Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dijitali inavyowezesha vyama kupata fedha

CHADEMA Vs CCM Dijitali inavyowezesha vyama kupata fedha

Thu, 3 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maendeleo ya teknolojia ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazotumiwa na makundi mbalimbali ya kijamii kufanikisha shughuli zake.

Vyama vya siasa ni kati ya makundi ya kijamii yanayochangamkia matumizi ya teknolojia katika shughuli zake kwa lengo la kuongeza ufanisi, ikiwemo kusajili wanachama, kukusanya ada na michango mbalimbali.

Kwa uchache, ACT-Wazalendo, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ni miongoni mwa vyama vilivyochangamkia matumizi ya teknolojia kufanya shughuli za kisiasa.

Vyama vyote vitatu tayari vimezindua kadi mpya za wanachama za kielektroniki ambazo siyo tu zina taarifa zote muhimu za mwanachama, bali pia zinatambulika na kuwawezesha kulipa ada za uanachama.

Wakati CCM imezindua kadi hizo ikiwa imepita miaka 45 tangu chama hicho tawala kiundwa Februari 5, 1977 baada ya kuungana kwa vyama vya ukombozi vya Tanu (Tanganyika) na Afro Shirazi Party kwa upande wa Zanzibar, Chadema wao walizindua kadi zao za kielektroniki Mei, 2021.

Akizindua kampeni ya kwenda kidijitali wakati wa halfa iliyofanyika jijini Arusha, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kwenda kidijitali kitakiimarisha chama hicho kiuchumi kwa sababu wanachama watalipa ada kwa wakati na hivyo kuondoa utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali inayotolewa kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kulingana na uwakilishi kwenye halmashauri na bungeni.

Mbowe alisema kutokana na zuio la mikutano ya hadhara na shughuli za kisiasa, Chadema kitatumia teknolojia kuendesha operesheni nchi nzima kupitia vikao na mikutano ya ndani itakayohusisha wanachama popote walipo.

“Operesheni hiyo itafanyika nchi nzima na moja ya mikakati yake ni uelekeo wa chama wa kubadili mfumo wake wa kuendesha siasa kwa kufanya siasa zisizo za kiharakati ili kupata uungwaji mkono mpya kutoka kwa wananchi wa ngazi zote,” alikaririwa akisema Mbowe wakati wa uzinduzi.

Operesheni hiyo ya Chadema ya kidijitali yenye kauli mbiu ya “Tunakwenda Kidijitali” itahusisha kuandikisha upya wanachama na kupewa kadi za kielektroniki, ambazo ziko katika makundi matano kulingana na kiwango cha pesa kitakachotolewa na wanachama.

Chama cha ACT-Wazalendo nacho kilizindua kampeni ya kujiendesha kidijitali, ikiwemo uandikishaji wa wanachama ambapo katika taarifa yake kwa umma Januari 24, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu anasema mfumo huo siyo tu utarahisisha uendeshaji, bali pia uwezo wa chama kiuchumi.

ACT Wazalendo ambacho kinahesabiwa kuwa chama cha tatu kwa ukubwa nchini nyuma ya chama tawala CCM na Chadema, tayari kimetoa kadi za kielektroniki kwa viongozi na wanachama kadhaa.

Hivi sasa viongozi wa chama hicho wanafanya ziara katika maeneo tofauti nchini kuutambulisha mfumo huo ambao si tu utakifanya kiende kisasa, lakini pia kiboreshe utendaji kazi wake.

Teknolojia kutumika kuruka viunzi

Japo viongozi wake wanasisitiza kuendeleza mfumo wa asili wa kufanya siasa za viongozi na wanachama kukutana uso kwa uso, Chadema ni kama imeamua kupiga hatua moja mbele katika matumizi ya teknolojia kwenye siasa.

Ukweli huu unadhihirishwa na tukio la wiki iliyopita la Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu kuwahutubia viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho akiwa ughaibuni nchini Ubelgiji, umbali wa zaidi ya kilomita 11,000.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusu mkutano huo wa Lissu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche anasema maendeleo ya teknolojia yamevunja minyororo inayotumiwa na mamlaka kuzuia watu kukutana kujadili mambo na mustakabali wao.

“Zaidi ya robo tatu ya wanachama wetu wamezungumza moja kwa moja na Makamu Mwenyekiti wetu Lissu akiwa umbali wa zaidi ya kilimita 11,124. Teknolojia imefanya dunia kuwa kijiji, huku ikivunja minyororo ya fikra za kikoloni za kuminya uhuru wa maoni kwa kuzuia watu kukutana,” anasema Heche.

Huku akisisitiza msimamo wa Chadema wa kuendelea kufanya siasa za jadi na asili za watu kukutana uso kwa uso, Heche ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, anasema uwepo wa teknolojia umefifisha zuio la shughuli za kisiasa, ikiwemo mikutano ya hadhara lililodumu tangu mwaka 2016 hadi sasa kinyume cha sheria.

“Teknolojia imerahisisha siasa na kufanya vyama vya siasa vya upinzani kuendelea kufanya siasa na kujiimarisha zaidi kinyume cha matarajio ya watawala waliozuia shughuli za kisiasa kwa nia ya kudhoofisha vyama vya upinzani,” anasisitiza Heche.

