Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DED awakwaza wajumbe wa mkutano wa CCM, DC amwombea radhi

77296 Pic+ded

Wed, 25 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga (DED) mkoani Kilimanjaro Zefrin Lubuva leo Jumatano Septemba 25, 2019 amejikuta katika wakati mgumu katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kulazimika kuombewa radhi baada ya kutoa majibu ambayo yalidaiwa  kuwakwaza na maudhi.

Kikao hicho cha kujadili utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/20, mkurugenzi huyo alitakiwa kutoa majibu kuhusu fedha za mradi wa Mchanga katika kijiji cha Kifaru na ujenzi wa kituo cha Afya Kifaru ambapo alieleza hawezi kuyatoa kwa kuwa ni ya kitaalamu na yangehitaji  majibu ya kina.

Kauli ya mkurugenzi huyo iliibua mjadala mkubwa na baadhi ya wajumbe wa kikao hicho kudai mbali na kumdharau mkuu wa mkoa ameidharau halmashauri kuu na kumtaka abadilike.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema majibu ya mkurugenzi yamewakwaza wajumbe na kumtaka kutambua amepewa nafasi hiyo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

"Kama kazi hii ni nzito sana, wewe mtu mzima unajipima tu, kwani unapaswa kufanya kazi yako kama mkurugenzi na wewe ndiye msimamizi wa shughuli zote za halmashauri, tatizo ubishi na hapa hatuko kubembelezana,” alisema Boisafi

"Majibu uliyoyatoa mkurugenzi, sikuyategemea hapa, yamekuwa si rafiki na mwanzoni nikizungumza nilisema tunahitaji umoja na mshikamano na sisi hapa tumekaa kwa ajili ya wengi na mmepewa dhamana kwa sababu mlionekana mnafaa."

Pia Soma

Advertisement
Mwenyekiti huyo alisema, "usitoe majibu kama unaongea na watu wasiofaa, toa majibu yanayofanana na watu hawa hapa, kwani tuliwaita pamoja na wataalamu, kwa sababu tunajua Mkuu wa Mkoa hawezi kujua mambo yote," alisema

"Mkurugenzi umewakwaza wajumbe wa kikao na watumishi wengine na hiyo si staili ya majibu, umepewa madaraka, tafuta njia ya kujibu watu na kwa haki, kwani kazi unazofanya si za kwako bali ni za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wewe ni mwakilishi tu," aliongeza

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson ameomba radhi kwa kauli aliyoitoa Mkurugenzi  na kueleza wao kama serikali wapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kwamba walipata nafasi hizo baada ya chama kushinda.

Amesema suala la Kifaru tayari wameanza kulishughulikia na kuahidi wanaendelea kulifuatilia na watatoa majibu sahihi pindi watakapolikamilisha.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga, Jafari Kandege alisema katika wilaya hiyo kuna shida na kuomba Halmashauri kuu kuona namna ya kuwasaidia ili kuweza kufanya kazi kwa umoja na kuyafikia yale yaliyokusudiwa.

"Hali ya Mwanga ni tete, tunaomba halmashauri kuu itusaidie kwani nafasi na kutupatia ufumbuzi kwani suala hili linatupa wakati mgumu na kutufanya tufanye kazi katika mazingira magumu," alisema

Chanzo: mwananchi.co.tz