Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mahanga achambua kushindwa kwa Sumaye

86710 Pic+mahanga Dk Mahanga achambua kushindwa kwa Sumaye

Mon, 2 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni mawazo yangu kwamba Mhe. Frederick Sumaye na wapiga kura wa Baraza la Uongozi la Kanda ya Pwani wote wanaweza kuwa na sehemu yao ya lawama katika sakata la Sumaye kunyimwa kura za kuwa Mwenyekiti wa Kanda hiyo.

Kwa wapiga kura sehemu yao ya lawama inaweza kuonekana kwamba iko wazi zaidi wakati kwa upande wa Sumaye mtu anaweza kuona hastahili lawama, lakini kumbe anastahili lawama ambazo lazima uziangalie kwa jicho la tatu la kisiasa kuweza kuzitambua vizuri. Nitafafanua

Kwa wapiga kura lawama zinaonekana ziko wazi kwa sababu wamemwadhibu Sumaye kwenye sanduku la kura kwa sababu tu ya nia yake ya kutaka kutekeleza haki yake ya kikatiba na demokrasia ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chadema Taifa. Ni vigumu kuona ni sababu gani nzuri zilizowafanya wapiga kura walio wengi wa Kanda ya Pwani kumkataa Sumaye kwenye nafasi ya Uenyekiti wa Kanda ya Pwani kwa kumpigia kura nyingi za HAPANA, tena baada ya kumwachia agombee nafasi hiyo peke yake bila mpinzani. Shida imetoka wapi ghafla? Ni rahisi kusema hakukuwa na sababu nzuri bali ni ile tu azma yake ya kugombea pia nafasi ya Uenyekiti Taifa ndiyo iliyomponza. Kama kugombea nafasi hiyo ya Uenyekiti wa Taifa ni haki ya kidemokrasia ya mwanachama yeyote, kwanini wapiga kura wa Kanda ya Pwani wakaamua kumwadhibu Sumaye kwa hili?

Nataka nieleze mazingira ambayo watu wanatakiwa wayaone kwa jicho la tatu la kisiasa kabla ya kuwapa lawama zote wapiga kura wa Kanda ya Pwani waliompigia kura za HAPANA Sumaye. Ni imani yangu pia kwamba Sumaye naye hakuangalia mazingira haya kwa umakini wa kisiasa hasa kwa mwanasiasa mkubwa na mkongwe kama yeye. Mazingira haya ni ya muda mrefu sasa ingawa mengine yamejitokeza kuelekea uchaguzi wa Kanda na siku yenyewe ya uchaguzi wa Kanda ya Pwani ambayo hayakuwa rafiki kwa upande wa Sumaye na yeye hakuyang’amua kabla kwa jicho kali la kisiasa. Baadhi ya mazingira haya toka kabla ya uchaguzi huu na mpaka wajumbe kupiga kura Kanda ya Pwani ni kama yafuatayo:

1. Ukifuatilia mjadala na mchakato wa Uchaguzi wa Chadema ngazi ya Taifa mwaka huu, hata kabla haujatangazwa rasmi, kumekuwepo na hisia kali sana miongoni mwa wanachama wa Chadema, wanachama wa vyama vingine, wananchi wa kawaida na hata ndani ya vyombo vya Serikali vikiwemo vya usalama kuhusu kwa nini Mbowe

bado anafaa au hafai kuendelea kuwa mwenyekiti wa Chadema. Mijadala hii imefanyika kwa hisia kali kwenye mitandao ya kijamii na kwenye mijadala rasmi na isiyo rasmi.

Kwa nini mjadala wa kufaa au kutofaa kwa Mbowe umechukua hisia kali sana, tena hadi nje ya chama? Kwa asilimia kubwa ya wanachama, inaonekana kwamba wale wanaotaka Mbowe ang’olewe, hasa kutoka nje ya Chadema na kutoka serikalini, hawafanyi hivyo kwa sababu ya kutetea demokrasia bali wana nia ovu, siyo ya kuokoa chama bali ya kuangamiza chama.