Anasema matumizi ya teknolojia katika shughuli za kisiasa ni uthibitisho kuwa dunia imekataa mbinu za jadi zilizotumiwa na watawala tangu enzi za ukoloni za kuzuia watu kukutana ili kuwanyima fursa ya kujadiliana kuhusu maisha yao na namna nchi inavyoendeshwa.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo aliyeibukia kwenye siasa za vyuoni anasisitiza kuwa kamwe Chadema na vyama vingine vya upinzani havitatoka kwenye mfumo na njia ya jadi ya kufanya siasa kwa viongozi na wanachama kukutana uso kwa uso kwa sababu kukutana uso kwa uso kunatoa fursa ya kila mmoja kuona na kupata hisia za mwingine.

Katibu wa ACT-Wazalendo mkoa wa Mwanza, Emmanuel Mashiku anaunga mkono hoja ya matumizi ya teknolojia katika siasa, akisema siyo tu imerahisisha kusajili na kuwatambua, bali pia ukusanyaji wa mapato kupitia ada za uanachama kwa sababu malipo hufanyika moja kwa moja kwa njia ya mtandao.

“Watu wanajiunga na chama kwa njia ya mtandao, wanalipa ada kimtandao na hata mawasiliano yetu sasa ni kimtandao kwa sababu ujumbe mmoja unaweza kutumwa na kuwafikia wanachama wote kwa wakati mmoja,” anasema Mashiku.

Anasema kupitia mitandao, viongozi na wanachama ndani na nje ya nchi wanaweza kufuatilia mikutano na matukio ya kisiasa ya chama bila kulazimika kuwepo eneo moja.

“Hotuba ya kiongozi wa chama inaweza kufuatiliwa kila pembe ya dunia kwa njia ya mtandao. Hata utoaji wa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari pia umeimarika na kuboreka zaidi kwa sababu taarifa hiyo inaweza kufikia umma wote kwa wakati mmoja na kwa gharama nafuu,” anasema Mashiku.

Mapato na nguvu ya kiuchumi

Akizungumzia nguvu za kiuchumi, Heche anasema kupitia njia ya mtandao, Chadema inaweza kukusanya zaidi ya Sh1 bilioni kwa mwezi iwapo wanachama milioni moja watachangia Sh1,000 kila mmoja.

“Hatuhitaji kuendelea kutegemea ruzuku kutoka serikalini kuendesha shughuli za chama iwapo wanachama milioni moja pekee wa Chadema watajitolea kuchanga Sh1,000 tu kwa mwezi. Chama chetu kina zaidi ya wanachama 7 milioni, kila mmoja akichangia Sh1,000 kwa mwezi tutakusanya zaidi ya Sh7 bilioni na hivyo kumudu kujitegemea,” anasema Heche.

Anasema vyama vya siasa vinapopata misuli ya kiuchumi vitamudu kuendesha shughuli zake, ikiwemo ujenzi wa miundombinu na mitandao kuanzia ngazi ya chini.

“Uwezo wa kifedha utatuwezesha kujenga ofisi za chama kila wilaya, mkoa, kanda na taifa. Tutanunua magari, pikipiki na vyombo vingine vya usafirishaji kwa ajili ya viongozi na watendaji wa chama. Hii itawezesha na kuongeza kasi ya kushinda uchaguzi na kushika dola,” anasema.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo naye ameonyesha umuhimu wa matumizi ya teknolojia wakati wa uzinduzi wa kadi za kidijitali mjini Musoma Februari 5, ambapo alitangaza kuwa ifikapo Februari 5, 2027, chama hicho kitakuwa kimekamilisha usajili wa wanachama wake wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 12 milioni.

NCCR-Mageuzi

Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma wa NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye alisema suala la kuhamia kwenye dijitali ni la lazima kwa chama chochote kinachotaka kuendelea kubaki kwenye siasa kutokana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia.

Alisema chama chake kiko kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya uzinduzi wa mpango wa chama hicho kuendeshwa kidijitali ambao utaambatana na mabadiliko makubwa ya chama, ikiwamo rangi za chama.

“Sisi tuko kwenye hatua za mwisho za maandalizi, siyo tu ya kwenda kwenye dijitali, lakini kufanya kitu kinaitwa ‘party rebranding’, ni tukio kubwa ambalo linahitaji utulivu mkubwa na investment kubwa.

“Tuko asilimia 70 ya maandalizi kwa sasa ambapo tutakuja na mabadiliko makubwa sana, hata ya mwonekano wa rangi za bendera yetu na pia tutazindua huo mfumo wa dijital na tutakuwa na mashine za kisasa zaidi zenye uwezo wa kuzalisha kadi 14,000 – 20,000 kwa saa,” alisema Simbeye.

Alisisitiza kwamba wameajiri kampuni za nje kwa ajili ya ushauri na wamejiandaa vizuri katika jambo hilo, tofauti na vyama vingine ambavyo viliingia kwenye mfumo wa kidijitali bila maandalizi ya kutosha.

Mikakati ya CUF

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya alisema chama hicho kinaendelea na uratibu wa mfumo wake wa kidijitali na ukikamilika utazinduliwa rasmi kwa ajili ya kutoa kadi za kielektroniki kwa wanachama wake pamoja na ulipaji wa ada za uanachama.

“Kila kitu huwa kinapitishwa na mamlaka za maamuzi, mpango huu ulishapita kwenye vikao vyote vya kikatiba, vikao vikuu, ukapata baraka zote. Kwa hiyo sasa hivi mchakato unaendelea, ukikamilika utazinduliwa rasmi,” alisema.

Alisisitiza kwamba wanatarajia kuwa na kadi za wanachama za kielektroniki, usajili kuanzia ngazi za wilaya pamoja na kanzidata ya wanachama kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa. Alisisitiza kwamba mfumo huo uko katika hatua nzuri na muda wowote mwaka huu utazinduliwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live