Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Kahangwa akumbuka ujio wa Lowassa ulivyoitawanya Ukawa

48876 Pic+kahangwa

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mwaka 2015 ulileta mtafaruku mkubwa hasa baada ya Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani kutua Chadema.

Siku chache baada ya Lowassa kujitoa Chadema na kurudi CCM, aliyekuwa mjumbe wa Ukawa kupitia NCCR Mageuzi, Dk George Kahangwa amezungumza na Mwananchi na kueleza kwa undani hali ilivyokuwa. Endelea

Swali: Umekuwa kada wa NCCR Mageuzi na mwaka 2015 ulipendekezwa kugombea urais. Nini kilitokea katika mchakato huo?

Jibu: Ni kweli kwamba nilikuwa katika siasa. Nilijiunga na NCCR mwaka 1995 mpaka mwaka jana nikaondoka kwenye hicho chama na nilipoondoka sijajiunga na chama chochote, labda wazo litakaponijia tena.

Mwaka 2015 tulikuwa kwenye Ukawa, NCCR Mageuwzi, Chadema, NLD na CUF. Vyama hivi vilikubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa urais.

Kwa hiyo katika majadiliano kila chama kilitakiwa kihalalishe wagombea wake, halafu mwisho tukubaliane tumsimamishe nani.

Wakati ule, vijana wa NCCR walinipendekeza nigombee. Tulipokuwa kwenye meza za mazungumzo kuhusu suala la mgombea, yalitokea mengi, mwisho wake akatokea Edward Lowassa.

Swali: Wakati mko kwenye mchakato, Profesa Lipumba ni kama hakufurahishwa na mchakato ule akaondoka. Ilikuwaje?

Jibu: Mambo ya siasa yana siri nyingi. Kwa hiyo yapo mengi ninaweza kusema Profesa Lipumba anayajua mwenyewe undani wa kilichosababisha uamuzi wake. Tofauti na kile alichoweka mezani na kutuambia.

Tulikuwa na mabishano ya muda mrefu kwamba nani awe mgombea, mpaka mimi nilipopeleka pendekezo kwamba kwa kuwa mjadala huu umeshindikana na hatutapiga kura, tuachieni sisi tunaotajwa ili tufanye makubaliano.

Hilo lilifanyika, tukakaa nyumbani kwa Profesa Lipumba, tukakubaliana kwamba atakayegombea kwa tiketi ya Ukawa awe Dk Willibrod Slaa.

Swali: Profesa Lipumba alikubali?

Jibu: Alikubali.

Swali: Kwa hiyo baada ya kukubali iliwaje tena hakutokea siku ya kutangaza?

Jibu: Ni kweli. Pamoja na kukubali huko kulikuja kuleta picha ya ajabu, maana baada ya hapo tulikubaliana kwamba siku mbili baadaye tutafanya mkutano waandishi wa habari tuwaambie tulichokubaliana.

Na hiyo ni siku ambayo ilileta shida kidogo kwamba sababu Profesa Lipumba hakuonekana, bila shaka alishanusa nini kinachoendelea.

Unajua mnaweza kukaa wagombea watatu ili kupitishana kwamba wewe ni mgombea kuna mambo mnakubaliana. Kwamba unapogombea wewe, kama Waswahili wasemavyo, unaniachaje? Sasa hayo makubaliano yalikuwapo ambayo siwezi kusema kwa sasa, kwamba wewe unasimama sasa tutaishije pamoja katika serikali yako?

Sasa anapokuja mtu mwingine ambaye kupatikana kwake si kwa maridhiano ya namna hiyo, kwa vyovyote vile unaweza kusema ngoja aje labda kutakuwa na makubaliano.

Swali: Wewe binafsi ulijisikiaje alipokuja Lowassa?

Jibu: Nilipata shida kidogo kwa sababu tulishakuwa tumefanya maamuzi ya Ukawa, halafu Chadema ndiyo wanakuja na mgombea wao mwingine. Kwa nguvu ya Chadema ikaonyesha kuwa ndiye mgombea wa Ukawa.

Kwangu mimi nilikuwa na amani kwa sababu kama ni ‘future’ bado ninayo. Pengine najua kwamba hiki chamba ambacho tulisema Dk Slaa atoke agombee, ndicho kimepindua maamuzi, basi hata hukasiriki sana.

Lakini shida ni kwamba kaja mtu wa wanne wakati kulikuwa na watatu wanazungumza, basi naye angejiunga na mazungumzo. Hicho hakikutokea.

Unapata shida kwamba mifumo ya Chadema ilifuatwa au haikufuatwa? Lakini mtu ambaye amekuja Chadema amekuwa na nguvu kubwa kiasi cha kuvunja taratibu zilizopo, kitu kilileta shida kwenye demokrasia.

Lakini unaona Dk Slaa ambaye ilikuwa awe mgombea alikuwa wa kwanza kuudhiwa na hayo mambo. Profesa Lipumba akajitoa akaenda safari zake Rwanda. Mimi sikukimbia, kwa sababu kwanza sikuteuliwa kuwa mgombea.