Kwa nini? Kwa sababu kwa wana Chadema walio wengi wanaamini kwamba, angalau katika kipindi cha miaka mitano ijayo hakuna mwana Chadema aliye tayari na anayeweza kuiongoza Chadema vizuri kuliko Mbowe.

Sababu zao ziko wazi: Mbowe ameongoza Chadema kwa ufanisi katika mazingira magumu sana ya kisiasa kwa chama na kwake mwenyewe. Na kwa mazingira ya siasa nchini chini ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano, ni Mbowe tu kwa sasa anayeweza kuiongoza Chadema vizuri kuvuka wimbi hili.

Ni mtazamo wa wana Chadema hawa walio wengi kwamba kwa kutambua ukweli huu wabaya wa Chadema ndani na nje ya Chama, wangependa Mbowe aondoke leo na siyo mwaka 2024 ili Chama kiharibikiwe.

Swali la kujiuliza: Sumaye amekuwa kundi gani? Kundi la kuona umuhimu wa Mbowe kuendelea kuwa Mwenyekiti ili Chama kiendelee kuwa imara licha ya vitimbwi vingi kutoka Serikali ya CCM, au yuko kundi la wanaotaka Mbowe ang’oke hata kama hawana uhakika nani mwingine kipindi hiki anaweza kuibeba Chadema kama alivyofanya Mbowe? Hili ni swali la kwanza ambalo wapiga kura wa Kanda ya Pwani walijiuliza.

2. Mazingira ya pili ya kuangalia katika suala la Sumaye, na ambalo linatokana na yaliyojadiliwa hapo juu, ni kwamba kumekuwepo na hisia na maswali miongoni mwa wanachama wengi kwamba wanaojitokeza kutaka kugombea nafasi ya uenyekiti wa Chadema ni kweli wanasukumwa na takwa la haki yao ya kikatiba na kidemokrasia tu au wanasukumwa na nguvu kutoka ndani na nje ya Chadema isiyompenda Mbowe na inayotaka tu aondolewe kwa maslahi ya wasioitakia mema Chadema na hasa Serikali ya CCM? Wengi wanahisi kuna ukweli wa hili la mwisho.

Huenda hisia zao haziko sahihi sana, lakini je, Sumaye katika kutaka kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chadema Taifa amejiuliza haya na anajiona yuko kundi gani? Au ameangalia tu demokrasia? Kwa mzoefu kama yeye ameshindwa kweli kusoma hisia hizi?

3. Kwa miezi ya hivi karibuni kumekuwepo na viongozi wa Chadema ambao wameonekana kumpinga waziwazi Mbowe kwa kujaribu kuunda mbinu za kumng’oa na wengine kama wabunge (Saed) Kubenea na (Anthony) Komu wamefikia hatua ya kuitwa mbele ya Kamati Kuu na kuonywa kwa matendo yao ukosefu wa kimaadili.

Pamoja nao kuna mtandao fulani ndani ya chama nchi nzima wa wanaompinga Mbowe wakiongozwa na baadhi ya watendaji wakuu wa chama hicho.

Ingawa viongozi hawa ama watakanusha hili ama watasema ni haki yao ya kikatiba, na huenda ndivyo ilivyo, lakini kwa jicho la wana Chadema walio wengi ni kwamba viongozi hawa wanatumiwa kwa nia ovu ya kuhujumu chama, ama wakijua au bila wao kujua.

Sumaye pia katika siku za karibuni amesikika na kuthibitika kuwa na mawasiliano au ukaribu na watu hawa ambao wanahisiwa kuwa “wasaliti” wa Chama. Je, Sumaye aliliona hili na kulitafakari kabla ya uamuzi wake wa kuchukua fomu ya kugombea ngazi ya Taifa? Na kwa hisia zilezile za awali, wapiga kura wa Kanda ya Pwani wanawezaje kulaumiwa kwa hatua yao ya kumtosa Sumaye?

