Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diwani mwingine Chadema ajiuzulu, ajiunga CCM

11816 Ajiuzulu+pic TanzaniaWeb

Thu, 19 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Diwani wa Nasa (Chadema), Solomon Mmary amejiuzulu leo Alhamisi Julai 19, 2018 na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Valerian Juwal amethibitisha kupokea barua ya diwani huyo kujiuzulu huku Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya akieleza kuwa wamejipanga kesho Julai 20,2018 kumpokea Mmary pamoja na kumkabidhi kadi ya CCM.

Mmary amejiuzulu ikiwa ni siku chache tangu alipovuliwa uenyekiti wa Chadema wilaya ya Siha. Kata hiyo ipo wilayani Siha Mkoa wa Kilimanjaro.

Mmary amesema amechukua uamuzi huo ili kuunga mkono juhudi za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.

Amesema amechukua hatua hiyo kutokana na vikwazo alivyokutana navyo ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini, ikiwa ni pamoja na kulalamikiwa kushirikiana na mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel ambaye awali alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema.

"Niligombea udiwani ili kushughulika na matatizo ya wananchi na baada ya kuchaguliwa niliamini siasa zimeisha,  ni muda wa kufanya kazi hivyo nilifanya kazi ya kuleta maendeleo, lakini nimepata vikwazo vingi," amesema.

Diwani huyo anakuwa wa 51 wa Chadema kujiuzulu tangu mwaka 2015.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz