Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diwani CCM achaguliwa kuwa Meya Ilala

69088 Pic+meya

Wed, 31 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Diwani wa Vingunguti (CCM), Omary Kumbilamoto leo Jumatano Julai 31, 2019 amechaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Ilala baada ya kupata kura 41 dhidi ya mpinzani wake, diwani wa Kinyerezi (Chadema), Greyson Selestine aliyepata kura 14.

Kumbilamoto amechukua nafasi ya Charles Kuyeko aliyejiuzulu Machi 23, 2019 baada ya kutangaza kukihama chama chake cha Chadema na kujiunga na CCM.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni katibu tawala wa wilaya ya Ilala, Sheila Lukuba amesema kura zilizopigwa ni 55 na  Kumbilamoto amepata kura 41 na Selestine kura 14.

“Kwa matokeo haya, ninamtangaza Kumbilamoto kuwa meya wa manispaa ya Ilala,” amesema Lukuba wakati akitangaza matokeo hayo huku madiwani wa CCM wakishangilia wakati meya huyo akielekea meza kuu.

Kumbilamoto amewashukuru madiwani wote kwa kumchagua kuwa meya na kuahidi kuongeza kasi ya utendaji katika halmashauri hiyo ili kuendana na kasi ya Rais John Magufuli ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa upande wake, Selestine amesema ameacha demokrasia ifanye kazi yake na kwamba huu siyo wakati wa malumbano. Hata hivyo, amesema utaratibu uliotumika wa kuandika jina la mgombea badala ya kuweka alama ya tiki haukubaliki kikanuni.

Pia Soma

“Kura ni siri ya mtu, unapoandika jina zima la mgombea usiri unapotea kwa sababu kila mtu ana mwandiko wake na unaweza kutambuliwa kwa mwandiko wako,” amesema Selestine.

Wakati upigaji kura ukianza, kuliibuka mvutano kati ya msimamizi wa uchaguzi na baadhi ya madiwani waliotaka kutoa taarifa. Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi hakuwapa nafasi na kuendelea na upigaji kura.

Diwani wa Segerea (Chadema), Edwin Mwakatobe amesema taarifa aliyotaka kumpa msimamizi ni kuhusu utaratibu wa kuandika jina kwenye karatasi ya kupigia kura wakati kanuni zinaelekeza kwamba kura inakuwa na majina ya wagombea na madiwani wanaweka alama ya vema mbele ya mgombea.

Chanzo: mwananchi.co.tz