Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chozi la Naibu Waziri laiibua CCM

Byabato Chozi Maswali.png Chozi la Naibu Waziri laiibua CCM

Wed, 18 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

akati mbunge wa Bukoba Mjini, Steven Byabato (CCM) akimwaga chozi jukwaani akidai baadhi ya watu wanamkwamisha jimboni kwake, uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukoba umemtaka kuwasilisha malalamiko yake vikaoni badala ya kulalamika kwenye majukwaa.

Byabato, naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, juzi alipiga magoti mchangani mbele ya wakazi wa jimbo hilo, huku akizungumza kwa hisia kali kutokana na alichokiita hujuma kwenye ubunge wake.

Kufuatia tukio hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba, Joas Zachwa, aliyezungumza na Mwananchi, alisema chama hicho kina kanuni na taratibu za viongozi na wanachama wake huwasilisha malalamiko na hoja zao kwa ajili ya kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi na si kusema mitaani.

“Mimi ndiye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba…naongoza vikao vyote vya kimaamuzi kuanzia kamati ya siasa, halmashauri na mkutano mkuu wa wilaya ambavyo pamoja na mambo mengine, ndivyo hujadili, kupitisha na kufuatilia utekelezaji wa ilani na miradi ya maendeleo. Hakuna malalamiko ya mbunge kukwamishwa,” alisema Zachwa.

Mwenyekiti huyo alisema hadi sasa, utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Jimbo la Bukoba mjini unaendelea bila mkwamo na alitaja miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na stendi kuu ya mabasi mjini Bukoba kuwa mfano hai.

“Miradi ya maendeleo inatekelezwa na hakuna anayekwamisha. Kwa mfano, wapo wananchi ambao nyumba zao zinatakiwa kubomolewa kupisha upanuzi na ujenzi wa barabara ambao wameanza kubomoa nyumba zao kwa hiari…tena wengine hata hawajalipwa fidia. Sasa hapo kuna kumkwamisha mbunge?’’ alihoji Zachwa.

Mwenyekiti huyo alisema hata utoaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo jimbo la Bukoba Mjini unafanyika kwa wakati na akataja zaidi ya Sh3.1 bilioni za mradi wa stendi na zaidi ya Sh1 bilioni za kupanua barabara na kona ya Nyangoye kuwa mfano.

“Eneo pekee lenye manung’uniko kutoka kwa wananchi ni suala la fidia kwa baadhi ya mali na nyumba zinazotakiwa kupisha miradi ya barabara. Hili linafanyiwa kazi na chama kwa kushirikiana na Serikali na tayari baadhi ya wananchi wameanza kubomoa nyumba zao wenyewe,” alisema kiongozi huyo.

“Kiongozi hakosei wala kukosolewa hadharani hata akikosea. Hivyo, ninachoweza kusema kwa sasa ni kumshauri mbunge na kiongozi yeyote mwenye hoja au malalamiko kuyawasilisha kwenye vikao vya kikatiba na kikanuni ili yajadiliwe na kuamuliwa,” alisisitiza.

Mwananchi lilipomtafuta Byabato kwa simu ili afafanue madai yake, alisema “naomba nilichokizungumza na kinachozunguka kupitia kwenye mitandao ya kijamii kibaki hivyo hivyo...sitaki kuongeza lolote kukwepa yale ninayoyalalamikia.”

Alisema katika kukwepa kuibua mambo makubwa zaidi ndiyo maana hakutaja majina ya wahusika, miradi inayokwamishwa na namna inavyokwamishwa.

“Kwenye macho ya kawaida, miradi ya maendeleo jimbo la Bukoba inaonekana inatekelezwa...lakini tunayokumbana nayo huko ndani, sisi ndio tunayajua,” alisema Byabato, akisisitiza kutozungumzia suala hilo kwa undani.

Kilio cha mbunge

Lakini akizungumza juzi wakati wa hafla ya uzinduzi na kukabidhi kwa mkandarasi mradi wa ujenzi na upanuzi wa stendi mjini Bukoba, Byabato alidai kuna watu wanamkwamisha katika jitihada zake za kutekeleza miradi ya maendeleo jimboni humo.