Pili kukaa Ukawa kungeweza kukufungulia milango kwa sababu safari bado ilikuwa inaendelea.

Swali: Kwa hiyo kutoteuliwa kwako pengine ndiyo kulikukatisha tamaa hata ukajitoa NCCR-Mageuzi?

Jibu: Wala siyo sababu hiyo. Kwa sababu kama unagombea siyo kwamba fursa ikikosekana mwaka huu, Mungu akikujalia uhai unaweza kupata nafasi katika miaka inayokuja.

Swali: Kwa hiyo nini kilikuondoa NCCR-Mageuzi?

Jibu: Nilisema na niliandika hata kwenye Facebook, mwelekeo wa NCCR niliona hauna matumaini. Kwa hiyo ninaona haina sababu ya kupoteza muda wakati uwezekano wa kufanikiwa ni 0.000.

Swali: Baada ya kuondoka na NCCR-Mageuzi una mpango wa kujiunga na chama kingine?

Jibu: Baada ya hapo tumeanzisha chama kingine cha maendeleo, siyo cha siasa. Kinaitwa Partnership for Development of Tanzania (Pandep). Kiko wazi kwa mtu yoyote anayetaka kujiunga, tunachangia ada kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Swali: Ulipokuwa NCCR-Mageuzi na hadi kufikia mchakato wa kugombea urais, hujawahi kusumbuliwa na mwajiri wako?

Jibu: Sikuwahi kusumbuliwa, isipokuwa jina langu lilipotajwa kama mgombea, mwajiri aliniandikia barua akitaka nijieleze na maelezo yangu yalikuwa wazi kwamba, sikugombea isipokuwa jina langu limetajwa.

Kwa sababu ili ugombee lazima uende kikatiba kwenye chama upitishwe. Sasa kwa kuwa huo mchakato wa kikatiba haukuwepo, sikugombea.

Hata kama mtu anagombea, hata kama yupo chama tawala, anatakiwa kumjulisha mwajiri wake kwamba nakwenda kwenye hatua za awali za chama kupata wagombea.

Swali: umekaa NCCR-Mageuzi kwa muda mrefu, kwa nini vyama vya upinzani vinaibuka na kushuka?

Jibu: Siasa za vyama vingi ni za ushindani, kwa maana vyama vyote vinashindana. Hata ukiona vyama vinashirikiana siyo kwamba ushindani umeisha, kila mmoja angetaka amshinde mwenzake.

Tuko kwenye nchi ambayo kuna chama kikubwa kilichoshikana na dola, kana kwamba ni dola yenyewe. Kwa hiyo kina nguvu ya kuvishinda vyama vingine katika chaguzi na katika nguvu ya kawaida ya siku kwa siku,.

Miongoni mwa vitu vinavyoathiri vyama vingine ni nguvu kubwa iliyonayo CCM – nguvu ya kiuchumi na uwezo wa kumpa mtu tuzo. Hata katika nadharia za uongozi wanakwambia, kiongozi awe na nguvu na vyanzo vyake ni pamoja na kutoa kitu ili mtu awe upande wako.

Sasa ukiangalia CCM kwa muda mrefu inashinda viti vingi vya ubunge, kwa hiyo ina nafasi nyingi kwa mfano za viti maalumu, kwa hiyo inaweza kutoa kwa wale wanaohitaji viti maalumu.

Kwa hiyo chama kinachounda Serikali kwa muda mrefu kinapata nafasi wakurugenzi hawa na unaona wengine ni makada, makatibu wakuu, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na wengineo.

Sasa katika wale watu muhimu na maofisa katika dola, unakuta kwa mfano mkuu wa mkoa ni mwenyekiti wa usalama wa mkoa, katika vikao vyao wanaohudhuria viongozi wa jeshi, kwa hiyo ina nguvu ambayo vyama vingine havina.

Ni sawa na kumwambia mwanariadha Hussein Bolt ashindane na mtu ambaye hana hata viatu vya mazoezi. Kama kushindanisha nguvu za uchumi wa Marekani na nchi masikini. Kwa hiyo huu ushindani si sawa.

Bahati mbaya unakuta mwenyekiti wa chama ndiye Rais ndiye anateua mkuu wa tume na mkurugenzi ambaye atakuja kusimamia uchaguzi kwenye wilaya na diwani.

Kwa hiyo refa ndiye mchezaji wa kundi fulani, ndiyo maana watu wakapiga kelele mabadiliko ya Katiba, kwamba chama tawala kitengwe na dola kisiwe na nguvu iliyopitiliza.

Ni watu wachache tu watabaki kwenye chama kidogo, lakini njaa ikiuma atachomoka na kwenda CCM ambako kule njaa haipo. Vyama vingine vinakuwa dhaifu kwa sababu vinakosa rasilimali fedha na watu. CCM haina shida ya rasilimali watu wala fedha.

Shida nyingine ni kwa vyama vyenyewe, kwamba vinaongozwa na watu ambao wanaendekeza masilahi binafsi, badala ya kuangalia masilahi ya nchi. mtu yuko kwenye chama siyo kwa ajili ya itikadi ya chama, bali apate nini?



Chanzo: mwananchi.co.tz