Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Bashiru: Wananchi wanaona uchaguzi ni kituko na maigizo

20915 Pic+bashiru TanzaniaWeb

Sat, 6 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema vitendo vya rushwa na kutowajibika kwa viongozi, kumesababisha wananchi wadharau uchaguzi na hivyo kutoshiriki na kusababisha kuwa na idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kupiga kura.

Katibu huyo wa chama tawala amesema kwa mara ya kwanza hali hiyo ilisababisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ambao waliojitokeza walikuwa asilimia 42 ya watu waliojiandikisha, kuzalisha Serikali ambayo ilikosa uhalali wa kisiasa.

Dk Bashiru aliyasema hayo jana wakati akizungumzia umuhimu wa wananchi kuiwajibisha Serikali wakati akitoa mada katika kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) lililofanyika kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu mjini Morogoro.

Kongamano hilo lilishirikisha zaidi ya wakulima 2,000 kutoka sehemu mbalimbali za nchi na liliandaliwa kuadhimisha miaka 25 ya mtandao huo.

Dk Bashiru alisema ushindi ambao CCM imekuwa ikiupata umekuwa ukitokana na wapigakura wasiofikia asilimia 50 ya wanaojiandikisha kupiga kura.

Wakati Dk Bashiru akieleza hayo, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (Nec), Dk Athuman Kihamia hakutaka kupingana na takwimu zake.

“Siwezi kuchangia (maoni ya NEC) kwa sababu yeye hadi anazungumza (hayo) atakuwa amefanya tathmini hivyo na sisi ili kuchangia itabidi tufanye tathmini,” alisema Dk Kihamia.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofurika wajumbe hao wa Mviwata, Dk Bashiru alisema ni lazima wananchi wawe sehemu ya mchakato wa kuwawajibisha viongozi wote ambao alisema wana vyeo walivyopewa na wananchi kwa njia ya kura.

“Ukweli ni kwamba mamlaka yote yaliyoko serikalini ni mali yenu, isipokuwa kuna mchakato wa usimamizi wa vyeo vyenu kupitia Serikali na moja ya michakato ni uchaguzi,” alisema.

“Hebu tujiulize, tabia yenu na mwenendo wenu wakati wa uchaguzi ukoje? Tuambizane ukweli. Mkishapewa kofia na T-Shirt, halafu nyimbo zikaanza kupigwa za mbele kwa mbele, huwa mnapata nafasi ya kuhoji sifa za mnayetaka kumchagua? Je, sifa ya chama kinachopiga mbele kwa mbele mnaijua?”

Alisema njia pekee ni kuwa sehemu ya mchakato wa kuwawajibisha wanaowachagua na kwamba wasichague viongozi kutokana na vitu wanavyowapa kwa kuwa kufanya hivyo ni kutengeneza viongozi watakaowaonea baadaye.

Alisema vitendo vya uonevu na dhuluma havifanywi na wakoloni, bali watu waliochaguliwa na wananchi au wanaoteuliwa na viongozi wa kuchaguliwa.

“Sasa watu ambao ni wajanja mimi naweza kusema, wapigakura wa Tanzania, watu ambao wamefikia hatua ya kudharau uchaguzi, wanakaa nyumbani kwa sababu wanaona ni kama vituko, ni mchezo wa kuigiza,” alisema Dk Bashiru.

“Na ndio maana leo kupata watu kuhudhuria kwenye kupiga kura imekuwa shida. Kote tunakoshinda chini ya asilimia 30, chini ya asilimia 40. Hakuna mahali wapigakura wamejitokeza kwa asilimia 50.”

Dk Bashiru alijenga hoja yake kwa kutoa mfano wa hali ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2010, ambao idadi ya watu waliojiandikisha ilikuwa milioni 20.13 lakini waliojitokeza walikuwa milioni 8.63.

“Mwaka 2010 ulitia fora, watu wengi walijiandikisha, zaidi ya asilimia 100 kumbe walikuwa wanataka kile kibali (kitambulisho cha mpigakura), kwa sababu kinatumika kwenda polisi kudhamini, unajitambulisha. Walipokipata wakaingia mitini,” alisema.

“Kwa Mara ya kwanza katika historia ya nchi hii tulipata Serikali ambayo haina uhalali wa kisiasa kwa sababu wapigajikura wengi zaidi ya ailimia 50 walibaki nyumbani.

“Tatizo hili halijaisha. Lakini wanasiasa wakishashinda wanasema ushindi ni ushindi tu hata kama ni kwa kura moja. Hajali kwamba ushindi ule unatakiwa uwe na uhalali.”

