Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mwinyi kumaliza migogoro ya ardhi

3e20f03eb2bf266f53bf976478085ad2 Dk Mwinyi kumaliza migogoro ya ardhi

Tue, 22 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema akichaguliwa atalipatia ufumbuzi tatizo la migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji kwenye sekta ya utalii.

Alisema hayo katika mkutano wa kampeni za uchaguzi Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja. Dk Mwinyi alisema ardhi ni rasilimali ya kunufaisha makundi yote ya wananchi wakiwemo wazawa.

Alisema anafahamu kuna migogoro ya ardhi baina ya wananchi wa Kijiji cha Nungwi na jirani zao wa Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja na wapo wananchi waliopoteza ardhi bila kulipwa fidia.

“Nikichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar nakusudia kulipatia ufumbuzi tatizo la migogoro ya ardhi linalowakabili wananchi wa vijiji vya Nungwi na Matemwe...nataka kuona kwamba wananchi wanafaidika na ardhi ambayo ndiyo rasilimali kubwa na hazina kwa vizazi vijavyo”alisema Dk Mwinyi.

Alisema akiwa Rais anakusudia kuhakikisha sera ya uwekezaji inaweka bayana misingi bora, kuhakikisha wananchi wazawa wananufaika na uwekezaji.

Mapema Dk Mwinyi alisema anakusudia kulipatia ufumbuzi tatizo la maji safi na salama katika Kijiji cha Nungwi na majirani zake. Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imejitahidi kusambaza huduma hiyo kwa asilimia 72 kwenye maeneo ya vijijini na kubaki asilimia 28 tu.

Alisema huduma za maji safi na salama ni muhimu kwa Kijiji cha Nungwi na majirani zake kwa ajili ya kuimarisha sekta ya utalii, ambayo imepata mafanikio makubwa kwa kuwepo kwa idadi kubwa ya hoteli.

Mapema akimtambulisha Dk Mwinyi kwa wananchi wa Kijiji cha Nungwi na maeneo ya jirani, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema mgombea huyo ni sahihi na chaguo la CCM, kwa kuwa anaweza kuzitatua changamoto za wananchi Zanzibar.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar wasifanye majaribio ya uongozi, kwa kuchagua watu ambao hawana sifa na uzoefu wa kuongoza na wenye malengo binafsi.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Iddi Ame aliwataka wananchi wa mkoa huo wasifanye makosa na kujaribu kuchagua wagombea wa vyama vya upinzani, kwani hawawezi kuwasaidia wananchi kupata maendeleo.

Alisema yapo majimbo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, yamechagua wabunge na wawakilishi kutoka upinzani na baadaye walijuta, kwa sababu waliochaguliwa wamekuwa wakijinufaisha, badala ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Kijiji cha Nungwi ni miongoni mwa maeneo yenye ufukwe mrefu. Kijiji hicho kina zaidi ya hoteli 150 zikiwemo zinazomilikiwa na wananchi wazalendo na wageni.

Chanzo: habarileo.co.tz