Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DED, ofisa tawala wajitosa kumrithi Profesa Majimarefu

10910 DED+PIC TanzaniaWeb

Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Korogwe. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, John Shari na Ofisa Tawala wa wilaya hiyo, Michael John ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kurithi nafasi ya ubunge wa Korogwe Vijijini iliyoachwa na marehemu Stephen Ngonyani ‘Profesa Majimarefu’.

Profesa Majimarefu alifariki dunia Julai 2, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Mbali na wagombea hao, pia yumo Thomas Ngonyani, mtoto wa Majimarefu ambaye pia ni diwani wa Kata ya Kilole iliyopo Korogwe.

Orodha ya wagombea 44 wanaowania nafasi hiyo kutoka chama hicho pia inamhusisha Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini, Nassoro Hemed ‘Malingumu.’

Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini, Suraiya Kangusu alisema jana kuwa makada wao 44 tayari wamerudisha fomu za kuomba kuteuliwa.

Kangusu aliwataja wengine waliorejesha fomu za kuwania ubunge huo kuwa ni John Nyika, aliyewahi kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia Mkoa wa Tanga na madiwani wengine wawili.

Aliwataja madiwani hao mbali na Thomas kuwa ni Seif Hillary wa Kata ya Mashewa na Shebila Iddi Shebila wa Kerenge. Uchaguzi wa marudio katika Jimbo la Korogwe Vijijini unatarajiwa kufanyika Septemba 16 pamoja na ule wa udiwani katika kata 21 za Tanzania Bara.

“Makada wengine waliorejesha fomu kuomba ridhaa ya CCM kuingia katika kinyang’anyiro hicho ni Allan Bendera, Kallaghe Yusuph, Lucy Mganga, Mwanaidi Kihamia, Hemed Chanika na Issa Kiango,” alisema Kangusu. Wengine ni Bendera Shekigenda, Rose Jally, Ramadhani Mohamed, Dk George Kinyashi, Yahaya Calamba na Shwaibu Mwanyoka.

Timotheo Mzava, Dk Dominic Muya, Dk Peter Mfumya, Ally Hoza, Hussein Ramadhani, Richard Kuyangana, Zakaria Mnkai, Raymond Mndolwa, Yusuph Chambo, Salimini Shempasi na Ahmad Gao.

Wengine ni Pernest Kimaya, Hassan Mathias, Privanus Simon, Stephen Shetui, Profesa Cathbert Mhilu, Adam Mwakajitu, Kimea Kisaka, Shelai Kanyawana, Japhari Kizumba, Hamad Dege, Ismail Mbwana, Machimbuko Zuakuu, Richard Rwizile na Constantine Daffa.

Katibu huyo aliwataja waliochukua fomu na ambao hadi muda uliopangwa hawakujitokeza kuzirejesha kuwa ni Diwani wa Magoma, Aweso Mandondo; Hadija Mshahara na Hoza Shehoza.

Kangusa alisema mchakato utakaofuata ni wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini kukutana leo kupiga kura za maoni kwa wagombea waliojitokeza.

“Baadaye vitafanyika vikao vya uchambuzi kabla ya majina hayo kupelekwa (vikao vya CCM) ngazi ya Mkoa wa Tanga,” alisema.

Alisema, “Katika mkutano wa kura za maoni utakaofanyika kesho (leo) tumeagiza kila aliyerejesha fomu aje mwenyewe na siyo kutuma mwakilishi kwa sababu huu ni mchakato muhimu katika chama chetu.”

Mbali na Korogwe Vijijini, pia uchaguzi huo utafanyika katika Jimbo la Ukonga lililokuwa likiongozwa na Mwita Waitara aliyehamia CCM kutoka Chadema na Monduli lililokuwa chini ya Julius Kalanga (Chadema), aliyerejea CCM. Waitara ameshachukua fomu kuwania tena kiti hicho kwa tiketi ya CCM.

Chanzo: mwananchi.co.tz