Uamuzi wa kesi ya wabunge 19 wa Viti Maalumu waliofukuzwa uanachama katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), unatarajiwa kutolewa na Jaji Cyprian Mkeha, Mahakama Kuu Masjala Kuu, leo Desemba 14, 2023 kuanzia saa nane mchana.
Halima Mdee na wenzake 18 wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022 wa kutupilia mbali rufaa walizokata wakipinga Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua uanachama, Novemba 27, 2020.
Walivuliwa uanachama wakidaiwa walienda kuapishwa kuwa wabunge wa Viti Maalumu bila kupendekezwa wala ridhaa ya Chadema.
Uamuzi wa Mahakama ndiyo utakaotoa hatima ya uhai wa uanachama wao kama unakoma rasmi au wataendelea kuwa nao ijapokuwa nao unaweza kuwa ni wa muda mfupi.
Iwapo Mahakama itakubaliana na madai yao kuwa rufaa zao zilitupiliwa mbali bila kupewa haki ya kusikilizwa, basi Mahakama itatengua uamuzi wa Baraza Kuu na inaweza kuelekeza rufaa zao zisikilizwe upya na wapewe haki ya kusikilizwa; lakini kama Mahakama itatupilia mbali hoja zao basi uanachama wao utakuwa umekoma rasmi na vivyo hivyo ubunge wao.