Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Bashiru awapigania wakulima wa Kahawa

33969 Pic+bashiru Tanzania Web Photo

Sat, 29 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Karagwe. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amemwagiza naibu waziri wa kilimo Innocent Bashungwa kutafuta fedha za kuwalipa wakulima wa zao la Kahawa mkoani Kagera kwa bei inayoridhisha kulingana na gharama watumiazo katika uzalishaji.

Dk Bashiru alitoa agizo hilo jana Ijumaa Desemba 28, 2018 mbele ya wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa huo alipokutana nao wanaotoka wilaya ya Ngara Kyerwa na Karagwe.

alisema haiwezekani wakulima waendelee kutaabika kukosa fedha wakati Kahawa yao inashikiliwa na vyama vya ushirika.

Katibu mkuu huyo alisema licha ya Serikali kuzuia magendo ya Kahawa kutoka Kagera kuingia nchini Uganda lakini Kahawa inanunuliwa kiuficho kisha inasafirishwa ikifungwa ndani ya kasha au kopo la robo kilo  hadi nje ya nchi hiyo inakuwa na thamani kubwa katika soko la kibiashara nchini China.

"Waganda wananunua Kahawa kwa magendo wanaikaanga na kuifunga kwa kuweka picha ya mwanamke mrembo wa kiganda, wanaisafirisha hadi China kupitia bandari yetu inauzwa kakopo Sh40,000 iweje mkulima apatiwe Sh1,000"? alihoji Dkt Bashiru

Pia ameagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ngara Aidan Bahama kusitisha kazi ya kupora ardhi kuwanyang’anya wananchi wa wilaya hiyo kwa madai ya kuwagawia wawekezaji kutoka Korea Kusini.

"Nilikupigia simu kukuzuia sasa nakupa live sitaki kusikia wawekezaji wa nje wanaopewa ardhi bila kufuata utaratibu wa kuridhiwa kwanza na mikutano mikuu ya vijiji" alisema Dk Bashiru

Katika hatua nyingine, Dk Bashiru aliwahimiza viongozi na watendaji wa serikali ya mkoa huo kufanya kazi kwa ushirikiano katika kuboresha mazingira na miundombinu mbalimbali katika kutoa huduma bora za kijamii, bila kutofautiana kisiasa, kidini wala kikanda katika majimbo ya uchaguzi.

Mkuu wa mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti alisema wananchi wanahamasishwa kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya afya ambapo katika wilaya ya Kyerwa itajengwa Hospitali ya wilaya kwa fedha zinazotoka serikalini huku vikiboreshwa vituo vya afya na zahanati

Brigedia Jenerali Gaguti alisema katika kupambana na biashara ya magendo ya zao la Kahawa wilaya ya Misenyi imekamata magari 12 yenye tani zaidi ya 60 na pikipiki zilizosafirisha kahawa kwenda nchini Uganda na wamiliki wa vyimbo hivyo wametozwa faini Sh68 milioni na kahawa kutaifishwa.

"Fedha hiyo ilitumika kuimarisha ulinzi na usalama lakini pia kiasi kingine kiligawiwa halmashauri ya wilaya ya Misenyi kuboresha miundombinu katika huduma za kijamii" alisema Gaguti



Chanzo: mwananchi.co.tz