Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mwinyi: Tukitonesha vidonda havitapona

Mwinyi Pic Nnnn Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Thu, 6 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametaja mambo makuu manne yatakayoleta maelewano ya kitaifa, ikiwamo kuondoa mifarakano na kulaumiana.

Pia amewasisitiza wanasiasa nchini kutoruhusu tofauti zao kuwa chanzo cha kufarakana na kuhasimiana baina ya wananchi.

Rais Mwinyi aliyasema hayo jana, wakati akifungua mkutano wa wadau wa demokrasia wa kujadili masuala mahususi ya Zanzibar, ikiwamo demokrasi ya vyama vingi kwenye ukumbi wa Golden Tulip, mjini Unguja.

Alisema hakuwezi kuwa na maelewano kama jamii ya Wazanzibari ikiwa na mifarakano na kutafuta visingizio vya kulaumiana.

“Maelewano ya kijamii hayawezi kudumu iwapo kila siku mtakuwa mnakumbushana au kutishana kwa mambo yaliyopita, kiini cha maelewano na maridhiano ni ujasiri na kuacha kutonesha vidonda, maana tukifanya hivyo kila mara kamwe haviwezi kupona na maelewano ya kweli huanza na methali inayosema ‘yaliyopita si ndwele, tugange yajayo,” alisema.

Dk Mwinyi alitaja jambo lingine ni kukubaliana juu ya mgawanyo wa majukumu ndani ya maelewano na maridhiano hayo, vigezo vya utekelezaji wa majukumu hayo na namna bora ya kusuluhisha matatizo yanayojitokeza bila kuvunja maridhiano.

Alisema mambo hayo manne ni muhimu katika kudumisha maridhiano ya jamii, maana yatatoa uelewa wa pamoja wa jinsi ya kuendesha shughuli za kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Alisema: “Wanasiasa wanatakiwa kukumbuka kuwa watu wao ni kama watu wengine duniani, ambao wanaweza kubadilika kwa mujibu wa mazingira yalivyo, hivyo wasiwafanye wakabadilika kwa mivutano isiyokuwa ya lazima. “Tukidumisha utulivu na ustahamilivu tutaondoa shaka ya kutoaminiana baina yetu na tukiimarisha dhamira ya maridhiano na maelewano ya kijamii, tutaona mema zaidi kuliko mabaya.

“Tofauti zetu za itikadi za kisiasa zisiruhusiwe kudhoofisha udugu, umoja na mshikamano wetu, ndiyo maana tunapotofautiana kisiasa huwa tunakaa na kuzungumza kwa lengo la kuziondoa ili tubakie wamoja, ” alisema.

Aliwata washiriki wa mkutano huo kuhakikisha kuwa michango watakayoitoa inazingatia maslahi ya Taifa na siyo binafsi, wadhifa au taasisi.

Kwa upande wa Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Fransis Mutungi alisema ni jambo la kihistoria mkutano huo kuhudhuriwa na vyama vyote vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib alisema hatua ya kuwa na mkutano huo unaohusisha vyama vyote vya siasa ni kubwa katika utawala bora.

Akizungumza katika mkutano huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo, Ismail Jussa alisema ipo haja ya kusimama na kujenga mifumo, misingi ya kweli na haki na kuwapo chombo cha kudumu cha kusimamia maridhiano tofauti na ilivyo sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live