil 61/- kusaidia kujenga madarasa

Tue, 19 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson, ametoa Sh 60,574,000 kwa Shule ya Sekondari ya Iduda iliyopo jijini Mbeya ili kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa ya kidato cha tano na cha sita.

Alikabidhi fedha hizo jana katika hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo zikiwa ni fedha za mfuko wa jimbo zilizotolewa na serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021.

"Fedha hizo tulizozitoa zina uwezo wa kujenga madarasa matatu tutakayoanza nayo na huo ujenzi utaanza mara moja kwa sababu fedha zipo. Mbeya Mjini safari hii tunahitaji maendeleo na hatutarajii kuona mtu wa kutukwamisha,” alisema.

Akaongeza: “Niwaombe sana, fedha hizi hazitatosheleza kujenga na kufikia mahitaji yetu yote kwa sababu bado tutahitaji pia mabweni hivyo basi, tunapaswa kushirikiana kwa umoja wetu kila mmoja anapoweza hata kutoa nguvu kazi ikiwemo kuleta mawe."

Alisema Jiji la Mbeya ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na uhaba wa shule za sekondari zenye kidato cha tano na sita, hivyo ni wakati kwa wadau kuwekeza kwenye eneo hilo.

"Kama tunavyofahamu, wilaya yetu imekuwa na uhaba mkubwa wa shule za sekondari zenye kidato cha tano na sita na zaidi, katika bonde letu la Uyole hakuna hata shule moja.”

“Leo tumekuja hapa baada ya kukubaliana kwamba, fedha zote za mfuko wa jimbo zitaelekezwa hapa Iduda kwa ajili ya ujenzi wa shule," alisema Dk Tulia.

Akaongeza; "Safari hii mtoto aliyeongoza kidato cha nne ametoka hapahapa Mbeya, hivyo tunataka tuendelee kuweka mazingira mazuri ili kuongeza ushindani mzuri zaidi katika siku za usoni na ikibidi, Mbeya tuendelee kuwa vinara wa elimu nchini."

Chanzo: habarileo.co.tz