Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Bashiru: Hawatopoa kusimamia nidhamu na utendaji kazi

23058 Ccm+pic TanzaniaWeb

Sat, 20 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho na Serikali yake hawatapoa katika kusimamia nidhamu na utendaji kazi ili kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Dk Bashiru ameyasema hayo juzi Jumatano Oktoba 17, 2018 mjini Beijing nchini China alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Mje wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Song Tao.

Taarifa iliyotolewa kwa umma leo Ijumaa Oktoba 19, 2018 na Grace Kingalame ambaye ni  mwenyekiti wa kamati ya mawasiliano Jumuiya ya Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) imemnukuu Dk Bashiru akisema Serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli iko imara.

Dk Bashiru amesema hakuna uzembe utakaovumiliwa na mtumishi wa aina yeyote awe wa chama au Serikali ambaye kwa makusudi atakwamisha mipango na nia njema ya Serikali.

“Tutazidi kuwa wakali na kusimamia nidhamu kwa vyombo vya chama na Serikali ili kuhakikisha juhudi zinazofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Rais Magufuli, zinafikiwa,” amesema Dk Bashiru

Katibu mkuu huyo ametolea mfano juhudi zinazofanywa na Serikali ni pamoja na uboreshaji wa miundobinu ya barabara, akiitaja barabara ya juu ya Mfugale ambayo imejengwa katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere jijini DSM, Tanzania.

Amesema barabara hiyo kwa kiasi kikubwa ina lengo la kupunguza msongamano wa magari, uboreshaji wa shirika la ndege la Tanzania (ATCL), Shirika la simu (TTCL), huduma za afya na uboreshaji wa elimu kwa kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne.

Dk Bashiru amesema katika siku chache walizokuwa China wamejifunza mambo mengi ambayo Tanzania wanaweza kuyatekeleza na kufika mbali lakini kubwa akisisitiza nidhamu ya uwajibikaji na kuweka maslahi ya Taifa mbele.

Naye mwenyekiti wa UWT, Gaudentia Kabaka amesema yapo mengi ambayo amejifunza kupitia wanawake wa CPC ambapo amesema ni lazima wanawake wa Tanzania wawe chachu ya maendeleo kwa kufanya kazi, kujiheshimu na kusimamia maadili ili Tanzania iwe na watu watakaolisaidia katika maendeleo ya nchi badala ya kuwa na jamii ya kukaa vijiweni na kulalamika.

Akiwa nchini China pamoja na ujumbe wake, Dk Bashiru ametembelea chuo maalum cha kuwaandaa viongozi wa chama na serikali katika ngazi mbalimbali kinachosimamiwa na CPC.

Pia, ametembelea ukuta wa kihistoria uliojengwa na China miaka 200 iliyopita ili kujilinda na maadui, miradi mbalimbali inayotekelezwa na vijana wa CPC, shughui za akina mama wa CPC China na namna wanavyoisaidia serikali katika maendeleo.

Dk Bashiru yupo nchini China kwa ziara ya takriban siku kumi ya makada wa CCM na jumuiya zake kwa mwaliko wa CPC ambacho ni chama rafiki kwa CCM na Tanzania kwa muda mrefu.

Chanzo: mwananchi.co.tz