Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Cuf Maalim wafunguliwa milango kwa Lipumba

54708 CUF+pic

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF), Vedasto Ngombale amewaomba wabunge wengine wa chama hicho ambao bado wana misimamo, kurudi kwa mwenyekiti wao Profesa Ibrahim Lipumba ili wakijenge chama chao.

Ngombale alitoa kauli hiyo jana Jumatatu Aprili 29, 2019 katika viwanja vya Bunge la Tanzania alipoulizwa kuhusu ushiriki wake katika mkutano wa juzi ambao wabunge wa chama hicho waliitwa na Mwenyekiti wao Profesa Lipumba.

Awali mbunge huyo alikuwa miongoni mwa wabunge waliokuwa wanaunga mkono msimamo wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye amejiunga na chama cha ACT-Wazalendo.

Alikiri kuwa na msimamo usiomuunga mkono Profesa Lipumba wala Maalim Seif katika kipindi cha mgogoro kwani aliamua kubaki kati baada ya kujaribu kufanya usuluhishi kwa viongozi hao na kushindikana

“Ni kweli nilikuwa na msimamo wa kutokumuunga mkono  yeyote kati yao, lakini nilikubaliana na uamuzi wa mahakama hivyo nikaamua kurudi kwa Lipumba na juzi aliniita nikaenda pamoja na wabunge wengine,” alisema

Akizungumzia kilichojiri katika mkutano huo alisema, walizungumza vitu vya kawaida visivyokuwa vya siri na kikubwa ni namna bora ya kukijenga Cuf lakini pendekezo la uteuzi wa wakurugenzi.

Kwa upande wake mbunge wa Malindi (CUF) Ali Saleh alisema ni mapema kuzungumzia kwa kutoshiriki kwake katika mkutano wa juzi lakini akasema yeye ni mwanachama wa CUF si vinginevyo.

“Kwa leo siwezi kuzungumza lakini wewe unajua mimi ni mbunge kupitia chama cha Cuf, aamini hilo ila ukifika wakati ukanitaka kusema nitasema ilimradi isiwe leo,” alisema Saleh.

Mbunge wa Chambani (CUF), Yusufu Salim Hussein alikataa kuzungumzia chochote kuhusu kutokuwa katika orodha ya wabunge walioshiriki kwenye mkutano wa mwenyekiti wao.



Chanzo: mwananchi.co.tz