Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mwinyi awapa neno mabalozi nyumba kumi

Ba65138168a4c844ab708439ad068e93 Dk Mwinyi awapa neno mabalozi nyumba kumi

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Ali Mwinyi amewaagiza mabalozi wa nyumba kumi wa chama hicho katika kisiwa cha Pemba kuhakikisha siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka huu, wanasimamia wananchi wao na kuhakikisha hakuna mwanachama atakayeshindwa kupigakura.

Dk Mwinyi alisema hayo katika Shule ya Sekondari ya Fidel Castro wakati akizungumza na viongozi hao katika ziara ya kampeni kisiwani Pemba.

Alisema tathmini inaonesha kwamba licha ya CCM kuwa na idadi kubwa ya wanachama wengi na wafuasi wake lakini baadhi yao hawajitokezi kwenye vituo vya kupigakura.

“Nawaomba wanachama wa CCM pamoja na wafuasi, wajitokeze kwa wingi kupigakura katika siku ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, tuache mawazo kwamba Chama Cha Mapinduzi kitashinda tu katika uchaguzi mkuu,”alisema.

Alisema miongoni mwa viongozi wanaotegemewa sana ndani ya CCM ni kufuatilia mwenendo wa uchaguzi pamoja na wanachama na wafuasi wa CCM, ni mabalozi wa nyumba kumi.

Aidha aliwataka viongozi wa majimbo kuhakikisha wanaweka mawakala wa vyama wenye uwezo na sifa ambao wapo tayari kufanya kazi kwa maslahi ya chama na sio kukubali kurubuniwa na wapinzani.

“Viongozi wa majimbo hakikisheni mnaweka mawakala wenye sifa na uwezo mkubwa wa kusimamia masuala ya uchaguzi ili kuepuka mbinu zinazoweza kutumiwa na wapinzani wetu,”alisema.

Jumla ya mabalozi 471 walihudhuria mkutano huo ambapo walisema wapo tayari kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 na kuhamasisha wanachama kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

‘’Sisi mabalozi wa nyumba kumi tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba uchaguzi mkuu wanachama wetu na wafuasi wote wenye sifa za kupiga kura wanashiriki,” alisema Hamadi Issa ambaye ni balozi wa nyumba kumi shehia ya Mchanga mdogo.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdalla Juma Sadalla aliwaondoa hofu wanachama wa CCM katika kisiwa cha Pemba na kuwaambia wasitishwe na wapinzani kwani huu ni mwaka ambapo watasambaratishwa vibaya.

‘’Wanachama wa CCM pamoja na mabalozi tembeeni kifua mbele msitishwe na wapinzani, huu ni mwaka ambao tutawasambaratisha vibaya,’’ alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz