Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diwani aliyewekwa ndani na DC aachiwa kwa dhamana

12020 PIC+DIWANI TanzaniaWeb

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Diwani wa Chadema, Nice Gisunte aliyewekwa ndani kwa amri ya mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema ameachiwa kwa dhamana.

Gisunte aliyekuwa akishikiliwa kituo cha polisi Stakishari jijini Dar es Salaam, aliachiwa kwa dhamana jana Agosti 14, 2018 saa tatu usiku.

Mkuu wa wilaya Mjema, juzi alitoa amri ya kukamatwa na kuwekwa ndani kwa saa 48 Gisunte ambaye ni diwani wa  Kitunda akidaiwa alitaka kuvuruga ziara yake.

Akizungumza na MCL Digital leo Agosti 15, 2018, Gisunte amesema alitoka mahabusu jana baada ya mkuu wa upelelezi kumweleza atafute mdhamini ili apatiwe dhamana.

“Muda wangu wa saa 48 alizosema Mjema ulitakiwa kumalizika leo saa sita  mchana lakini jana mkuu wa upelelezi aliniambia nitafute mdhamini mmoja kwa ajili ya kupewa dhamana na leo niende kuripoti polisi,” amesema Gisunte.

Amesema si kweli kuwa alitaka kuvuruga ziara ya mkuu wa wilaya bali yeye alikuwa anatimiza majukumu yake kama diwani wakati mkuu wa wilaya alitaka kuingiza siasa katika mkutano.

Gisunte amesema wakati mkuu wa wilaya akihutubia wakazi wa Kitunda alikuwa kimya na mtulivu akimsikiliza lakini aliingiza siasa kwa kutoa salamu za CCM katika mkutano wa Serikali.

“Nilimwambia Mjema ukianza kusema salamu za CCM nami nikisema za Chadema itakuaje kwa sababu ndiyo ninayeongoza kata hiyo. Nilimwambia hupaswi kufanya hivyo,” amesema.

Gisunte amesema, “Baada ya kauli hii, Mjema aliagiza polisi wanikamate na kuniweka ndani. Niseme baadhi ya viongozi wanatumia madaraka yao vibaya, ni vyema wakatenganisha shughuli za chama na Serikali.”

Amesema viongozi wakiendelea na hatua hiyo watasababisha mgawanyiko kwa wananchi kwa sababu wana itikadi tofauti za vyama.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo akizungumza na wakuu wa wilaya wapya jana, alikemea tabia ya baadhi yao kutumia madaraka vibaya kwa kuwaweka watu ndani.

Chanzo: mwananchi.co.tz