Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Bashiru kumbana waziri anayemiliki ekari 1,000

14792 Pic+bashiru TanzaniaWeb

Fri, 31 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema atamwita waziri mmoja anayemiliki eka 1,000 za ardhi mkoani Morogoro ili aeleze amezipata vipi.

Akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Wanawake la CCM, (UWT) jijini hapa jana, Dk Bashiru alisema Sekta ya ardhi imekuwa na migogoro mingi kutokana na udhaifu katika mipango na usimamizi.

“Lakini hivi karibuni imezuka tabia miongoni mwetu, wengine ni viongozi wetu kuhodhi ardhi au kuwageuza Watanzania kuwa vibarua kwa kuwakodisha,” alisema Dk Bashiru ambaye amejiwekewa utaratibu wa kuwalima barua viongozi wa Serikali na CCM kuhusu masuala mbalimbali.

Hivi karibuni katibu mkuu huyo alisema amekwishamwandikia barua tatu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihoji kuhusu masuala mbalimbali ya kiutendaji na kuwa hatasita kuwalima barua mawaziri kuhusu utendaji wao.

Katibu huyo mkuu alieleza kusikitishwa na mambo yanayoendelea, akisema yanayoonekana katika vyombo vya habari kuwa Serikali inachukua hatua kutatua migogoro ya ardhi, hayafanani na uhalisia katika maisha ya wananchi. “Viongozi na mawaziri katika sekta hii acheni kufanya kazi na vyombo vya habari, nendeni kufanya kazi katika maeneo ambayo migogoro ipo,” alisema.

Dk Bashiru ambaye aliongoza kamati iliyoundwa na mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kuchunguza mali za chama hicho, aliwataka wanachama kuwaumbua viongozi wanaosema wanafanya kazi vizuri katika migogoro, lakini kwenye maeneo husika hali ni mbaya.

“Nilikuwa Morogoro, akatajwa waziri mmoja ana eka 1,000 (za ardhi), watu wanasema wanataka kujua amezipataje na mimi nitamwita nimuulize amezipataje kusudi nikawajibu wale walioniuliza. Hatuwezi kuwa na chama kinachojitambulisha ni cha wanyonge halafu tunapora ardhi ya watu,” alisema Dk Bashiru bila kumtaja waziri huyo.

“Ni suala la kuchagua kati ya kuwa kiongozi wa CCM au kuwa mporaji wa ardhi ya watu. Kazi yenu ni kuwataja na kulinda haki ya ardhi, hasa ile ya wazalishaji wadogo.”

Urais wa Zanzibar

Katika hatua nyingine, Dk Bashiru aliwataka wanawake hao kuelekeza majeshi yao kwa watu ambao wameanza kujenga makundi ya kuwania urais wa Zanzibar.

Alisema kwa bahati mbaya wanaCCM wanaoshiriki kampeni kabla ya muda baadhi yao ni mawaziri na akatumia fursa hiyo kuwahoji ni nani aliyesema Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein amemaliza muda wake wa uongozi. “Mawaziri wanatumia muda wa Serikali, ofisi za Serikali, magari ya Serikali, simu za Serikali na posho za Serikali. Hatutaki viongozi wa chama kutumia muda wao kuendesha makundi ya kusaka uongozi. Mkiwakatalia hawatafika mbali, waelezeni ukweli,” alisema.

Alisema kitendo cha kuingia katika makundi ya kutafuta uongozi kinawapotezea sifa wanachama wa CCM wanaofanya hivyo.

“Mkiingia katika kompyuta yangu kuna jina la kila mmoja alichosema, wakati ukifika tuta-print (kuchapisha) na kuwapa wajione na wakijiona hawatathubutu hata kuchukua fomu,” alisema.

Aliongeza kuwa Mtanzania yeyote anaweza kuwa Rais.

“Lakini unakuta mtu anajipamba, anajipaka wanja, kisa urais. Mtu anayefaa kuwa Rais hajipitishi kuombaomba. Mtu bora anayefaa kuwa rais anaombwa.”

Aidha, Dk Bashiru alisema kuna tatizo la uhusiano kwa baadhi ya watendaji au mawaziri hawaelewani na manaibu wao ingawa wote ni wateule wa Rais.

“Wakati mwingine kiongozi wa kuchaguliwa haelewani na watendaji, viongozi wa chama hawaelewani na wa Serikali. Unakuta DC ana mgombea wake, mwenyekiti wa halmashauri ana mgombea wake, katibu wa chama ana mgombea wake, hivyo hakuna shughuli inayofanyika bali kusaka vyeo,” alisema.

Katibu mkuu huyo alisema amewaambia wabunge watulie yeye atawalinda kwa sababu muda wa kujipitisha pitisha kuomba uongozi bado haujafika.

Chanzo: mwananchi.co.tz