Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mwinyi ahimiza siasa za kistaarabu

D7033d0971b41635e7ba7a4508dd75cd Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Thu, 21 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesisitiza umuhimu wa siasa za kistaarabu kwa kuweka mbele maslahi ya taifa na kudumisha amani.

Dk Mwinyi alisema hayo jana Ikulu, Zanzibar wakati akizungumza na kikosi kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kikiongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala.

Alisema amani ni jambo muhimu kwenye taifa lolote na hilo linawezekana kwa kuwa na siasa za kistaarabu.

Dk Mwinyi alimpongeza Rais Samia kwa kuunda kikosi hicho ili kikusanye maoni na baadae kitoe mapendekezo kwa serikali zote mbili.

Dk Mwinyi aliviomba vyama vya siasa ambavyo havijaamua kuwa sehemu ya jambo hilo vijiunge kwa sababu inatakiwa Watanzania wote wawe sehemu ya suala hilo.

Alisema kutokana na migogoro inayojitokeza kila ikifika wakati wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar, ni vyema wadau wakubwa wa kikosi hicho wakawa Wazanzibari wenyewe na vyama vya siasa visiwani humo.

“Si vyema kuona yaliyojitokeza siku za nyuma yanajirudia kwani wakati huu ni mwafaka kueleza changamoto zilizopo na kuzifanyia kazi ili ifikapo mwaka 2025 mambo yote yawe yamewekwa vizuri,” alisema.

Rais huyo wa Zanzibar alisema amani iliyopo haiwezi kudumu kama bado kuna baadhi ya changamoto zisizofanyiwa kazi na akaeleza umuhimu wa ushiriki kwa vyama vyote vya siasa ili mambo yakae sawa.

Profesa Mukandala alimpongeza Dk Mwinyi kwa juhudi anazozifanya kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa Zanzibar, pia alimshukuru kwa hotuba zake kwani wanatumia kama dira ya kazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live