Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Tulia aahidi mambo matatu

Tulia (3) Dk. Tulia Ackson Spika Tanzania

Thu, 3 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Spika mpya wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameahidi mambo matatu atakayotekeleza kwenye uongozi wake baada ya kuchaguliwa kwa kura 376 kuongoza mhimili huo.

Idadi hiyo ya kura ni sawa na idadi ya wabunge waliokuwamo ukumbini jana kutoka vyama vya ACT-Wazalendo, Chadema, CUF na CCM yenye wabunge wengi.

Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na mbunge mwenye umri mrefu bungeni, William Lukuvi (Isimami), wagombea wengine wanane walioshindana na Dk Tulia hawakuambulia kura hata moja.

Wagombea wengine katika kinyang’anyiro hicho walikuwa Abdullah Mohamed Said (NRA), Aivan Maganza (TLP), David Mwaijojele (CCK), Georges Bussungu (ADA-Tadea) na Maimuna Kassim wa ADC.

Wengine ni Kunje Ngombale Mwiru (SAU), Ndonge Saidi Ndonge (AAFP) na Sadoun Abrahmani Khatibu (DP). Wote walitoka katika vyama visivyo na wabunge.

Uchaguzi huo ulifanyika kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa spika wa Bunge, Job Ndugai Januari 6, 2022 na CCM kupitisha jina la Dk Tulia kama mgombea pekee kati ya makada 70 waliochukua na kurudisha fomu.

Dk Tulia anakuwa Spika wa saba wa Bunge tangu uhuru. Maspika wengine waliotangulia ni Adam Sapi Mkwawa, Chifu Erasto Mang’enya, Pius Msekwa, Samuel Sitta, Anne Makinda na Ndugai.

Mambo atakayosimamia

Dk Tulia alisema anatamani Bunge liwe daraja la mfano kati ya Serikali na wananchi na ataliongoza kwa umakini ili liweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Alisema atawapa wabunge nafasi ya kuuliza maswali na kuihoji Serikali “kwa hekima na busara” huku wakizingatia kiapo chao.

Pia, alisema hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni Aprili 22, 2021, itakuwa ndiyo ni dira yake ya kuliongoza Bunge.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia ilielezea vipaumbele kwa ajili ya nchi, ikiwemo kuimarisha uchumi wa nchi, kuvutia wawekezaji, kukuza uchumi kwa asilimia nane, kuleta nidhamu katika kusimamia mali za nchi na kuwawajibisha wazembe na wabadhirifu wa mali za umma.

Katika salamu zake, Dk Tulia alimtaja mtangulizi wake, Ndugai kuwa ni miongoni mwa waliomsaidia kufika mahali alipo sasa, huku akisema alimpatia nafasi akiwa msaidizi wake kiasi cha uwezo na kipaji chake kuzidi kukua.

“Namshukuru Spika mstaafu Mheshimiwa Job Ndugai kwa namna alivyonifunza mengi, alinielekeza, alinishauri na kuniongoza vizuri, alinipa fursa mbalimbali katika kukuza uongozi wangu. Tunamtakia maisha mema ya kustaafu kwake,” alisema Dk Tulia.

Ndugai, ambaye jana hakuonekana bungeni, alipotajwa na Dk Tulia wabunge walipiga zaidi makofi.

Kauli za wagombea

Awali alipoomba kura, Dk Tulia aliwaomba wabunge waondoe hofu kwa sababu chombo hicho hakitakuwa na unyonge kama baadhi wanavyodhani, akasisitiza kuwa mihimili yote ifanye kazi yake kwa kufuata misingi ya sheria.

Kwa upande wa wagombea wengine, Abdullah Said alisema uwezo wa kuongoza anao na amepewa nguvu nyingi na mke wake, hivyo aliomba wamchague kwa sababu angeenda kubadilisha hadhi ya Bunge.

