Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Bashiru: UWT ina majukumu zaidi ya uchaguzi

15674 Pic+bashiru TanzaniaWeb

Wed, 5 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Upo msemo kwamba ‘wanawake ni jeshi kubwa na ushindi ni lazima’. Msemo huu umekuwa ukitumika mara nyingi wanapokutana wanawake wa CCM kupitia umoja wao wa UWT na kupitia kwake, wengi hupata tafsiri kwamba ushindi unaozungumziwa ni wa kisiasa katika chaguzi mbalimbali.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ana mawazo tofauti. Wiki iliyopita alipofungua kikao cha Baraza Kuu la UWT, alitoa tafsiri pana zaidi, ili msemo huu usiwe unamaanisha tu uchaguzi.

Anasema ushindi uwe lazima dhidi ya mifumo yote ya unyonyaji na ukandamizaji ambayo ndio msingi wa kuanzishwa kwa UWT.

“Mimi ukiniuliza ushindi juu ya nini? Nitakujibu ni juu ya mifumo ya unyonyaji na ukandamizaji. Huu ndio msingi wa kuanzishwa kwa chombo hiki (UWT), uliofanywa na waasisi wa chombo hiki akiwamo marehemu Sophia Kawawa,” anasema Dk Bashiru.

Msoni huyo wa siasa anasema endapo wanawake wataelekeza jeshi lao kubwa katika kufichua na kutoa taarifa juu ya mifumo ya ukandamizaji na unyonyaji, wataisaidia jamii kwa sababu bado ipo na inaendelea kulisumbua Taifa.

“Kwa hiyo nyinyi ni jeshi kubwa dhidi ya mifumo ya unyonyaji na ukandamizaji. Bado kazi ipo mjifunge kibwebwe, muungane na mwenyekiti wetu na chama kuhakikisha malengo ya waasisi yanatimia,” anasema Dk Bashiru na kufafanua kuhusu uchaguzi.

“Baada ya kumaliza uchaguzi, tufanye kazi ya kupambana na mifumo (ya unyonyaji na ukandamizaji kwa kuelekeza jeshi lao kubwa kwenye mapambano hayo katika maeneo mbalimbali nchini.

Eneo lenye ukandamizaji

Dk Bashiru anaitaja sekta ambayo wanawake wa CCM wanapaswa kuiangalia miongoni mwa sekta nyingi kuwa ni ardhi. Anasema Sekta ya Ardhi imekuwa na migogoro mingi kutokana na udhaifu katika mipango na usimamizi wake.

Katibu Mkuu anaeleza kukerwa na baadhi ya viongozi wanaokumbatia migogoro hiyo kwa kujinufaisha.

“Hivi karibuni imezuka tabia miongoni mwetu wengine ni baadhi ya viongozi wetu kuhodhi ardhi au kuwageuza Watanzania kuwa vibarua kwa kuwakodishia au vyombo vinavyosimamia (ardhi) kugubikwa na rushwa na hivyo kuwafanya watu kukosa haki wanapokuwa na migogoro,” anasema.

Kinyume na idhaniwavyo, anasema yanayoonekana katika vyombo vya habari kuwa Serikali inachukua hatua mbalimbali za kutatua migogoro ya ardhi hayafanani na hali halisi katika maisha ya wananchi.

“Viongozi na mawaziri katika sekta hii acheni kufanya kazi na vyombo vya habari, nendeni kufanya kazi katika maeneo ambayo kuna migogoro,” anasema.

Bashiru anawataka wanachama hao kuwaumbua viongozi wanaosema wanafanya kazi vizuri katika kutatua migogoro lakini kwenye maeneo hali bado hali ni mbaya.

Akitoa mfano wa kauli yake, Dk Bashiru anasema, “Nilikuwa Morogoro akatajwa waziri mmoja ana eka 1,000, watu wanasema wanataka kujua amezipataje na mimi nitamwita nimuulize amezipataje, kusudi nikawajibu wale walioniuliza.