Alisema mfumo wa uchaguzi nchini umegubikwa na rushwa kiasi kwamba ilifika mahali wakati wa uchaguzi wagombea wanauza nyumba, wanakopa na kuitisha mikutano ya kuchangisha na wasipochangiwa wanakuwa wakali kama wanakwenda hospitali kutibiwa.

“Akishazikusanya fedha anakwenda kuwanunua wale mawakala na mawakala nao wanawanunua wapigakura. Msimu wa uchaguzi unakuwa msimu wa rushwa ya uchaguzi. Ninachowaomba, nafasi yenu ni kubomoa na kuharibu soko la kura,” alisema Dk Bashiru.

Alisema kama CCM itajipanga na wananchi kuona shule na hospitali, hakutakuwa na haja ya kwenda kuhonga.

“Ukiona mtu anakuhonga, hana sifa,” alisema.

Suala hilo la rushwa ya uchaguzi lilikuwa moja kati ya mambo manne aliyozungumza katika mkutano huo. Suala jingine lilikuwa ni umuhimu wa wakulima hao kuwa na umoja imara utakaosimamia na kutetea masilahi yao.

Alisema tangu aanze kazi hiyo, amekuwa akipokea malalamiko na mengi ni kuhusu haki za msingi na hasa suala la ardhi.

“Tuwe na ushirika wa wananchi kudai haki za msingi kama ardhi. Kataeni kuuzwa kwa ardhi kama mnavyokataa kuuziwa damu. Tangu nimeingia ofisini, asilimia 99 ya malalamiko ni ya ardhi. Wengi (wanaonifuata) ni maskini. Matajiri wanakwenda wizarani. Mtafanywa watumwa kwenye ardhi yenu,” alisema.

Akichambua mada kuu, Profesa Issa Shivji kutoka Kavazi la Mwalimu Nyerere, aliendelea kusisitiza umuhimu wa kuunda ushirika wenye nguvu ya kusimamia masilahi yao.

“Bila wakulima kuongeza nguvu zao, hawataweza kuzalisha na kulinda rasilimali zao. Mara nyingi tunaambiwa wazalishaji wadogo hawawezi. Ndio maana tunaalika wawekezaji,” alisema.

“Ni lazima muungane muwe na ushirika wenye nguvu. Ni tofauti na ushirika wa kuuza mazao tu. Ushirika huo ndio utakuwa unatoa mikopo. Benki za biashara haziwezi, mtaweka dhamana ardhi zenu zitaporwa.”

Shivji, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika harakati za haki za ardhi, aliitaka Serikali kuweka sera na sheria rafiki kwa wakulima wadogo katika masuala ya ardhi, mikopo na masoko.

“Mifumo wa umiliki ardhi haulindi ardhi ya wazalishaji. Kwa mfano kuna kifugu kinasema Serikali kupitia Rais inaweza kutwaa ardhi kwa manufaa ya umma na masilahi yenyewe ni pamoja na uwekezaji. Sheria na sera tulizonazo hazilindi masilahi ya ardhi ya wananchi,” alisema.

Akijadili mada ya mkutano huo inayoeleza nafasi ya wakulma katika uchumi wa viwanda, mmoja wa wakulima kutoka Kilombero, Richard Hanga alisema wakulima hawana nafasi katika uchumi huo kwa sababu bado wananyonywa.

“Inawezekanaje wakati ardhi inamilikiwa na mwekezaji ambaye ni mnyonyaji? Ili mkulima awe na nafasi kwenye viwanda lazima awe na ardhi,” alisema.

Huku akiitaja kampuni moja (jina linahifadhiwa) inayowekeza katika kilimo cha mpunga wilayani Kilombero, Hanga alisema imekuwa ikiwanyonya na kusababisha wananchi kuichukia CCM.

“Kuna vitu mnafanya vinawakosesha kura. Ndio maana ukienda kilombero mjini mbunge ni Chadema na Mlimba ni Chadema. Kwa sababu mkija mnaongea na wawekezaji mnatoka na bahasha. Hao wanaotakiwa kusimamia uchumi wa viwanda ni wapotaji wanaotaka kujimilikisha rasilimali,” alisema.

Hata hivyo, Kamishna wa Ardhi, Mary Makondo, ambaye alikuwepo mkutanoni, alisema masuala ya ardhi yapo kisheria na kwamba Serikali imeshaanza kutatua kero za wananchi, hasa migogoro ya ardhi na kurejesha mashamba pori yaliyokuwa mikononi mwa wawekezaji.

Chanzo: mwananchi.co.tz