4. Hili la Demokrasia. Wanasiasa tunapenda kujificha kwenye neno demokrasia kisiasa tu hasa linapokuja suala la kugombea uongozi. Utasikia mtu anasema “nataka kupambana na Mahanga kwenye nafasi yake kwa sababu ni demokrasia yangu”.

Lakini, ukweli ni kwamba mtu huyo ameona mapungufu ya Mahanga ya kiuongozi na kwamba Mahanga hafai na nia yake ni kutaka amng’oe ili yeye afanye mazuri zaidi. Wakati wa kujibu swali moja la mjumbe wa Kanda ya Pwani kwenye uchaguzi huo, Sumaye alijibu kwamba ana hakika ya asilimia zote kwamba hata akisimama na Mbowe, yeye Sumaye atashindwa kwa mbali sana!

Maana yake ni kwamba hagombei ili amtoe Mbowe na kuleta mabadiliko ndani ya Chadema bali anagombea kwa ajili ya kutimiza tu haki yake ya kidemokrasia lakini bado Mbowe atashinda na kuwa mwenyekiti! Hii ni hadaa ileile ya wanasiasa wanapotaka kumng’oa mtu kwenye nafasi yake.

Hivi kweli mtu kama Mzee Sumaye, waziri mkuu kwa miaka 10 anaweza kwenda kwenye uchaguzi wa “kushindwa vibaya” na Mbowe huku yeye akijua matokeo hayo kabla, ati kutimiza tu takwa la demokrasia?

Bila shaka Sumaye anaona mapungufu ya Mbowe na kwamba yeye anaweza kuwa mbadala mzuri zaidi. Sasa kama ni hivyo kwa nini aseme ana hakika Mbowe atamshinda kwa mbali?

Je, ni kwa ajili ya kuwahadaa wapiga kura wa Kanda ya Pwani ili wamchague kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kanda? Ilivyotokea ni kwamba wapiga kura hawakutaka kukubaliana na hadaa hiyo.

Wakasema ni heri angesema tu kwamba kwa mtazamo wake kuna mapungufu anayoyaona kwenye uongozi wa juu wa Chadema, ndio maana anataka kupambana na Mbowe ili akishinda ayarekebishe.

Ukizingatia nafasi na wadhifa mkubwa wa sasa na wa huko nyuma wa Sumaye, hakutakiwa kujificha nyuma ya demokrasia tu. Sasa ukizingatia imani na hisia za Chadema kutaka kuhujumiwa kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa, Sumaye na watu wengine wanawalaumuje wapiga kura wa Kanda ya Pwani kwa maamuzi yao?

Nihitimishe kwa kusema kwamba wakati watu kadhaa wakiwalaumu wapiga kura wa Kanda ya Pwani kwa “kumwadhibu” Sumaye aliyetaka kutekeleza demokrasia yake, wanatakiwa wajiulize, Je, Sumaye kwa uzoefu na wadhifa wake, hivi hatakiwi kulaumiwa kwa kushindwa kusoma mazingira ya kisiasa na alama za nyakati ndani ya Chadema na ndani ya nchi kwa sasa, hata kama anaipenda sana Chadema na hakuwa na nia mbaya katika kuchukua fomu ya Taifa?

Mimi ni mmoja wa watu wanaoamini kwamba Sumaye ana dhamira ya kweli na ya dhati kabisa ya kupambania mabadiliko, haki na usawa wa kisiasa nchini Tanzania unaobinywa na Serikali ya CCM, na anatamani sana CCM iondolewe madarakani mwaka 2020, lakini katika hili la sasa alishindwa kusoma kabisa alama za nyakati na mazingira ya sasa ya kisiasa...... Anatakiwa ajilaumu mwenyewe kwa kilichotokea Kibaha.

Chanzo: mwananchi.co.tz