Waziri ahusishwa, ang’aka

Pamoja na kuwa Dk Bashiru hakutaja jina la waziri husika, lakini Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliwahi kuhusishwa na wananchi kuwa amechukua mashamba ya wananchi hao eka 700 na nyingine 300.

Hata hivyo, Mpina alipoulizwa kuhusu kuhusishwa kwake na mashamba hayo, alilijibu gazeti hili kuwa

“Hayo unayouliza ni majungu, acha majungu bana na kama katibu mkuu ameongea si umuulize yeye katibu mkuu. Alipoulizwa iwapo mshamba hayo ni ya kwake Mpina alikata simu.

Lakini katibu mkuu anasema, “Hatuwezi kuwa na chama kinachojitambulisha ni cha wanyonge halafu tunapora ardhi ya watu. Ni suala la kuchagua kati ya kuwa kiongozi wa CCM au kuwa mporaji wa ardhi ya watu.

Anatoa agizo kwa wanawake akisema, “Kazi yenu ni kuwataja na kulinda haki ya ardhi hasa ile ya wazalishaji wadogo.”

Ubora wa elimu

Mhadhiri huyo wa zamani wa chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anampongeza Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kwa kauli yake kuwa kunahitajika mjadala mpana na shirikishi katika kukuza ubora wa elimu nchini.

Hata hivyo, anasema hajasikia kama kauli hiyo imepata mapokeo mazuri na kuwataka wajumbe wa baraza kuu la wanawake kumuunga mkono Mkapa katika kufanya mijadala ya wazi na ya kina juu ya hali ya elimu nchini.

“Hili naliacha mezani mlijadili, mna watoto, mkono wenu ni mrefu katika elimu, kaeni mkishauri chama tufanye nini ili sekta ya walimu inayopanuka kwa kasi iweze kutuzalishia watoto ambao wataweza kuijenga nchi miaka ijayo,” anasema.

Kwa maoni yake, Dk Bashiru anasema ingawa fedha katika sekta ya elimu zimeongezeka, shule za umma zimepanuka, udahili wa wanafunzi umeongezeka lakini usimamizi wake bado ni dhaifu.

“Tumejikuta tunatumia muda mwingi na fedha nyingi lakini matokeo bado ni madogo sana hasa katika eneo la ubora, pia katika masilahi ya walimu na mazingira ya kujifunzia,” anasema.

Anasema chama hicho kinalo jukumu la kuhakikisha linaisimamia Serikali ili kupata matokeo yanayolingana na uwekezaji unaoendelea katika sekta ya elimu.

Amtetea Makilagi

Dk Bashiru anasema kuna watu wanaosema aliyekuwa Katibu Mkuu wa UWT, Anna Makilagi aliondolewa kwenye nafasi hiyo kwa sababu ya ubadhilifu wa mali za chama, jambo ambalo halina ukweli.

Anasema wapo watu wengine kazi yao ni kuwakatisha tamaa viongozi kwa kuwasingizia mambo ambayo hayana ukweli.

“Nilikuwa katika kamati (ya kuchunguza mali za CCM) sikukuta uhalifu ila nilichokuta ni makundi ya uchaguzi. Kama mna shida naye, hangaikeni naye huko (kwenye makundi ya uchaguzi) lakini si huku (kwenye ubadhirifu),” anasema.

Mitambo ya uongo

Pamoja na kukosoa suala la Makilagi, Dk Bashiru anasema kuna mitambo ya uongo ndani ya CCM ambayo inatengeneza uongo kwa ajili ya kuwabomoa washindani wa baadhi ya watu ndani ya chama.

“Chama chetu kinasema sitasema uongo na fitina kwangu ni mwiko, lakini mitambo ya uongo imejaa ndani ya chama. Mtu anaweza kutengeneza na kuchonga jambo kwa nia ya kumdhoofisha mpinzani wake kisiasa. Wanawake nyie ni jeshi kubwa, tukisaidie chama chetu kubomoa hiyo mitambo ya uongo kwa sababu haina nidhamu,” anasema.

