Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diwani CCM adaiwa kutumia ng’ombe kuingiza bidhaa kwa magendo

46335 Pic+kino+polisi Diwani CCM adaiwa kutumia ng’ombe kuingiza bidhaa kwa magendo

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Polisi mkoa wa Kinondoni kwa kushirikiana na mkuu wa wilaya hiyo, Daniel Chongolo wamemkamata diwani mmoja wa CCM (jina tunalo) na wenzake wanne kwa tuhuma za kuingiza bidhaa mbalimbali za magendo ikiwemo mifuko 72 ya sukari.

Akizungumza leo Jumanne Machi 12, 2019, Chongolo amesema diwani huyo amekuwa akishirikiana kuingiza vitu vya magendo kupitia fukwe za Bahari ya Hindi zilizopo Mbweni Vijijini jijini Dar es Salaam akishirikiana na watuhumiwa wengine ambao ni wakazi wa Mbweni.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa na mifuko 72 ya sukari, mafuta ya kula madumu 25, pikipiki mbili, mashine ya boti moja na ng'ombe wawili.

Amesema shehena hizo zilikamatwa usiku wa kuamkia leo Jumanne zikitokea Zanzibar ambazo zilipakiwa kwenye  majahazi na zilipofikishwa kwenye fukwe za bahari eneo hilo watuhumiwa hao walitumia ng'ombe wawili kusomba sukari na mafuta hayo.

"Ng'ombe hawa wanaspeed ya ajabu wanapochukua sukari na mafuta wanapeleka moja kwa moja kwenye nyumba husika anakotakiwa kushusha na kila mmoja ana uwezo wa kubeba mifuko 20 ambao kila mmoja una kilo 50 na madumu 20 ambapo kila moja lina lita 20,"alisema Chongolo.

Pia, Chongolo ametoa siku mbili kwa wananchi wa eneo hilo wanaotumia ng’ombe hao kwa ajili ya kubebea shehena za magendo wahakikishe wanawapeleka kituo cha polisi Mbweni wasipofanya hivyo watawachukulia hatua za kisheria.

Amesema wanawafahamu wote wenye ng'ombe hao wakiwaacha watu wataendelea kuwatumia kuingiza vitu vya magendo ambavyo havina ubora matokeo yake wataendelea kuwaua wananchi kwa kuwalisha bidhaa zenye sumu.

Mkuu wa upelelezi wilaya ya Kawe, Dk Ezekiel Kyogo amesema watuhumiwa hao ni wajanja wanapoona mzigo umeshafika wanawaagiza ng’ombe hao ambao wanaenda pembezoni mwa fukwe na wanapofika wanachukua na kupeleka eneo husika.

"Inavyoonekana hawa ng'ombe wamepewa mafunzo wanajua sehemu gani ya kuchukua mzigo na wanapeleka sehemu husika tena kwa haraka sana(speed),” amesema



Chanzo: mwananchi.co.tz