Upanga Mashariki, barabara inayoanzia Hospitali ya Regency hadi Shule za Aga Khan, Dar es Salaam, kuna jengo kubwa linaitwa Vijana Tower. Lina urefu wa mita 95.65 na ghorofa 25. Lilianza kazi mwaka 2012.
Ukipita Barabara ya Morogoro, kushoto kama unaelekea Kisutu au kulia macho yako ukiyaelekeza Magomeni, Vijana Tower linaonekana vizuri kabisa. Ni jengo la Umoja wa Vijana CCM (UVCCM).
Vijana Tower ni alama ya Dk Emmanuel John Nchimbi. Mwaka 1998, Nchimbi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti UVCCM. Uongozi wake wa mihula miwili, ulimfanya aone deni la kuacha alama ya kudumu kwenye umoja huo.
Alikaribia kuondoka UVCCM, je, historia ingemkumbuka kwa lipi la maana? Eneo ambalo Vijana Tower imejengwa, lilikuwepo jengo lingine kuu-kuu, ambalo lilitumika kama Makao Makuu ya Taifa ya umoja huo.
Jengo la Umoja wa Vijana CCM, ndivyo liliitwa. Maandishi makubwa mbele lililosanifiwa kwa mkono ulioshika Mwenge. Lilikuwa moja ya alama za Barabara ya Morogoro, Dar es Salaam.
Hivi sasa, UVCCM wana ofisi za kisasa ndani ya Vijana Tower. Jengo hilo linafanya biashara, hivyo kuwa kitega uchumi kizuri kwa jumuiya hiyo ya vijana na mwekezaji. Si hivyo tu, Vijana Tower hivi sasa ni moja ya majengo yanayoipendezesha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam.
Kurasa za Dk Nchimbi Nimetangulia na simulizi ya Vijana Tower kama muhtasari kuhusu wasifu wa Dk Nchimbi, ambaye Januari 15, 2024, alipendekezwa na Kamati Kuu CCM, kisha kuridhiwa na Halmashauri Kuu Taifa (Nec), kuwa Katibu Mkuu CCM.
Dk Nchimbi anachukua nafasi hiyo baada ya Daniel Chongolo kujiuzulu kwa madai ya kuchafuliwa. Wasifu wake kisiasa na kiuongozi ni mpana. Kwa kila anayemfahamu Dk Nchimbi, ataweka matarajio chanya katika nafasi aliyoishika.
Dk Nchimbi anakuwa Katibu Mkuu wa 11 tangu CCM ilipozaliwa Februari 2, 1977, baada ya vyama vya Tanu (Tanganyika African National Union) na ASP (Afro Shiraz Party), kuungana. Kuanzia Pius Msekwa kisha Rashid Kawawa.
Walifuata Horace Kolimba, Lawrence Gama, Philip Mangula, Yusuf Makamba, Wilson Mukama, Abdulrahman Kinana, Bashiru Ally, Chongolo na sasa Nchimbi. Kipindi cha Msekwa, aliitwa Katibu Mtendaji. Cheo cha Katibu Mkuu kilianzia kwa Kawawa.
Nchimbi ni mtoto wa familia ya CCM. Baba yake, John Nchimbi alikuwa ofisa wa polisi, aliyepanda ngazi hadi cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP). Kipindi cha chama kimoja, John Nchimbi alikuwa Mjumbe wa Nec – CCM, akiwakilisha majeshi.
Nchimbi (Emmanuel), ni mwajiriwa wa zamani wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kuanzia mwaka 1998. Ajira ya Nchimbi Nemc ilikoma mwaka 2003, alipoteuliwa na Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda.
Mwaka 2005, Nchimbi aliingia bungeni baada ya kushinda jimbo la Songea Mjini.
Mambo sita moto yaliyojadiliwa kikao cha CCM leo
Baada ya hapo akateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, akahamishwa kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, kisha Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Cheo cha naibu waziri katika wizara hizo tatu tofauti, Nchimbi alikitumikia kuanzia Januari 2006 mpaka Oktoba 2010.
Ilipofika Novemba 2010, Nchimbi aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, kisha Mei 2012, alihamishwa kwenda kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Kashfa kubwa iliyoikumba Serikali kupitia Operesheni Tokomeza Ujangili, majeshi ya nchi yalipopiga, kutesa na kunyanyasa raia, haikumwacha salama Dk Nchimbi. Kama mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, inayoliongoza jeshi la polisi, alilazimika kujiuzulu. Ilikuwa Desemba 2013.
Vyama na taifa Jambo moja ambalo halina kazi kubwa kulithibitisha kuhusu Nchimbi ni kwamba ni mtu wa siasa za ushindani, anajiamini na anaweza kuzungumza fikra zake pasipo hofu. Anajua kutofautisha nyakati za kufanya siasa na kujenga nchi.
Mwaka 2010 mwanzoni, iliibuka kashfa na mgogoro mkubwa kuhusu umiliki wa kampeni ya kupambana na malaria Tanzania, iliyoitwa “Zinduka, Malaria Haikubaliki”. Mwanamuziki wa Hip Hop, Joseph Mbilinyi “Sugu”, alilalamika kudhulumiwa jasho lake.