Makundi UWT

Hata hivyo, Mwenyekiti wa UWT, Gaudensia Kabaka anasema makundi ya uchaguzi lazima yawepo kwa sababu ya idadi ya wagombea kuwa kubwa, lakini ubaya unakuja pale yanapoendelea kuwepo baada ya uchaguzi.

“Hayatakiwi, hayana afya, yanatuletea vurugu. Na katibu mkuu utakumbuka nimekushirikisha katika baadhi ya wilaya na mkoa mmoja ambao umetupa shida ya makundi ya uchaguzi. Kwa hiyo hili vuguvugu la makundi ya uchaguzi na hisi bado lipo halijatulia katika maeneo mengine,” anasema.

Anasema hata hivyo, wanaenda vizuri kwa kuelekezana kwa sababu yakiendelea kuwepo yataleta shida katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwakani na uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Kuzingatia kanuni

Anasema yako matatizo ya kutozingatia kanuni na miongozo ikiwamo baadhi ya wenyeviti wa mikoa na wilaya wa chama hicho kujihusisha na masuala ya fedha kinyume cha kanuni za chama ambazo zinampa mamlaka katibu mkuu kushughulika na masuala hayo.

“Unamkuta mwenyekiti anaenda benki kuchukua fedha, anapanga matumizi, ndiye anatumia na kusimamia miradi. Si kazi yenu hiyo. Mwenyekiti kazi yake ni kusimamia vikao ili vijadili na kupanga hizo bajeti na si kujishughulisha na fedha,” anasema Dk Bashiru.

Urais wa Zanzibar

Katibu mkuu hakuacha kuonya kuhusu makundi ya kusaka urais wa Zanzibar, akiwataka wanawake hao kuelekeza majeshi kwa watu ambao wameanza kujenga makundi ya kuwania urais wa Zanzibar.

Kuhusu hilo, anasema kwa bahati mbaya wanaCCM wanaoshiriki kampeni kabla ya muda, baadhi yao ni mawaziri na anatumia fursa hiyo kuwahoji ni nani aliyesema Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Ali Shein amemaliza muda wake wa uongozi.

“Mawaziri wanatumia muda wa Serikali, ofisi za Serikali, magari ya Serikali, simu za Serikali na posho za Serikali. Hatutaki viongozi wa chama kutumia muda wao kuendesha makundi ya kusaka uongozi. Mkiwakatalia hawatafika mbali, waelezeni ukweli,” alisema.

Alisema kitendo cha kuingia katika makundi ya kutafuta uongozi kinawapotezea sifa wanachama wa CCM.

“Mkiingia katika kompyuta yangu kuna jina la kila mmoja alichosema, wakati ukifika tuta-print (kuchapisha) na kuwapa wajione na wakijiona hawatathubutu hata kuchukua fomu,” alisema.

Aliongeza kuwa Mtanzania yoyote anaweza kuwa rais, lakini unakuta “Mtu anajipamba, anajipaka wanja, kisa urais. Mtu anayefaa kuwa rais hajipitishi kuombaomba. Mtu bora anayefaa kuwa rais anaombwa,” alisema.

Aidha, Dk Bashiru alisema kuna tatizo la uhusiano baina ya watendaji au mawaziri hawaelewani na manaibu wao ingawa wote ni wateule wa Rais.

“Wakati mwingine kiongozi wa kuchaguliwa hawaelewani na watendaji, viongozi wa chama hawaelewani na wa Serikali. Unakuta DC ana mgombea wake, mwenyekiti wa halmashauri ana mgombea wake, katibu wa chama ana mgombea wake, hivyo hakuna shughuli inayofanyika bali kusaka vyeo,” alisema.

Katibu mkuu alisema amewaambia wabunge watulie yeye atawalinda kwa sababu muda wa kujipitisha pitisha kuomba uongozi bado haujafika.

Chanzo: mwananchi.co.tz