Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Bashiru: Muswada huu usibadilishwe hata koma

Fri, 18 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali, amesema muswada wa sheria ya vyama vya siasa ni mzuri hivyo asingetamani upunguzwe hata koma.

Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 17, 2019 Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa wanachama wa CCM wa mkoa wa Dodoma waliokusanyika kutoa maoni yao kuhusu muswada huo.

Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa White House ambao ulifurika wana CCM, Dk Bashiru alisema kuna wababaishaji ambao wanataka kuyumbisha nchi kwa maslahi yao binafsi.

"Kuna mbabaishaji mmoja sitaki kumtaja jina alikimbia chama fulani akisema wanatumia vibaya ruzuku lakini leo tunaleta muswada wa kudhibiti ruzuku kwa vyama anapinga tena, huyu ni mtayarishaji," amesema Dk Bashiru.

Dk Bashiru amewataka wana CCM kuujadili muswada kwa nia njema kwani unakwenda kuimarisha siasa za Tanzania na kuweka imara vyama vya siasa na vinavyotaka kuanzishwa.

"Lakini msiwe na wasiwasi, mashine zimetegwa tayari kinachosubiriwa ni kuanza kazi tu wala si kusubiri, tuko imara kisiasa na chama chenu kiko imara kuliko wakati mwingine," amesema.

Kiongozi huyo amewataka viongozi wa CCM kujipanga kwa uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Dk Bashiru pia amepinga kauli kwamba CCM kinataka kurudi katika mfumo wa chama kimoja akisema hilo haliwezekani kwani hata Mwalimu Nyerere alishatoka huko hivyo hawatarudi nyuma.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz