Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Bashiru awashangaa wanaougua urais CCM

55746 BASHIRU+PIC

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ameshangazwa na baadhi ya wana-CCM walioanza kuugua ugonjwa wa kusaka urais na kuibua makundi ndani ya chama, akisema wanawajua na wameanza kuwafuatilia.

Dk Bashiru alionyesha kushangazwa kwake na watu hao wakati akijibu swali kutoka kwa mwanahabari aliyetaka kujua kuhusu hali ya uchaguzi na jinsi ya kuwapata wagombea kupitia kura za maoni ndani ya CCM katika mkutano na wahariri, wamiliki na waandishi wa habari juzi jijini hapa.

Alisema kuna watu wameanza kupanga safu za urais wa 2020 na 2025 hata kabla ya wakati, huku akisisitiza kuwa hawatakuwa na nafasi katika uongozi.

“Mpasuko wa kisiasa Zanzibar sasa umeibua kugombea urais wa Unguja Kaskazini, Unguja Kusini, urais wa Pemba, Zanzibara na Unguja mjini, mambo mabaya kabisa hayo,” alisema.

Alisema wanaofanya kampeni za mapema wametangaza vita kwake na wanatakiwa kujiandaa kwa vita hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa mtendaji huyo mkuu wa CCM kuwaonya wanachama wanaovizia kumridhi Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ambaye anatarajia kumaliza mihula miwili ya urais mwakani.

Mara ya kwanza, Agosti 18, Dk Bashiru akiwa katika ziara ya kujitambulisha visiwani Zanzibar, alizungumzia mbio hizo za urais kwa kuwaonya walioanza kampeni kabla ya wakati.

Akizungumza na wanachama wa chama hicho katika viwanja vya ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja, aliwataka kuzingatia kanuni na katiba ya chama chao.

Septemba 29, mwaka jana, kikao cha Kamati Kuu Maalumu ya Halmashauri Kuu Taifa ya CCM kilichoketi chini ya uenyekiti wa Rais John Magufuli kilitoa onyo kwa wanachama wanaodaiwa kufanya kampeni za chini kwa chini wakiwania kumrithi Dk Shein.

Katika mazungumzo yake na wahariri juzi, Dk Bashiru alisema chama hicho kina taratibu zake za kupata viongozi kwani hata Rais aliyepo kwa sasa madarakani atapaswa kuomba ridhaa ya wana CCM ili ateuliwe tena.

Alionya kuwa safu iliyopo madarakani chini ya mwenyekiti wao (Rais Magufuli) iko imara na haiwezi kuyumba wala kuyumbishwa na katu hawawezi kumbeba mtu yeyote.

“Kuanzia kwangu mimi sikubebwa na sitabeba mtu, Rais Magufuli hajabebwa, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein hajabebwa hata makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula pia hajabebwa na hatambeba mtu,” alisema.

Alisema kazi kubwa iliyopo mbele yao ni kuendelea kurejesha umoja ndani ya chama na kuendeleza fikra za kuhakikisha Taifa linasonga mbele.

Hata hivyo, alisema kuna wagombea wameanza kupitapita, kudhamini makambi ya vijana, kutoa misaada ya mashuka katika hospitali huku wakiandika majina yao na wengine wanagawa kanga, akasema wamewafungulia mafaili ambayo yako chini ya Mangula.

“Uchaguzi wa mwaka kesho tutapunguza jeuri ya wanaotaka kutumia fedha katika uchaguzi kwani rushwa ni adui wa haki na mimi narudia kuwa sihongeki wala mwenyekiti hahongeki sasa wajiandae,” alionya.

Alisema hata wale ambao watashinda kura za maoni katika maeneo yao watambue kuwa haitakuwa kigezo pekee cha kuteuliwa kugombea kwa kuwa mifano wanayo katika majimbo ya Korogwe Vijijini, Songea, Singida Kaskazini na maeneo mengine.

Kamati ya Mangula

Mwaka 2014, Kamati Kuu ya CCM iliwapa onyo kali wanachama wake sita kwa kosa la kuanza kampeni za urais wa 2015 mapema kabla ya wakati.

Waliokumbana na onyo hilo ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe; mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.

Wengine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja. Awali, kamati ndogo ya maadili ya CCM iliwahoji viongozi hao waliotuhumiwa kukiuka taratibu za chama kwa kuanza kampeni mapema.

Baada ya kamati hiyo kumaliza kazi ilipeleka taarifa kwenye Kamati ya Maadili ya CCM iliyopeleka suala hilo kwa Kamati Kuu ambayo iliwapa karipio kali na kuwafungia kutogombea uongozi wowote ndani ya chama kwa mwaka mmoja



Chanzo: mwananchi.co.tz