Akiwa amepiga magoti mbele ya umati wa wananchi, viongozi wa Manispaa ya Bukoba, CCM na Serikali, Byabato alijikuta sauti yake ikianza kutetemeka mithili ya mtu anayetaka kuangua kilio, hali iliyowalazimu baadhi ya viongozi kutoka meza kuu kwenda kumtuliza na kumnyanyua.

Byabato, aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza kuwakilisha jimbo hilo mwaka 2020, amewahakikishia wananchi kuwa ataendelea kutekeleza bila hofu majukumu yake ya kibunge, ikiwemo kusukuma utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hata kama kwa kufanya hivyo kutamfanya akose ubunge katika uchaguzi mwaka 2025.

“Mimi ubunge sikuzaliwa nao…nautaka, naupenda na nitautumikia kufa na kupona. Mmenipa miaka mitano, mnisaidie niukamilishe. Mkiniona nafaa nipeni tena na mkiona sifai sawa. Lakini ninachoahidi sitaacha kufanya (shughuli za maendeleo) eti nitakosa ubunge. Kama naukosa ubunge 2025 kwa sababu stendi imejengwa Bukoba mjini, niko tayari,” alisema Byabato.

Aliongeza “kama kufanya stendi nzuri iwepo Bukoba mjini itanifanya niukose ubunge (mwaka) 2025, sawa. Ubunge waninyime, stendi ipo, mtanikumbuka.”

Bila kutaja wanaomkwamisha na jinsi anavyokwamishwa, mbunge huyo aliongeza kuwa “hii Bukoba ni ya kwetu sote, tusaidiane tuipeleke mbele tumechelewa, maneno yanakwaza na yataturudisha nyuma.”

Huku akiendelea kulalamikia kukwamishwa, mbunge huyo aliuomba umma wa wana Bukoba kumuunga mkono katika jitihada za kusukuma gurudumu la maendeleo ya jimbo hilo badala ya hali ya sasa ya baadhi kumkwamisha.

“Mimi nawaomba ndugu zangu, tusaidiane tusogeze Bukoba yetu mbele, tusikwamishane. Hizi kazi nafanya siyo zangu, ni kazi zenu ninyi mmenituma.Kwa nini unikwamishe?” alihoji Byabato akiwa amepiga magoti mbele ya wananchi.

Akizungumzia malalamiko ya mbunge Byabato, Juliana Samson, mkazi wa Rwamishenye alisema kuna uwezekano ama ni kweli wapo wanaofanya hivyo au hakuna, bali madai hayo yanachangiwa na joto la uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Wanasiasa wana mambo yao ya kisiasa, ni vigumu sana kukataa au kukubali malalamiko ya mbunge, ninavyoweza kusema ni kuwashauri viongozi wa kisiasa kuanzia wenyeviti wa mitaa, madiwani na wabunge kila mmoja atekeleze wajibu wake. Masuala ya uchaguzi tutaamua sisi wapigakura kutegemeana na utendaji wao,” alisema Juliana.

Redemptus Muganyizi, mkazi wa Hamugembe alisema kiuhalisia kama kuna kumkwamisha, basi mbunge Byabato atakuwa anakwamishwa na viongozi wenzake, kwa kuwa upande wa wananchi hakuna yeyote anayepinga utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo upanuzi na ujenzi wa barabara eneo la kona ya Nyangoye na Rwamishenye. “Kuna watu wameishi maeneo hayo zaidi ya miaka 30 na wameanza kubomoa wenyewe nyumba zao, licha ya kuambiwa ni nyumba 25 pekee ndizo zitakazofidiwa,” alisema Muganyizi.

Miradi inayotekelezwa

Pamoja na ujenzi wa Stendi Kuu ya Bukoba utakaogharimu zaidi ya Sh3.1 bilioni, miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa mjini Bukoba inayoambatana na ulazima wa baadhi ya nyumba na makazi ya watu kubomolewa ni upanuzi wa eneo korofi la barabara kwenye kona ya Nyangoye, Mtaa wa Hamugembe.

Licha ya kuwa finyu, eneo la kona kali ya Nyangoye pia kuna mteremko mkali unaosababisha ajali za barabarani zinazosababisha vifo na majeruhi kila mara.

Ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Bandari ya Bukoba hadi mzunguko wa Barabara ya Rwamishenyi ni mradi mwingine unaotekelezwa ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Kagera, nyumba 42 pekee ndizo zitafidiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live