Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Tulia abebeshwa zigo, changamoto uhaba wa maji

SPIKA TULIA ARUSHA Dk Tulia abebeshwa zigo, changamoto uhaba wa maji

Sat, 30 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi wa Kijiji cha Kibatala Kata ya Kisondelo, wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya, wamefanya mapokezi ya aina yake kwa Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson kwa kumwaga maji huku wakilala kwenye tope kama ishara ya uhaba wa maji kijijini hapo.

Dk Tulia ambaye ni Spika wa Bunge amekutana na mapokezi hayo leo, Jumamosi Desemba 30, 2023 mara baada ya kuwasili na kuzungumza na wananchi kabla ya kukabidhi nyumba kwa mlemavu wa viungo Ambele Mwakipesile (36).

Miongoni mwa waliokuwa wamelala chini ni mkazi wa kijiji hicho, Queen Kenneth amesema kumekuwepo na changamoto kubwa ya maji hali inayosababisha watumie muda mwingi kusaka maji kwenye mito na mifereji.

“Spika umefika kwenye kijiji chetu changamoto kubwa ni maji tunatumia ya mito na mifereji licha ya wadau mbalimbali kutusaidia, ndoa zinavunjika, wajawazito wanapata tabu kwani tunatembelea umbali wa kilometa 5.”amesema.

Kwa upande wake, Mbunge Viti Maalum, Sophia Mwakagenda ambaye alikuwapo kwenye hafla hiyo amemuomba Dk Tulia kusaidia katika utatuzi wa changamoto hiyo ya maji kwa kuwa jambo hilo liko ndani ya uwezo wake.

“Dk Tulia umekuwa mtu wa kujishusha sana kwa wananchi na kuwaunganisha katika maendeleo bila kujali vyama vya siasa, Mkoa wetu wa Mbeya unahitaji maendeleo na nitaendelea kukuombea na kuunga mkono jitihada zako,” amesema.

Akijibu juu ya changamoto ya maji katika kijiji hicho, Dk Tulia amesema: “Nimeona mmenipokea kwa kilio cha maji kwa kumwaga chini na kulala, huku mfano wa wajawazito wakiwa wamebeba watoto mgongoni na ndoo kichwani, ikiwa ni tafsiri ya ukosefu wa huduma ya maji.”

Mbunge huyo wa Mbeya Mjini amesema alatifikisha suala hilo kwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso ili lipatiwe ufumbuzi.

Aidha, Dk Tulia amekemea tabia ya baadhi ya wanaume wanaotekelekeza familia zenye watoto wenye ulemavu sambamba na kuitaka jamii kujitolea kuwasaidia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rungwe, Mpokigwa Mwankuga amekiri kuwepo kwa changamoto ya maji na kuomba Serikali kuliangalia hilo kwa upana ili kuondoa adha kwa wakinamama kutembelea umbali mrefu.

”Serikali kimetoa Sh 3.4 bilioni kutekeleza mradi wa maji katika vijiji vya Ndubi na Bugoba ambao ukikamilika utapunguza adha kwa kiwango fulani,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live