Kwa upande wake David Mwaijojele, aliomba apewe nafasi hiyo kwa kuwa ni “mtu wa watu” (akimaanisha askofu), hivyo ataongoza kwa hekima ya Mungu.

Aivan Maganza aliomba wabunge wamchague akarekebishe sera ya vijana wakati Georges Bussungu aliahidi kuongoza kwa uzalendo bila kufuata itikadi za vyama na dini.

Kunje Ngombale Mwiru alitembelea turufu ya kupunguza vikao vya wabunge na kuongeza posho, huku akiahidi kuunda kikosi kazi cha kuwafuatilia wabunge ili waende majimboni.

Ahadi nyingine za wagombea zilitolewa na Maimuna Kassim aliyeomba kuchaguliwa ili afanye Bunge kuwa na umoja huku Ndonge Saidi Ndonge akitumia turufu ya Rais Samia katika ujenzi wa madarasa na Sadoun Abrahman Khatibu akitaka achaguliwe ili kuleta mshikamano baina ya Bunge, wananchi na Serikali.

Matarajio kwa Tulia

Akizungumza na Mwananchi baada ya uchaguzi huo, Spika Mstaafu, Anne Makinda alitoa wito kwa wanawake waliopewa nafasi za uongozi kuwa na nidhamu na kuwajibika zaidi.

Akizungumzia uwajibikaji bungeni, alishauri uwapo wa uhuru kwa wabunge kuzungumza bungeni. Alisema hata kipindi nchi inaongozwa na chama kimoja, Rais Mstaafu, Julius Nyerere alitamani uwepo uhuru wa kuzungumza.

“Ukinyamaza wale (wananchi) waliokutuma wanakushangaa ulikuja kufanya nini? Kwa hiyo uwepo uhuru wa wabunge kuzungumza lakini uwe responsible (wa kuwajibika), mtu amefanya research (utafiti). Na mazungumzo hayo yanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika nchi,” alisema.

Alisema kitu wanachokosea baadhi ya wabunge ni kuzungumza vitu ambavyo hawana uhakika navyo.

Makinda alisema kufanya utafiti kabla ya kuzungumza kunaifanya Serikali kutoa majibu ya kweli na kwamba mbunge akizungumza ovyo, mawaziri watawajibu ovyo.

“Mimi naamini kuwa Bunge (la 12) litakuwa lenye nguvu zaidi, wabunge watakuwa huru zaidi kwenye comment (kutoa maoni) na kucorrect (kusahihisha) na kukosoa kama Bunge linavyotakiwa,” alisema.

Dk Paul Loisilie wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), alisema Dk Tulia anaingia katika uongozi huku wananchi wengi wakiliona kuwa halina msaada kwao, bali linajali masilahi yao binafsi.

“Hii inatokana na aina ya uongozi uliokuwepo wakati yeye akiwa Naibu Spika ambapo mtangulizi wake alikuwa amebakia kujali masilahi yake na kuwasuta watu waliokuwa wanakemea au kukosoa Bunge,” alisema.

Alisema kazi kubwa aliyonayo ni kurejesha heshima ya Bunge kwa kuwafanya wabunge kuwajibika kwa waliowachagua.

Pia, alisema atakuwa na kazi kubwa ya kuweka usawa wa mizania sawa kati ya Bunge, wananchi na Serikali.

Aidha, alisema suala la wabunge wa viti maalumu walioingia bungeni bado limeendelea kupigiwa kelele na baadhi ya Watanzania.

“Sijui atalitatuaje, lakini bado watu wameendelea kuhoji uhalali wa wao kuendelea kuwa bungeni,” alisema.

Baadhi ya wabunge nao walieleza matarajio yao kwa Dk Tulia kuwa atakwenda kusimamia sheria, kanuni na misingi ili kulifanya Bunge kuwa la uwazi na linalowajibika kwa wananchi.

Miongoni mwao ni Mbunge Viti Maalumu, Esther Matiko na Mbunge wa Kinondoni, Abass Tarimba.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz