Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Bariadi azuia mkutano wa ndani Chadema

23325 Dc+pic TanzaniaWeb

Mon, 22 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkutano wa Chadema uliopangwa kufanyika leo Jumapili Oktoba 20, 2018 wilayani Bariadi mkoani Simiyu umeshindwa kufanyika baada ya kuzuiwa na mkuu wa wilaya hiyo, Festo Kiswaga.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema mkutano huo ulikuwa ufanyike katika Ukumbi wa KKKT lakini katika hali ya kushangaza polisi wameupiga marufuku bila kutoa maelezo ya kina.

Amesema mkutano huo wa ndani ulikuwa ufanyike kwa ajili ya kupanga mikakati ya kufanikisha chaguzi zinazotarajiwa kufanywa hivi karibuni na kitendo cha polisi kuuzia kimewasikitisha.

“Tumeambiwa mkuu wa wilaya ndiye aliyetoa amri mkutano wetu usifanyike. Kama hiyo haitoshi gesti ambazo zilikuwa zimechukuliwa kwa ajili ya kuwahifadhi wageni wetu nazo pia zimezuiliwa.”

“Tunashangaa sana namna viongozi wanavyotumia vibaya madaraka maana huu ni mkutano wa ndani na unafanyika kama katiba inavyoelekeza, tumepata hasara kwa maana hiyo tunakusudia kumchukulia hatua za kisheria huyu mkuu wa wilaya kama yeye binafsi,” amesema.

Amesema kutokana na zuia hilo, chama hicho sasa kimeamua kufanya mkutano huo wilayani Shinyanga.

“Mkutano wetu unafanyika leo Shinyanga na kesho viongozi wetu wataanza kusambaa katika majimbo mbalimbali kwa ajili kufanya mikutano ya ndani,” amesema.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kiswaga amesema hakuzuia mkutano huo bali alikubaliana na baadhi ya viongozi wa chama hicho wapange tarehe nyingine kwa vile wakati huu kulikuwa na maandalizi ya shughuli nyingine ikiwemo ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz