Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Cuf wanusa kuchezewa rafu uchaguzi wa serikali za mitaa

Cuf wanusa kuchezewa rafu uchaguzi wa serikali za mitaa

Thu, 31 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Chama cha Wananchi (Cuf) kimesema hali inayoendelea kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa ni kiashiria tosha ya uvunjifu wa amani nchi.

Makamu mwenyekiti wa Cuf Bara Maftaa Nachumu amewaambia waandishi wa habari leo Jumatano Oktoba 30,2019 kuwa kumeibuka ukiukwaji mkubwa wa kanuni katika maeneo mengi wapinzani wakinyimwa fomu za kugombea wakati wagombea wa CCM wanapewa kupitia mabalozi.

Maftaa alitolea mfano wa Wilaya ya Liwale kuwa siku nzima ya jana watendaji wa vijiji waliamua kufunga ofisi zao na kuondoka ili wapinzani wasiende kuchukua fomu za kugombea.

Oktoba 28, 2019 Waziri wa nchi ofisi ya Rais Seleman Jafo, aliwaagiza watendaji wa mitaa na vijiji kuacha shughuli zingine na kubaki na kazi moja ya utoaji fomu ili kuepusha malumbano.

“Hii ni aibu kubwa na dalili mbaya kabisa, jana ilikuwa siku ya kwanza lakini tayari wameanza figisu, sisi wa kwetu wananyimwa wakati wagombea wa CCM walipewa fomu tangu juzi usiku, safari hii hatukubali kabisa,” alisema.

Makamu huyo alisema Cuf kimeshatoa maagizo kwa wagombea wake nchi nzima kuweka kambi katika ofisi za watendaji na kudai haki zao bila woga kwani bilakufanya hivyo hali ya demokrasia itakuwa mbaya kwa Tanzania. Naibu Katibu Mkuu wa Cuf (Bara) Magdalena Sakaya alisema walikofikia sasa ni vema CCM kikajitafakari kwani kinatumia vyombo vya dola na watendaji kulazimisha kuwa kinapendwa.

Sakaya pia alitaja kinachoitwa ni mizengwe kwa wapinzani kwamba wanabambikiziwa kesi za ajabu ikiwemo zaidi ya wanachama wao 500 katika wilaya ya Bagamoyo ambao wamewekewa mapingamizi kuwa siyo raia wa Tanzania lakini ni mbinu za chama kilichoko madaraka katika maeneo wanayoona upinzani una nguvu.

Chanzo: mwananchi.co.tz