Kwamba, Sugu alianza mazungumzo na taasisi ya kimarekani ya Malaria No More, wakaunda makubaliano ya kushirikiana kuendesha kampeni ya kupambana na malaria. Kisha, Sugu alifanikiwa kuwaleta nchini Malaria No More.
Kashfa kubwa ilielezwa kuwa baada ya wawakilishi wa Malaria No More kupelekwa Ikulu kutambulishwa, ushawishi ulifanyika uliosababisha taasisi hiyo ya Kimarekani ibadili mawazo ya kushirikiana na Sugu, kisha kampeni ikatekelezwa na familia ya Clouds Media Group (CMG).
Hali hiyo, ilisababisha Sugu aingie kwenye mgogoro mkubwa na CMG, hususan aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Utafiti, marehemu Ruge Mutahaba. Mwaka 2010, Sugu alishinda ubunge jimbo la Mbeya Mjini (Chadema).
Kisha, Sugu alikuwa Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni na Michezo. Nchimbi akiwa ndiye waziri wa wizara hiyo, na kwa vile CMG ni mdau wa wizara kwa kuwa inamiliki vyombo vya habari, alifanikiwa kuwakutanisha na kumaliza mgogoro wa muda mrefu baina ya Sugu na Ruge.
Mifano hiyo miwili itoshe kuonesha kuwa Nchimbi huwa tayari kushirikiana na yeyote, bila kujali itikadi na vyama, mradi jambo lenyewe lina mguso wa kitaifa. Vilevile ni mpatanishi na ana nguvu ya kushawishi maridhiano.
Mwanafunzi wa Kikwete, Lowassa Jambo moja halikwepeki kuzungumzwa kuhusu Nchimbi; ni uhusiano wake na magwiji wawili wa siasa Tanzania, Jakaya Kikwete na Edward Lowassa. Nchimbi alikuwa Mwenyekiti UVCCM nyakati za mtandao mkubwa wa urais, ulioratibiwa na Lowassa, ukampeleka Kikwete Ikulu.
Kipindi ambacho taifa lilinusa harufu ya mgawanyiko, baina ya Lowassa na Kikwete, minong’ono ikawa mingi kuhusu mafahari hao wawili, kila hatua, Dk Nchimbi alibaki kuwa mtu pendwa kwa wote wawili. Lowassa wake, hivyohivyo Kikwete.
Lowassa alipokatwa jina kabla ya kufika Kamati Kuu CCM, kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya kuwa mgombea urais CCM, Uchaguzi Mkuu 2015, Nchimbi alikuwa mmoja wa wajumbe watatu waliojitokeza mbele ya vyombo vya habari na kueleza kutokukubaliana na uamuzi uliofanyika.
Dk Nchimbi, aliongozana na makada wengine waandamizi CCM, Sophia Simba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake CCM (UWT) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa.
Nchimbi alisema kwa niaba ya wenzake: “Tunajitenga na uamuzi wa Kamati Kuu kwa sababu kuna majina yaliondolewa kabla ya kufika kwenye kikao.”
Hakutaja jina la Lowassa, ila alisema kilichofanywa kilikiuka Katiba ya CCM na kanuni za chama hicho, alichagiza kwa kusema, wao kama wajumbe wa Kamati Kuu, hawakukubaliana na uamuzi uliofanywa kwa sababu uliminya wanaokubalika kwa manufaa ya wasiokubalika.
Mwenyekiti wa CCM alikuwa Kikwete. Kikwete aliongoza mkutano wa Kamati Kuu ambao Nchimbi, Sophia na Kimbisa, walitangaza kujitenga na uamuzi wake. Hicho ni kipimo kuwa Nchimbi hana hofu linapokuja suala la kuzungumza fikra zake.
Alifanya hivyo dhidi ya Kikwete. Tafsiri za wengi zimebaki kuwa Nchimbi, Sophia na Kimbisa, walifikia uamuzi huo kwa sababu walimtaka Lowassa. Kauli “kuminya wanaokubalika”, ilimaanisha Lowassa ndiye alikubalika kwa wakati huo.
Naibu Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete ni mtoto wa kwanza wa Kikwete.
Nilipofanya naye mazungumzo kuhusu hekaheka za urais 2015, Ridhiwani alisema: “Mzee alitamani kumwona Emma (Nchimbi) anagombea urais, lakini hakufanya hivyo, akaenda kumpigia debe Lowassa, alikasirika sana.”
Nchimbi na utendaji Kipindi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Nchimbi aliweka rekodi ya kuwanasua mahabusu wengi waliokuwa nyuma ya nondo kwa kesi za kubambikiwa. Alishughulika pia na polisi waliobambikia watu kesi.
Nchimbi, alianzisha utaratibu wa kuzungukia magereza na kuzungumza na wafungwa pamoja na mahabusu. Kwa njia hiyo, alisaidia wengi waliokuwa na kesi za kubambikiwa.